• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Siku ni ya 12 ya mashindano ya olimpiki jijini London,Uingereza.Tutupe macho yetu viwanjani.

    (GMT+08:00) 2012-08-08 10:24:00

    Tuanze na riadha ambapo,Matumaini ya Kenya kujitilia medali mkobani yalififia zaidi jana baada ya wanariadha wake kushindwa kutamba kwenye mbio za mita 1500 kwa wanaume.Mwanariadha Kiplagat Silas alikuwa wa saba,Chepseba Nixon Kiplimo akachukua nafasi ya 11 nae bingwa mtetezi,Asbel Kiprop akimaliza wa mwisho baada ya kusumbuliwa na jeraha.Aidha mwanariadha Taoufik Makhloufi wa Algeria aliibuka na nishani ya dhahabu kwenye mbio hizo, Leonel Manzano akachukua medali ya fedha nae Abdalaati Iguider wa Morocco akavikwa medali ya shaba.Wakenya watapiga dua leo kwenye mbio za mita 800 za raundi ya kwanza kwa kina dada ambapo mwanariadha Pamela Jelimo anatarajiwa kushiriki.Kwenye mbio za mita 100 kuruka viunzi kwa kina dada, Sally Pearson wa Australia alijitwika nishani ya dhahabu, Dawn Harper na Kellie Wells wa Marekani wakabidi kuchukua medali za fedha na shaba mtawalia.Wakati huohuo mwanariadha Liu Xiang wa China anaueshiriki mbio za mita 110 kuruka viunzi kwa wanaume alishindwa kufuzu baada ya kugonga viunzi na kuanguka.

    Ilikuwa fahari kwa nchi ya Iran kwenye mchezo wa unyanyuaji vyuma kilo 105 kwa wanaume pale Behdad Salimikordasiabi aliponyanyua medali ya dhahabu huku raia mwenza Sajjad Anoushiravani akichukua medali ya fedha. Ruslan Albegov wa Russia akalazimishwa kuchukua nishani ya shaba.

    Wanamichezo Alistair Brownlee na kakake Jonathan Brownlee wa Uingereza walijinyakulia nishani za dhahabu na shaba mtawalia kwenye mchezo wa kuogelea,kukimbia na kuendesha baiskeli(Triathlon) kwa wanaume.Aidha Javier Gomez wa Hispania alifanikiwa kujipatia medali ya fedha.

    Mchezo wa uendeshaji mashua kitengo cha RS-X kwa wanaume kilishuhudia Dorian van Rijsselberghe wa Uholanzi akipeperusha nishani ya dhahabu, Nick Dempsey wa Uingereza akavikwa medali ya fedha nae Przemek Miarczynski wa Poland akatosheka na nishani ya shaba.kwa upande wa kina dada, Marina Alabau Neira wa Hispania alijitilia mkobani medali ya dhahabu, Tuuli Petaja wa Finland akainua nishani ya fedha nae Zofia Noceti-Klepacka wa Poland akabeba nishani ya shaba.Bado kwenye mchezo huo kwa kuendesha kwa kasi baiskeli kwa kina dada, Meares Anna wa Australia alibeba medali ya dhahabu, Victoria Pendleton wa Uingereza akavikwa nishani ya fedha nae Guo Shuang wa China akajivunia medali ya shaba.

    Tuangazie mchezo wa Gymnastics wa nguzo sambamba kwa wanaume, Feng Zhe wa China alijishindia medali ya dhahabu, Nguyen Marcel wa Ujerumani akatwaa medali ya fedha nae Sabot Hamilton wa Ufaransa akainua medali ya shaba.Bado kwenye mchezo huo kwa kina dada kujipima kwenye mhimili, Deng Linlin na Sui Lu wa China walijinyakulia nishani za dhahabu na fedha mtawalia na kumlazimisha Aly Raisman wa Marekani kujiliwaza na medali ya shaba.Tusalie kwenye mchezo wa gymnastics wa mtaimbo wa mlalo kwa wanaume, Epke Zonderland wa Uholanzi alijishindia medali ya dhahabu, Fabian Hambuechen wa Ujerumani akajizolea nishani ya fedha nae Zou Kai wa China akakumbatia nishani ya shaba.Aidha Aly Raisman wa Marekani alijizolea medali ya dhahabu kwenye mchezo wa Gymnastics wa sakafuni kwa kina dada, Catalina Ponor wa Romani akapokea medali ya fedha nae Aliya Mustafina wa Russia akajivunia medali ya shaba.

    Tujitose kidimbwini ambapo kwenye uogeleaji wa watu wawili kupokezana kwa kina dada ulishuhudia Natalia Ishchenko na Svetlana Romashina wa Russia wakiibuka na medali ya dhahabu, Ona Carbonell na Andrea Fuentes wa Hispania wakabeba nishani ya fedha nao Huang Xuechen na Liu Ou wa China wakatosheka na nishani ya shaba.wakati huohuo, Lengo la wanamichezo wa China kushinda medali zote nane za mchezo wa kupiga mbizi zilisambaratishwa baada ya Ilya Zakharov wa Russia kuwashinda He Chong na Qin Kai na kuibuka na medali ya dhahabu kwenye upigaji mbizi wa mita tatu kwa wanaume.

    Mwanadada Trott Laura wa Uingereza alijitwalia nishani ya dhahabu kwenye mchezo wa kuendesha baiskeli omnium kwa kina dada, Sarah Hammer wa Marekani akakumbatia medali ya fedha nae Edmondson Annette wa Australia akajitweka nishani ya shaba.

    China ilidhihirisha ubabe wake kwenye tenisi ya mezani ya watu watatu kwa kina dada baada ya Ding Ning,Li Xiaoxia na Guo Yue kuwazidi maarifa kina dada wa Japan na kujinyakulia nishani ya dhahabu.

    Kwenye mchezo wa mieleka wa kigiriki na kirumi(Greco-Roman) wa kilo 66 kwa wanaume, Kim Hyeon-woo wa Korea Kusini alijitilia kikapuni medali ya dhahabu, Tamas Lorincz wa Hungari akaridhika na medali ya fedha nao Manuchar Tskhadaia wa Georgia na Steeve Guenot wa Ufaransa wakangangania medali ya shaba.

    Mwanamichezo Robert Harting wa Ujerumani alijinyakulia medali ya dhahabu kwenye mchezo wa kurusha kisahani kwa wanaume, Ehsan Hadadi wa Iran akachukua medali ya fedha nae Gerd Kanter wa Estonia akakumbatia nishani ya shaba.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako