• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Siku ya saba kwenye mashindano ya olimpiki jijini London Uingereza

    (GMT+08:00) 2012-08-05 19:24:33

    Tuanze na riadha ambapo mwanariadha Tirunesh Dibaba wa Ethiopia alijishindia nishani ya dhahabu kwenye mbio za mita 10000 kwa kina dada.Aidha wanariadha Sally Jepkosgei Kipyego na Vivian Jepkemoi Cheruiyot wa Kenya wakalazimishwa kuchukua medali za fedha na shaba mtawalia.

    Wojdan Shahrkhani wa Saudi Arabia ameandikisha historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kutoka nchini humo kushiriki mashindano ya olimpiki. Shahrkhani mwenye umri wa miaka 16 alishiriki mchezo wa judo kitengo cha uzani wa kilo 78 kwa kina dada.Kwenye mchezo huo, Idalys Ortiz wa Cuba alishinda nishani ya dhahabu. Shahrkhani amekuwa akiangaziwa sana baada ya maafisa wa mchezo huo kudai kuwa hawezi kushiriki akiwa amevalia hijab kwasababu za kiusalama.Aidha Shahrkhani aliyekuwa amevalia kofia ya kubana nyeusi alishindwa kwa haraka na mpinzani wake MelissaMojica wa Puerto Rico.Mwanamichezo huyo ni mmoja wa wanawake wawili wa Saudi Arabia ambao wanashiriki olimpiki.Mwanamichezo mwingine wa nchi hiyo ni mzaliwa wa Marekani,Sarah Attar ambae atashiriki mbio za mita 800.

    Kwenye mchezo wa kupiga makasi kwa mtu mmoja kwa wanaume, Drysdale Mahe wa New Zealand alijizolea nishani ya dhahabu, Synek Ondrej wa Jamuhuri ya Czech akajipatia medali ya fedha nae Campbell Alan wa Uingereza akatosheka na nishani ya shaba.bado kwenye mchezo huo wa watu wawili kwa wanaume,timu ya Eric Murray na Hamish Bond wa New Zealand ilijizolea nishani ya dhahabu,Chardin Germain na Mortelette Dorian wa Ufaransa wakavikwa medali ya fedha nao Nash George na Satch William wa Uingereza wakatosheka na nishani ya shaba.Kwa upande wa kina dada wa makasia mawili ya timu ya watu wawili, Anna Watkins na Katherine Grainger wa Uingereza walijipatia nishani ya dhahabu, Crow Kim na Pratley Brooke wa Australia wakavikwa medali ya fedha nao Fularczyk Magdalena na Michalska Julia wa Poland wakaridhika na nishani ya shaba.

    Tujitose kidimbwini ambapo Muogeleaji Franklin Missy wa Marekani aliibuka na medali ya dhahabu kwenye uogeleaji mita 200 Backstroke kwa kina dada na kuandikisha muda mpya. Zueva Anastasia wa Russia akajitwika nishani ya fedha nae Beisel Elizabeth wa Uingereza akavikwa medali ya shaba.Kwenye uogeleaji kwa upande wa wanaume mita 100 Butterfly,Michael Phelps wa Marekani alidhihirisha ubabe wake kidimbwini kwa kuibuka na medali ya dhahabu, Chad Le Clos wa Afrika Kusini akajipatia medali ya fedha nae Evgeny Korotyshkin wa Russia akajivunia medali ya shaba.Kitengo cha mita 800 Freestyle kwa kina dada kilishuhudia muogeleaji mwenye umri wa miaka 15, Katie Ledecky wa Marekani akivikwa medali ya dhahabu, Mireia Belmonte Garcia wa Hispania akajipatia medali ya fedha nae Rebecca Adlington wa Uingereza akajizolea nishani ya shaba.Muogeleaji Florent Manaudou wa Ufaransa alijipatia nishani ya dhahabu kwenye uogeleaji kitengo cha mita 50 Freestyle kwa wanaume. Cullen Jones wa Marekani akajishindia medali ya fedha nae Cesar Cielo Filho wa Brazil akavikwa nishani ya fedha.

    Mchezo wa kurusha chuma yaani Shot Put kwa wanaume ulishuhudia Majewski Tomasz wa Poland akijishindia nishani ya dhahabu, Storl David wa Ujerumani akajipatia medali ya fedha nae Reese Hoffa wa Marekani akatosheka na nishani ya shaba.

    Wanamichezo wa China walitawala mchezo wa turubali yaani Trampoline kwa wanaume ambapo Dong Dong na Lu Chunlong walijizolea nishani za dhahabu na shaba mtawalia na kumlazimisha Ushakov Dmitry wa Russia kuchukua medali ya fedha.

    Timu ya Korea Kusini ya watu wawili ya wanaume ya mchezo wa kitara ilijinyakulia nishani ya dhahabu na kuilazimisha ile ya Poland kuchukua medali ya fedha.Timu ya Italia ilijiliwaza na nishani ya shaba.

    Mchezo wa kutembea kwa kasi ulishuhudia Cano Juan Manuel wa Cuba akijishindia nishani ya dhahabu, Erickson Chris na Rutter Adam wa Australia wakajivunia medali za fedha na shaba mtawalia.

    Wanamichezo Zhang Nan na Zhao Yunlei wa China walijizolea nishani ya dhahabu kwenye mchezo wa mpira wa vinyoya wa timu ya watu wawili kwa upande wa wanaume nae Guo Shuang akaipatia China medali ya fedha kwenye mchezo wa uendeshaji baiskeli wa mtu mmoja kwa upande wa kina dada.Victoria Pendleton wa Uingereza alijinyakulia nishani ya dhahabu kwenye mchezo huo.

    Adrian Zielinski wa Poland alijinyanyulia nishani ya dhahabu kwenye mchezo wa unyanyuaji vyuma kilo 85.Hii imekuwa nishani ya dhahabu ya kwanza kwa Poland kushinda kwenye mchezo huo tangu olimpiki ya mwaka 1972 mjini Munich, Ujerumani. Apti Aukhadov wa Russia alijipatia nishani ya fedha nae Kianoush Rostami wa Iran akatosheka na nishani ya shaba.kwa upande wa kina dada, Svetlana Podobedova wa Kazakhstan alijishindia nishani ya dhahabu kwenye kitengo cha kilo 75. Natalya Zabolotnaya wa Russia alijipatia nishani ya fedha nae Iryna Kulesha wa Belarus akatosheka na nishani ya fedha.

    Tuangalie meza ya medali kufikia sasa…..

    JUMLA Dhahabu Fedha Shaba

    1. Marekani 43 21 10 12

    2. China 42 20 13 9

    3. Korea Kusini 16 8 6 8

    4. Uingereza 22 6 4 6

    5. Ufaransa 18 8 5 6

    11. Afrika Kusini 4 3 1 0

    24. Ethiopia 1 1 0 0

    35. Kenya 2 0 1 1

    41. Misri 1 0 1 0

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako