• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kampuni moja kubwa ya huduma za simu ya Kenya yatangaza zawadi za pesa kwa washiriki wa olimpiki ya walemavu

    (GMT+08:00) 2012-08-02 10:08:45

    Kampuni moja kubwa ya huduma za simu ya Kenya imetangaza zawadi za pesa kwa washiriki wa olimpiki ya walemavu wanaotarajiwa kuondoka nchini humo baadae mwezi huu.Kampuni hiyo imesema itapeana dola 12000 kwa washindi wa medali ya dhahabu,dola 7150 kwa washindi wa Fedha na dola 5715 kwa washindi wa nishani ya shaba.Akiongea wakati wa hafla ya kuwaaga wanamichezo hao jijini Nairobi,Makamu wa rais wa Kenya,Kalonzo Musyoka amezitaka kampuni nyingine na wahisani wanaofadhili michezo kutoa ushauri kwa wanamichezo kuhusu njia bora za kuwekeza fedha zao.

    Wachezaji nane wa mchezo wa mpira wa vinyoya wamepigwa marufuku na bodi ya mchezo huo.Hii ni baada ya kujaribu kwa kusudi kupata sare.Wachezaji hao,Wang Xiaoli na Yu Yang kutoka China,Meiliana Jauhari na Greysia Polii wa Indonesia,Jung Kyun Eun,Kim Ha Na,Ha Jung Eun na Kim Min Jung wa Korea Kusini wameshtumiwa na shirikisho la mpira wa vinyoya duniani(BWF) kwa kutojituma kikamilifu kushinda mechi na kwa kuenda kinyume na kanuni za mchezo huo.Korea Kusini na Indonesia zimekata rufaa kuhusu uamuzi huo lakini BWF ikakataa ombi la Korea Kusini huku ikitupilia mbali la Indonesia.Wang na Yu pamoja na wapinzani wao,Jung na Kim kutoka Korea Kusini walizomewa na mashabiki na kurushiwa maneno ya matusi walipokuwa wakifanya kusudi kupiga mipira hiyo kwenye neti.Kocha wa timu ya China ya mchezo huo,Li Yongbo ameomba radhi kutokana na kashfa hiyo.

    Mchezo wa tenisi ya mezani kwa kina dada wa mtu mmoja ulishuhudia Li Xiaoxia wa China akivalishwa medali ya dhahabu huku raia mwenza, Ding Ning akijiliwaza na nishani ya fedha. Aidha Feng Tianwei wa Singapore na Ishikawa Kasumi wa Japan wakajipatia nishani ya shaba kila mmoja.China imekuwa ikishinda mchezo huo kwa kina dada tangu mchezo huo ulipoanzishwa mwaka 1988.

    Nchi mwenyeji imepata medali ya kwanza ya dhahabu katika siku ya tano tangu michuano mbalimbali ya Olimpiki ianze. Timu ya watu wawili ya kina dada ya Uingereza ya Glover Helen na Stanning Heather imejinyakulia nishani ya dhahabu kwenye mchezo wa kupiga makasi.Hornsey Kate na Tait Sarah wa Australia wakavikwa medali ya fedha nao Haigh Juliette na Scown Rebecca wa New Zealand wakaridhika na nishani ya shaba.kwenye mchezo huo kwa timu ya watu wanne kwa kina dada,timu ya Ukraine ilijipatia medali ya dhahabu,timu ya Ujerumani ikapata nishani ya fedha nayo ile ya Marekani ikajizolea nishani ya shaba.Bado kwenye mchezo huo kwa timu ya watu wanane kwa wanaume,Ujerumani ilivikwa nishani ya dhahabu,Canada ikajipatia nishani ya fedha nayo Uingereza ikaridhika na medali ya shaba.

    Mwanamichezo Kristin Armstrong wa Marekani alituzwa medali ya dhahabu kwenye mchezo wa uendeshaji baiskeli kwa muda wa kibinafsi upande wa kina dada. Arndt Judith wa Ujerumani alitosheka na nishani ya fedha huku Zabelinskaya Olga wa Russia akijiliwaza kwa medali ya shaba.kwa upande wa wanaume, Bradley Wiggins wa Uingereza alijipatia medali ya dhahabu, Tony Martin wa Ujerumani ya fedha nae Froome Christopher akajaza kikapu cha Uingereza kwa nishani ya shaba.

    Mwanadada Kim Jangmi wa Korea Kusini alijizolea medali ya dhahabu kwenye mchezo wa kulenga shabaha kwa bastola mita 25 kwa kina dada. Chen Ying wa China akajibandika nishani ya fedha huku Kostevych Olena wa Ukraine akiondoka na medali ya shaba.

    Mwanadada Jiao Liuyang wa China alijitweka medali ya dhahabu kwenye uogeleaji mita 200 butterfly kwa kina dada.Mireia Belmonte Garcia wa Hispani akajipatia nishani ya fedha nae Natsumi Hoshi akajiongoa na medali ya shaba.Kwa upande wa wanaume uogeleaji mita 200 Breaststroke,Daniel Gyurta wa Hungary aliibuka na medali ya dhahabu na kuandikisha rekodi mpya ya dunia.

    Kwenye mchezo wa kupiga mbizi kwa kuruka kutoka mabao yaliyooanishwa mita tatu kwa wanaume, Luo Yutong na Qin Kai wa China walijizolea nishani ya dhahabu, Zakharov Ilya na Kuznetsov Evgeny wa Russia wakajitwalia medali ya fedha nao Troy Dumais na Kristian Ipsen wa Marekani wakatosheka na nishani ya shaba.

    Molmenti Daniele wa Italia alishinda medali ya dhahabu kwenye mchezo wa kayaki kwa wanaume. Hradilek Vavrinec wa Jamuhuri ya Czech alijizolea medali ya fedha nae Aigner Hannes wa Ujerumani akaridhika na medali ya shaba.

    Kwenye unyanyuaji vyuma,China ilijizolea nishani yake ya nne ya dhahabu ya mchezo huo baada ya Lu Xiaojun kuvunja rekodi yake mwenyewe na kushinda kwenye kitengo cha kilo 77 kwa wanaume. Kwa upande wa kina dada kilo 69, Rim Jong Sim wa Korea Kaskazini alinyanyua nishani ya dhahabu, Cocos Roxana Daniela wa Romania akajitweka nishani ya fedha nae Shkermankova Maryna wa Belarus akavishwa medali ya shaba.

    Mchezo wa Judo kwa kina dada kitengo cha kilo 70, ulishuhudia Lucie Décosse wa Ufaransa akivikwa medali ya dhahabu,Thiele Kerstin wa Ujerumani akajipatia nishani ya fedha nae Alvear Yuri wa Colombia akaondoka na medali ya shaba.Tusalie kwenye mchezo huo upande wa wanaume kitengo cha kilo 90, Song Dae-Nam wa Korea Kusini alinyanyua nishani ya dhahabu, Gonzalez Asley wa Cuba akabeba medali ya Fedha nae Ilias Iliadis wa Ugiriki akajiliwaza na nishani ya shaba.

    Kohei Uchimura wa Japan aliweza kujipindapinda na kuibuka na nishani ya dhahabu kwenye mchezo wa Gymnastics kwa mtu mmoja kwa wanaume. Nguyen Marcel wa Ujerumani alijipatia nishani ya fedha huku Danell Leyva wa Marekani akijiliwaza na medali ya shaba.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako