• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Jengo linalohamahama laoneshwa na Ureno katika Maonesho ya Kimataifa ya Shanghai

    (GMT+08:00) 2010-06-21 18:06:43

    Ukitembelea katika eneo la uzoefu mzuri wa kuendeleza miji UBPA (Urban Best Practices Area) la Maonesho ya Kimataifa ya Shanghai, utaona jengo la mbao lenye ghorofa 3, na jengo hilo linaloitwa "Mnara wa Utalii Unaohamahama" ni mradi unaooneshwa na Ureno kwenye eneo hilo la Uzoefu Mzuri wa Kuendeleza Miji la Maonesho ya Kimataifa ya Shanghai.

    Jengo hilo la mita 9 linachukua eneo la mita 10 tu za mraba. Jengo hilo linasanifiwa na Bw. Jose Manual Pequeno, ambaye ni profesa wa elimy ya ujenzi katika Chuo Kikuu cha Minho cha Ureno. Bw. Pequeno amemwambia mwandishi wetu wa habari kuwa mnara huo unajengwa kwa mbao na vioo, na kujenga mnara huo si kazi kubwa, inachukua wiki moja tu, kwa kuwa sehemu mbalimbali za mnara huo zikiwemo kuta na madirisha zilitengenezwa awali viwandani na kuwa tayari, kinachotakiwa kufanywa ni kuunganisha tu sehemu hizo.

    "Kujenga mnara huo ni kuunganisha sehemu mbalimbali zilizotengenezwa awali, na mnara huo unaweza kuhamishwa, unaweza kutumiwa kama hoteli kwenye maeneo ya vivutio vya utalii, pia unaweza kutumiwa kama nyumba ya mtu binafsi. Mnara huo una kila kitu kilichopo kwenye nyumba ya kawaida, na kutokana na udogo wake, ni rahisi kuunganisha, kutenganisha na kusafirisha."

    Katika ghorofa ya kwanza ya mnara huo, kuna jiko na bafu, na ndani ya jiko, kuna vifaa vya kupikia, sehemu ya kuosha vyombo, na chombo cha kuvuta moshi; katika ghorofa ya pili, kuna sofa na meza; na ghorofa ya tatu ina chumba cha kulala na msala. Bw. Pequeno amefahamisha kuwa mnara huo unatosha kwa watu wawili, kwa mfano mume na mke. Na jambo linalowafurahisha watu zaidi ni kwamba mnara huo pia una kibaraza.

    Bw. Pequeno amefahamisha kuwa wakati aliposanifu jengo hilo alichofikiri ni kuliweka kwenye sehemu za vivutio vya utalii, hivyo vitu alivyotumia kutengenezea jengo hilo havichafui mazingira, kwa hiyo jengo hilo linafaa kutumiwa kwenye maeneo ya hifadhi, sehemu za vivutio vya utalii na sehemu nyingine ambapo haifai kufanya ujenzi mwingi.

    "Tunaweza kuweka mnara huo kwenye eneno la hifadhi au vivutio vingine vya utalii, wazo la kiujenzi la usanifu wa mnara huo ni kutochafui mazingira, na ujenzi wake si kazi kubwa. Hivi sasa watu wanapenda maisha yenye utulivu, wanataka kuishi katika mazingira ya asili, na mnara huo unaweza kukidhi mahitaji kama hayo."

    Ukubwa na muundo wa mnara huo unategemea mahitaji ya wateja, uwe mkubwa au mdogo, uwe mmoja mmoja, miwili miwili, au minne minne. Mnara huo hauna mfumo wa maji na umeme kama ilivyo nyumba ya kawaida, lakini je, umeme na maji yake yanatoka wapi? Bw. Pequeno amefahamisha akisema:

    "Kuna njia 3 za kupata maji na umeme. Ya kwanza ni ya kawaida yaani kujiunganisha na mfumo wa umeme na wa maji wa sehemu iliyopo; ya pili na ya tatu ni njia za kujitegemea, unaweza kuchimba shimo pembeni mwa mnara, na kuweka jenereta, bwawa la maji na chombo cha kusafisha maji, lakini katika eneo la hifadhi, ambapo hairuhusiwi kuchimba shimo kwenye ardhi, basi tunapendekeza wateja wanunue minara kadhaa, kwa mfano minara mitano, na minne kati yao inatumiwa kama makazi, na mmoja mwingine unatumiwa kwa ajili ya utoaji wa umeme na maji, hivyo mazingira ya asili ya eneo la hifadhi hayataharibiwa."

    Hivi sasa jengo hilo halijaanza kuzalishwa kwa wingi, kwa hiyo bei yake bado ni kubwa, ambayo ni Euro elfu 85. Msanifu huyo anatarajia kutumia fursa ya Maonesho ya Kimataifa ya Shanghai kutangaza uvumbuzi wake huo, na ana matumaini kwamba katika siku za usoni mnara huo unaweza kuzalishwa kwa wingi, na gharama yake itapungua. Kwa kweli kwenye maonesho hayo watalii wengi wamevutiwa na mnara huo, na kumwuliza msanifu Bw. Pequeno maswali mengi kuhusu mradi wake.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako