
Sikukuu ya Christmas au Noel kwa lugha yangu ya Kiswahili ni maarufu kila kona hapa na duniani. Hapa nchini China sikukuu hii inaitwa Shengdanjie. Wenyeji wangu wamenifahamisha kuwa Wachina wengi hawasherehekei sikukuu hii, kwa wana sherehe yao inayokuja mwezi Januari 2011 ambayo ni kubwa zaidi, lakini vijana wa China hivi leo wanafurahia sana sikukuu hiyo, kila ifikapo sikukuu hiyo wanakusanyika pamoja na kushiriki kwenye shughuli za sikukuu, ingawa ni tofauti kidogo na zile za wakristo. Kwa Wakristo sikukuu hii ni kubwa mno, kwa maana ni kumbumbuku ya kuzaliwa kwa mkombozi wao Yesu Kristo ambaye kwa mujibu wa imani hiyo alikuja kuwaokoa walimwengu.
Huko nyumbani (Tanzania) maandalizi makubwa yameshaanza, watu husafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kuungana na familia zao ili kusherehekea kwa pamoja sikukuu hii. Wachaga ni moja ya kabila ambalo watu wake wengi hupenda kurudi makwao pale inapofika sikukuu hii. Ingawa watu wa makabila mengine nao hufanya hivyo, lakini Wachaga ndio wanatia fora.
Kuna mamia kwa maelfu ya Waafrika wanaoadhimisha sikukuu hii wakiwa nje ya bara lao, na wanajua fika wakati kama huu kuna kitu wanakosa toka kwenye mizizi yao ya asili. Rafiki yangu mmoja kutoka Tanzania ambaye yupo hapa China aliniambia kuwa anakumbuka mlo wa pamoja akiwa na ndugu zake wakati wa sikukuu hii, kwenda Kanisani pamoja, na kutembelea ndugu, jamaa na marafiki. Anakiri kuwa wakati wa sikuku kama hizi ndio mawazo ya nyumbani yanazidi kuongezeka tofauti na wakati mwingine.
Barani Afrika sikukuu hii ni kubwa mno, lakini viongozi wengi wa dini wanaona kuwa waumini wengi wameichukulia zaidi sikuku hii 'kidunia' na kuitoa maana yake halisi. Hivi sasa msimu huu kwa waumini hao ni kulewa pombe kupindukia na kufanya starehe zisizo na maana na kusahau maana na umuhimu wa sikukuu hii. Hilo ni kweli, maana katika sikukuu hii, waumini wengi wanajianda zaidi kimwili kuliko kiroho. Viongozi hao wanasema, ingawa wakati huu makanisa hujaa sana, wengi wa waumini wanaenda makanisani kutimiza wajibu na kuweka historia kuwa "Christmas ya mwaka fulani nilienda kanisani", sio kwa imani ya kweli inayotoka moyoni mwao kama ilivyokuwa katika miaka ya 80 ya karne iliyopita.
| © China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |