• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mkutano wa kilele wa G20 wafikia makubaliano kuhusu masuala ya biashara, uchumi na uwekezaji

    (GMT+08:00) 2020-11-23 16:46:14

    Mkutano wa 15 wa kilele wa kundi la nchi 20 (G20) ulifanyika kuanzia Jumamosi hadi Jumapili kwa njia ya video. Naibu mkurugenzi wa kitengo cha masuala ya kimataifa cha Wizara ya Biashara ya China Bw. Chen Chao amesema mkutano huo kufikia makubaliano kwenye masuala mbalimbali muhimu ya biashara, uwekezaji, fedha, uchumi wa kidijitali na afya ya umma, kumeonesha imani thabiti ya nchi wanachama wa G20 katika kukabiliana na changamoto kwa pamoja, na kutia msukumo mkubwa kwenye kuhimiza ufufuaji wa uchumi wa dunia.

    Naibu mkurugenzi wa kitengo cha masuala ya kimataifa cha Wizara ya Biashara ya China Bw. Chen Chao amesema, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara ni moja ya nguzo muhimu za G20. Kutokana na juhudi za pamoja zilizofanywa na nchi wanachama, mkutano huu wa kilele umepata matunda makubwa kwenye fani mbalimbali za sekta ya uchumi na biashara. Anasema,

    "Kwanza ni kuidhinisha hatua za pamoja za G20 za kukabiliana na janga la virusi vya Corona na kuunga mkono biashara na uwekezaji duniani, nchi wanachama wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika mambo manane yakiwemo kuimarisha uratibu wa sera, kuongeza urahisishaji wa biashara, kuhimiza uwekezaji wa kimataifa na kuondoa vizuizi kwenye mtandao wa uchukuzi na ugavi, na kupitisha hatua 38 halisi za ushirikiano. Pili ni kufikia makubaliano muhimu ya kulinda utaratibu wa biashara ya pande nyingi, kufikia Azimio la Riyadh kuhusu mustakbali wa WTO, kusisitiza tena malengo na kanuni za WTO, na kusukuma mbele mageuzi ya lazima ya shirika hilo. Tatu ni kuahidi kudumisha uwazi wa soko, kuhakikisha ushindani wa haki na kuweka mazingira ya kibiashara yanayotabirika yenye haki na usawa, yaliyo shirikishi, wazi na tulivu na bila ubaguzi. Nne ni kuahidi kuongeza kiwango cha uendelevu na ustahimilivu wa mnyororo wa ugavi duniani, na kuzisaidia nchi zinazoendelea na zilizo nyuma zaidi kimaendeleo kujiingiza vizuri kwenye biashara ya kimataifa. Tano ni kuweka mwongozo wa sera, kuhamasisha mashirika madogo na yenye ukubwa wa kati kujishughulisha zaidi kwenye biashara na uwekezaji wa kimataifa, ili kuhimiza ukuaji shirikishi wa uchumi."

    Bw. Chen Chao amesema, G20 ni mwakilishi wa nchi zenye uchumi mkubwa zaidi duniani, ambazo zinachangia asilimia 86 ya uchumi wa dunia na zinachukua asilimia 65 ya watu wote duniani. Katika miaka 12 iliyopita, utaratibu wa mikutano ya kilele ya G20 ulianzishwa kwa lengo la kukabiliana na msukosuko wa kifedha duniani. Katika siku ya leo, jamii ya kimataifa inakabiliwa tena na changamoto ya pamoja na utatuzi wake unalihitaji kundi la G20 lichukue tena nafasi ya uongozi katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, ili kulishinda kwa pamoja janga la virusi vya Corona na kusukuma mbele maendeleo ya uchumi.

    "China inapenda kushirikiana na nchi wanachama wote wa G20, kutekeleza kwa kina makubaliano muhimu yaliyofikiwa kwenye mkutano huu wa kilele, kuendelea kuunga mkono kithabiti mfumo wa pande nyingi na biashara huria, kupinga sera za kujilinda kibiashara na hatua za upande mmoja, ili kudumisha utulivu kwenye minyororo ya viwanda na ugavi duniani, kuzisaidia na kuziunga mkono nchi zinazoendelea, kusukuma mbele ufufukaji endelevu na shirikishi wa uchumi wa dunia, na kutekeleza kivitendo dhana ya jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako