Straika wa Yanga ya Tanzania, Didier Kavumbagu ameupa uongozi wa timu yake siku tatu sawa na saa 72 kuanzia juzi Jumanne kumueleza hatma ya mkataba wake mpya, vinginevyo atajiunga na timu mojawapo kubwa nchini humo. Kavumbagu aliyeifungia Yanga mabao 12 kati ya 61 iliyofunga msimu uliopita huku akitoa pasi nyingi za mabao, mkataba wake umemalizika muda mfupi tu baada ya msimu wa ligi wa 2013/14 kumalizika Jumamosi iliyopita, lakini mshambuliaji huyo raia wa Burundi hakuwa ameambiwa jambo lolote na uongozi. Japokuwa Kavumbagu hajaweka wazi yuko kwenye mazungumzo na timu gani, lakini Azam FC wanafanya naye mazungumzo ili kuimarisha kikosi chao kitakachoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kitishe zaidi. Muda mfupi tu baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani, kocha wa Azam, Joseph Omog amesema anataka kufanya usajili wa kisasa ndani na nje ya nchi ili aweze kuwa na kikosi cha wachezaji wazoefu watakaoiwezesha timu yake kufanya vizuri.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |