• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Siku ni ya nne kwenye mashindano ya olimpiki jijini London,Uingereza.Tutupe macho yetu viwanjani.

    (GMT+08:00) 2012-08-01 14:38:35

    Tuanze na ushindi mpya wa China kwenye mashindano hayo ambapo Ye Shiwen wa China alitia mkobani nishani yake ya pili ya dhahabu baada ya kushinda uogeleaji mita 200 medley kwa wanawake. Ye alishinda medali yake ya kwanza na kuandikisha rekodi mpya ya dunia kwenye uogeleaji mita 400 medley. Kwenye uogeleaji mita 200 medley,Alicia Coutts wa Australia alijipatia nishani ya fedha nae Caitlin Leverenz wa Marekani akaridhika na nishani ya shaba.Ye alielezea kuhusiana na ushindi huo wa pili. "sikuwa katika hali yangu nzuri leo,nilikuwa nimebakia nyuma kiasi kwenye butterfly,backstroke na breaststroke kwa hivyo nikahitajika kuogelea kutumia mtindo wa freestyle ili kuongeza kasi". Wakati huohuo maafisa wa olimpiki wanaendelea kumtetea muogeleaji huyo mwenye umri wa miaka 16 kuhusiana na tetesi za utumizi wa dawa za kumuongezea nguvu.Colin Moynihan ni mwenyekiti wa chama cha olimpiki nchini Uingereza. "Ye Shiwen,tunafahamu uwezo wa shirika la kupambana na na utumizi wa dawa(WADA) na limethibitisha kuwa yuko safi na hakuna la zaidi.Ni jambo la kusikitisha kuona kuna dhana nyingi kutoka kwa vyombo vya habari".Ye Shiwen ameinua macho ya wengi baada ya kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 400 medley na kuogelea kasi zaidi kuliko mshindi kwa upande wa wanaume kwenye kitengo hicho.Hali hiyo imepelekea mtangazaji mmoja wa kituo cha televisheni nchini Uingereza BBC na kocha wa timu ya Marekani kukisia utumizi wa dawa za kuongeza nguvu.Hata hivyo maafisa wa China wamesema kulinganisha muda wa kina dada na waume si sawa kwani mshindi kwa upande wa wanaume,muogeleaji,Ryann Lochte wa Marekani hakupata upinzani mkali.Kufikia sasa hakuna mwanamichezo yeyote wa China aliyepatikana na utumizi wa dawa za kuongeza nguvu katika michezo ya Olimpiki ya London.

    Bado tukisalia kidimbwini,muogeleaji Michael Phelps wa Marekani alishinda medali mbili kwenye uogeleaji na kuandikisha historia kama mwanaolimpiki bora zaidi. Phelps alijinyakulia nishani ya fedha kwenye uogeleaji mita 200 butterfly na kujipatia medali ya dhahabu kwenye uogeleaji freestyle mita 200 kupokezana.Ushindi huo umemfanya muogeleaji huyo kuwa na idadi ya medali 19 kwa jumla kwenye amali yake na kumshinda mwanamichezo Larisa Latymina wa Russia wa mchezo wa gymnastics ambaye ana medali 18.Medali hizo 19 za Phelps zinajumuisha rekodi ya 15 za dhahabu,8 ambazo alishinda kwenye olimpiki mjini Beijing,China miaka minne iliyopita.Aidha muogeleaji Chad le Cos ndie aliyejinyakulia nishani ya dhahabu kwenye uogeleaji mita 200 butterfly.Kwa upande wa kina dada,Allison Schmitt wa Marekani alivikwa medali ya dhahabu kwenye uogeleaji mita 200 freestyle. Camille Muffat wa Ufaransa alijipatia nishani ya fedha nae Bronte Barrett wa Australia akachukua medali ya fedha.

    Mchezo wa kupiga mbizi wa timu mita 10 kwa kina dada ulishuhudia China ikiibuka na ushindi baada ya Chen Ruolin na Wang Hao kujizolea nishani ya dhahabu.Timu ya Mexico ya Paola Espinosa na Orzoco Orza Alejandra ilijinyakulia nishani ya fedha huku Benfeito Meaghan na Filion Roseline wa Canada wakitosheka na nishani ya shaba.

    Mwanariadha bingwa wa dunia wa mbio za mita 800,David Rudisha wa Kenya amesema anaelekeza nguvu zake kuivunja rekodi ya olimpiki iliyoandikishwa na mwanariadha Vebjorn Rodal kwenye olimpiki ya Atlanta mwaka 1996.Hata hivyo Rudisha anatazamia upinzani mkali kutoka kwa wanariadha raia wenza,Timothy Kitum na Anthony Chemut, wanariadha Mohammed Aman wa Ethiopia na Nijel Amos wa Botswana.Ratiba ya riadha inatazamiwa kuanza Agosti 3.

    Urska Zolnir wa Slovenia alimshinda Xu Lili wa China na kujinyakulia nishani ya dhahabu kwenye mchezo wa judo kilo 63 kwa kina dada.Xu alijipatia nishani ya fedha huku Yoshie Ueno wa Japan na Gevrise Emane wa Ufaransa wakijishindia medali za shaba kila mmoja.kwa upande wa wanaume kitengo cha kilo 81, Kim Jae-Bum wa Korea Kusini alituzwa nishani ya dhahabu, Bischof Ole wa Ujerumani akavishwa medali ya fedha nae Nifontov Ivan wa Russia akaridhika na nishani ya shaba.

    China iliendelea kuonyesha umahiri wake kwenye michezo hiyo ya olimpiki baada ya Lei Sheng kujinyakulia nishani ya dhahabu kwenye mchezo wa kushindana kwa vitara yaani fencing baada ya kumshinda Alaadldin Abouelkassem wa Misri kwa seti 15-13.Aidha ni wazi China itajinyakulia nishani ya dhahabu kwenye mchezo wa tenisi ya mezani kwa kina dada kwani washiriki wake wawili, Ding Ning na Li Xiaoxia watachuana kwenye fainali.

    Kwenye mchezo wa ustadi wa kupanda farasi kwa timu,Ujerumani ilijinyakulia nishani ya dhahabu,Uingereza ikajipatia medali ya fedha nayo New Zealand ikaridhika na nishani ya shaba.kwenye mchezo huo lakini wa mtu mmoja,Jung Michael wa Ujerumani alijipatia nishani ya dhahabu,Algotsson Ostholt Sara wa Sweden akajizolea nishani ya fedha nae Auffarth Sandra wa Ujerumani akaongeza medali ya shaba.

    Mnyanyuaji vyuma wa Kazakhstan,Maneza Maiya alijinyakulia nishani ya dhahabu kwenye unnyanyuaji vyuma kilo 63 kwa kina dada. Tsarukaeva Svetlana wa Russia akajipatia medali ya fedha nae Girard Christine wa Canada akajizolea nishani ya shaba.

    Timu ya Marekani ya mchezo wa Gymnastics kwa kina dada ilijipindapinda na kufanikiwa kutuzwa nishani ya dhahabu.Aidha nishani hiyo ilikuwa ya kwanza tokea mwaka 1996.Timu ya Russia ilijipatia nishani ya fedha nayo ile ya Romania ikatosheka na nishani ya shaba.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako