Mimi ninaitwa Evance Joseph Mhando (Mr Names) watu wananiita Mr Names kutokana na kuwa na majina mengi na jina hili lilianzia shule ya secondary Boza huko Pangani Tanga (Kaskazini mashariki kwa Tanzaia) mwishoni mwa miaka ya 1990 wakati nikisoma kwenye shule hiyo nikipata elimu yangu ya Sekondari.
Mimi ni mfanyakazi wa shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambae kwa sasa nipo hapa nchini China, ambapo nilijiunga na shirika hilo mwaka 2004 wakati huo likiwa Taasisi ya Utangazaji Tanzania (TUT) kama mwandishi na mtangazaji.
Toka kipindi hicho nimekuwa nikifanya kazi mbali mbali kwenye shirika hilo za uandishi,Utangazaji na uandaji wa vipindi mbali mbali hasa vipindi vya michezo.
Wasikilizaji wengi wa Radio na watazamaji wa Television nchini Tanzania wananijua zaidi kwenye vipindi vya michezo hasa kwenye Radio ya Taifa (TBC Taifa) kipindi ambacho kinarushwa mida ya saa 1:30 usiku kila siku ambapo nilikuwa mmoja wawatangazaji na waandaji wa kipindi hicho toka mwaka 2005.
Pia mie ni mtangazaji wa mpira miguu kwa Radio na Television hasa Radio mara nyingi, kazi ambayo nilianza kuifanya mwaka 2006 hivyo nimetangaza michezo mingi ya soka toka mwaka 2006 ya nchini Tanzania kuanzia ngazi ya vilabu hadi timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) mmoja ya michezo mikubwa niliyotangaza ni kati ya Taifa Stars Vs Senegal mwaka 2007 huko Dakar ,Senegal kwenye uwanja wa Leopold Sedar Senghor mchezo wa kuwania kufuzu kwa michuano ya mataifa ya Africa ya 2008 ambapo Taifa Stars ilifungwa mchezo huo kwa bao 4- 0,Taifa Stars na Ivory Coast mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na mmoja ya mechi ngumu za Tanzania ya ngazi ya klabu ya watani wa jadi wa soka la Tanzania , Simba na Yanga.
Kabla ya kuja China nilikuwa ni Muandaji, Mtangazaji na Mwandishi wa habari za michezo wa TBC (TV na Radio) Pia nilikuwa naandaa na kutangaza kipindi kiitwacho ASUBUHI HII YA MWISHONI MWA JUMA ambacho kilikuwa kinatangazwa kila jumapili ya mwisho wa juma kuanzia saa 12:00 - 2:00 asubuhi kupitia Radio ya Taifa (TBC Taifa), na kilihusu maswala ya asili ya Tanzania pamoja na mila zake.
Kusema kweli kipindi hicho cha mwishoni mwa juma cha kila Jumapili ndio nilikuwa kipindi bora kwangu kuliko vipindi vyote nilivyokuwa ninafanya TBC wakati huo,nilikuwa ninakipenda na ninadhani hadi sasa bado kipo imara.
Nimekuja hapa nchini China kwaajili ya kusoma na kwa sasa ninasoma lugha ya kichina kwenye Chuo Kikuu cha Kawaida cha Huazhong kilichopo Wuhan kwenye jimbo la Hubei China. Kwa kweli kichina ni moja ya lugha nzuri ila kazi ya ziada inahitajika kuweza kukijua maana ni lugha tofauti mno na ile lugha ya Kiswahili niliyoizoea mie kule nchini kwangu Tanzania.
Toka nije hapa nchini China nina kama miezi miwili hivi, ninajua kidogo kuongea kichina kama salamu na kuuliza kitu,salamu kubwa hapa ni Ni hao ambayo karibu kila mtu anaijua,nitafurahi sana siku ambayo nitakuja kuongea vizuri lugha ya Kichina mbayo ninadhani itanisaidia sana kwenye kazi zangu za uandishi wa habari na Utangazaji.
Baada ya kumaliza kusoma lugha ya kichina hapa Wuhan June 2011 nitaenda kwenye chuo cha Nanchang University kwaajili ya kusoma masomo yangu ya Uandishi wa habari ambayo nitayasoma kwa lugha ya kichina kwa kipindi cha miaka minne hivi hivyo nitakuwa kwenye aridhi hii ya China kwa kipindi cha miaka mitano Mungu akijalia.
Mimi ni mpenzi mkubwa wa mpira wa miguu (soccer) kuanzia soka la Tanzania,Africa mashariki, Africa nzima na duniani kote,ni shabiki mkubwa wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Satrs) pia ninaipenda sana Chelsea ya England. Kwa sasa sina timu ninayoipenda nchini Tanzania kutokana na timu zenyewe kutokuwa na muelekeo mzuri kama klabu kubwa za Simba na Yanga ambazo zimepoteza dira ya soka. Pia ninapenda mchezo wa Netball kwasababu mama yangu mzazi Upendo Chilundu alikuwa anacheza wakati wa ujana wake na mie nilikuwa nikienda nae uwanjani wakati huo na hicho ndio chanzo cha mimi kupenda michezo.
Mimi ni mwongeaji sana na mara nyingi ninapenda sana kuongea kuhusu michezo na maisha kwa ujumla na hapa China mara nyingi ninapenda kuongelea habari za nyumbani Tanzania na bara la Africa kwa ujumla.
Pia ni mdadisi. Ninapenda kujua mambo mbalimbali, hivyo mara nyingi nimekuwa mtu wa kusikiliza Radio (wakati nilipokuwa Tanzania) hapa China ninashindwa kusikiza Radio kwa sasa kwasababu lugha kidogo wanayotumia kwenye kutangaza inanitatiza kufanya hivyo, Pia ninapenda kuangalia TV hasa vipindi vya habari na makala mbali mbali.
Pia ninapenda sana kuchat na watu mbali mbali kwenye mitandao kama kwenye simu ya mkononi ,Facebook,Yahoo, Yahoo messenger na hapa China kuna mtandao unaitwa QQ. Ninapenda sana kutembea na kujua sehemu nyingi ila sipendi kufahamika sana na watu na hicho ndicho kinasababisha nisipende kutangaza kwenye TV ingawa ninafanya hivyo pale inapohitajika na sipendi watu waniweke kwenye kundi fulani au mtu wa aina Fulani, mi ni mtu wa kawaida sana, waweza sema simple man.
Ninapenda sana kula hilo siwezi kuficha, hasa chakula kizuri, na mara nyingi nikiwa nyumbani Tanzania ninapenda kula ugali na samaki au ugali na dagaa na wakati mwingine wali japo si sana. Kupenda kwangu kula ugali na samaki au dagaa kulinifanya karibu kila weekend (mwishoni mwa juma) kwenda nyumbani kwa mama yangu mzazi maeneo ya Mbezi Louis nje kidogo ya jiji la Dar es salaam kama kilometa 20 hivi toka kati kati ya jiji kula hicho chakula na hadi sasa bado ninaamini kuwa mama yangu ni moja ya watu wanaojua sana kupika, sijui mke wangu atakuwaje! Ila hapa China ugali hakuna hivyo ninamiss kitu muhimu mno kwenye maisha yangu na chakula changu kikubwa hapa China ni mifani (wali) na kuna baadhi ya yakula vya hapa vimenishinda kabisa kuvila.
Sina mke wala mtoto kwa sasa ila nipo kwenye mahusiano ya kimapenzi na binti mmoja wa Kitanzania ambae yupo nyumbani Dar es salaam na Mungu akipenda ndie atakuja kuwa mke wangu wakati wowote kuanzia sasa (Nina mmiss sana Mama Nancy) ninamuita mama Nancy kwasababu ninapenda sana mtoto wa kike na ninaomba Mungu anijarie nipate na jina lake litakuwa Nancy.
Mwisho mie ni mtu ambae ninajuana na watu wengi sana wa ndani ya Tanzania na njee ya Tanzania tena wa lika tofauti tofauti kuanzia vijana hadi watu wazima.
Kwa ufupi huyo ndio Evance Joseph Mhando (Mr Names) kijana wa Kitanzania ambae kwa sasa anaishi Wuhan China.
| © China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |