Kuna watu wengi hivi sasa wanaojifunza lugha hii wakiwa ndani ya China na wengine nje ya China na wengi wao wanaojifunza lugha hii ni kutoka kwenye mataifa ya nchi zinazoendelea hasa barani Afrika. Hii ni kutokana na nchi hiyo kujikita sana kwenye bara hilo kwenye mambo ya uwekezaji na kuongeza ajira.
Pamoja na hayo bado kuna baadhi ya watu wanaoamini kuwa lugha ya kichina ni ngumu lakini hilo sio tatizo kwa wale wanaosoma lugha hiyo na kugeuka kuwa walimu kwa kujaribu kuwafundisha baadhi ya ndugu zao au kuwashawishi kusoma lugha ya Kichina.
Vijana wengi wanaosoma luga ya kichina hapa kwenye mji wa Wuhan wanatumia njia za kisasa za mitandao kujaribu kuwafundisha baadhi ya ndugu zao lugha hiyo ya kichina kwa kuwapa ule mtazamo tu.
Wengi wao wanawafundisha watu wao wa karibu kama vile wapenzi wao, waume zao na wake zao watoto wao na rafiki zao wa karibu.
Njia kubwa inayotumiwa na wanafunzi hao kueneza lugha hii ya kichina ni mawasiliano ya moja kwa moja yaani kuchati kama kwenye facebook, badoo, yahoo messenger na njia ya kupiga simu za video ya skype ambayo inaonekana kushika kasi zaidi katika kutoa darasa hili.
Mwenzangu mmoja kutoka Tanzania ameniambia hivi sasa mchumba wake anajua maneno mengi tu ya kichina na hata akimpigia simu wanasalimiana kwa kichina yaani anajua kusema NI HAO salamu kubwa hapa nchini China na kusema awali walikuwa wakiambiana kwa kingereza ILOVE U ila kwa sasa anamwambia kwa kichina WO AI NI yenye maana hiyo hiyo ya Nakupenda.
Na sio yeye tu hivi sasa watu wengi wanatamani kujua hasa kuongea kichina kutokana na Taifa hili kukuwa kiuchumi na kuwekeza kila kona ya dunia hasa kwenye nchi zinazoendelea kama za barani Afrika.
Kwa kweli utakubaliana na mimi kuwa kumekuwa na ugumu wa mawasiliano baina ya wenyeji na wachina kwenye nchi mbali mbali wanazowekeza na ndio maana wengi wanatamani kuijua lugha hii.
Na ndio maana wengi waliobahatika kuijua lugha hii wanawafundisha wenzao ili nao wajue huku wakiwa na imani kuwa inaweza kuwasaidia hasa kwenye kufanya kazi na wananchi wa China wanaoenda kufanya kazi au kufanya biashara kwenye nchi hizo.
Kwa upande wake kijana Juan Leon Esono jina lake la kichina anaitwa Li song toka Guine ya Ikweta anasema yeye hivi sasa anamfudisha mchumba wake lugha hii ya kichina kwa kutumia njia ya mtandao wakati yeye yupo hapa Wuhan China na mchumba wake yupo nchini kwao.
Anasema kwa sasa mchumba wake huyo anaweza kusalimia kwa kichina na maneno mengi tu anayajua kwa sasa na ameonyesha kuipenda.
Kijana huyo anasema awali mchumba wake huyo alikuwa na imani kama waliyonayo watu wengi duniani kuwa kichina hakiwezekaniki hata kidogo kwasababu ni lugha ngumu ila hivi sasa yeye mwenyewe ameikubali na hata wakati mwingine anamsumbua kweli kweli aende kwenye mtandao ili amfundishe.
Vijana wengi wanasema kama mitandao ingekuwa bora kwenye nchi zao hasa zile za barani Afrika basi kazi hii ingekuwa rahisi kwani wanaotaka kujua lugha hii ni wengi tu na hivi sasa imekuwa kivutio kwenye nchi hizo kutokana na kuwepo kwa wananchi wengi wa China kwenye nchi mbali mbali barani humo.
Kwa upande wake kijana Luka Pawa kutoka Papua new Guine anasema yeye amedhamiria kabisa kufungua darasa atakaporudi nyumbani kwao ili awafundishe jamaa na rafiki zake kichina. Luke anasema amedhamiria kufanya hivyo baada ya kuona jamaa zake wengi wanavutiwa na lugha hiyo ambao tayari ameanza kuwafundisha kwa njia ya mtandao. Kama alivyosema kijana Li song, Luka nae mtu wake wa kwanza kumfundisha lugha ya kichina ni mchumba wake ambae moja kwa moja aliipenda na hivi sasa anaelewa maneno mengi sana ya kichina hata akimpigia simu wakiwa wanaongea anaweza kuingizia maneno ya kichina ila salamu ndio imemkaa sana.
Mbali na mchumba wake Luka pia anasema anawafundisha wadogo zake wawili lugha ya kichina kwa njia ya mtandao walioko huko nchini kwako na hadi sasa nao wanajua baadhi ya maneno ya kichina kuona hivyo nao wameanza kutamani sasa kuja kusoma nchini China ili waweze kujua vizuri kuiiongea na kuandika lugha hii.
Mwisho kijana huyo anasema pamoja na yote anafikiria kuanza kuandika kitu muhimu kuhusu China na lugha yake ya kichina ambayo hivi sasa inazidi kukua kila kukicha na anaamini baada ya miaka michache lugha hii itakuwa imeenea karibu dunia nzima.
Lakini kila mtu anasema kila ndugu yake anayemfundisha lugha ya kichina anavutiwa sana na kutaka kujua kuongea kuliko kutaka kujua kuandika ambako moja kwa moja wamesema kuna ugumu tena sio kidogo.
Kitu kingine ni kwamba watu wengi hivi sasa duniani wanataka kujua kuongea lugha nyingi tu kutokana na utandawazi uliopo na kuenea kwa teknlojia na ukiwa unajua kuongea lugha nyingi unaweza kupata ajira hasa kwenye nchi zinazoendelea.
Na wanasema kujua kuongea zaidi ndio kuna faida sana kwao hasa kwa kule kuwepo wa wanchi wengi wa China waliowekeza kwenye nchi hizo na ugumu unaopatikana kwenye kufanya mawasiliano kutokana na wao kutojua lugha ya mataifa hayo wanayowekeza au lugha ya kingereza iliyoenea duniani kote, hivyo kama akitokea mtu akijua kichina japo kidogo basi anaonekena mtu wa maana sana na hata anaweza kupata ajira kirahisi hasa ya kuwa mkalimani.
Sio hao tu wanaojaribu kutoa darasa la lugha ya kichina hata mimi siku moja moja ninafanya hivyo kwa Mama Nancy na ninahakika nae siku moja anajua kuongea kichina na wewe msomaji wangu usiwe na haraka ipo siku nawe utaongea kichina tena bila wasi wasi wowote na ondoa ile imani kuwa kichina ni lugha ngumu.
Hakuna kitu kigumu hapa duniani ukipania utakijua tu hivyo sio miujiza kichina kinaongeleka tena kwa kawaida tu kama zilivyo lugha nyingine na ndio maana jamaa zetu tunaowafundisha kwa njia ya mitandao wanakipenda wanaendelea kujifunza na ninaimani watajua tu.
| © China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |