• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • uchambuzi wa timu nyingine mbalimbali za Afrika zilizocheza wiki nzima

    (GMT+08:00) 2014-06-26 16:16:20

    Wiki iliyopita katika kipindi hiki cha Jamvi uchambuzi wa timu za Afrika zinazocheza kombe la dunia nchini Brazil, tuliizungumzia timu ya taifa ya Brazil na Croatia ambazo zilicheza Alkhamis iliyopita siku ya ufunguzi wa kombe hili ambapo Brazil iliifunga Croatia kwa mabao 3-1. na leo hii tunaendelea na uchambuzi wa timu nyingine mbalimbali za Afrika zilizocheza wiki nzima.

    Wiki hii tumeshuhudia timu zote tano za Afrika zikiwemo, Ghana, Cameroon, Cote d'livoire Algeria na Nigeria zikipambana katika viwanja mbalimbali nchini Brazil. Lakini katika mechi hizo nyingi zilikuwa ni za kukatisha matumaini ya Afrika kufika angalau kwenye raundi ya timu 16. tukianza na Cameroon ambayo hivi sasa imeshacheza mechi mbili katika kundi A ya kwanza ilikuwa dhidi ya Mexico ambayo ilifungwa kwa mabao 1-0 na ya pili ni ile iliyocheza juzi na Croatia ambayo waligaragazwa kwa magoli 4-0. Katika mechi hizo mbili Cameroon haikuonesha mchezo mzuri sana hususana ukizingatia kwamba katika mechi yake dhdi ya Mexico walikabiliana na mlinda mlango makini sana kwani ilikuwa bado kidogo tu wajipatie ushindi ila mpira uliokolewa na mlinda mlango huyo machachari wa Mexico. Na ile ya juzi dhidi ya Croatia ndio ikaihakikishia nchi hiyo kufungasha virago kabisa kwenye michuano hiyo. Mechi yake ya mwisho itakuwa tarehe 23 watakapovaana na wenyeji Brazil.

    Baada ya kusikia mawili matatu kuhusu Cameroon, sasa tuitizame Nigeria ambayo yenyewe imecheza mechi moja tu dhidi ya Iran. katika mchezo huo timu zote mbili zilitoka sare ya tasa kwenye kundi lao F . Kwa mujibu wa wachambuzi wa mchezo wanasema mechi hiyo ilikuwa chapwa kati ya mechi zote zilizochezwa hadi sasa. Ingawa Nigeria walimiliki mchezo lakini walipata nafasi chache dhidi ya Iran wanaoongozwa na kocha wa zamani wa Manchester United Carlos Queiroz. Watu wengi walikuwa wanaamini kuwa mabingwa hao wa Afrika watafuzu katika hatua ya timu 16 pamoja na miamba ya Amerika Kusini Argentina, lakini kwa sasa Nigeria ina kibarua kikubwa kwani inalazimka kuishinda Bosnia, ambayo ilionesha mchezo safi kabisa siku ya Jumapili.

    Timu ya Algeria ipo kundi H na juzi tarehe 17 ilichuana na Ubelgiji na kulazwa kwa mabao 2-1. Hiyo ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa Algeria ambayo ilitangulia kuona lango la Ubelgiji baada ya Sofiane Feghouli kufanyiwa madhambi na mlinzi wa Tottenham Jan Vertonghen katika kipindi cha kwanza na kupata bao la mapema la penalty. Hata hivyo Algeria walishindwa kutamba katika kipindi cha pili baada ya dakika ya 70 Ubelgiji kusawazisha goli hilo la Mbweha wa Jangwani huku Martens akipata goli la pili katika dakika ya 80 na kuifanya Ubelgiji iibuke washindi hadi mpira unamalizika. Kwa hiyo ingawa Algeria walijitahidi lakini miamba ya Ubelgiji iliwatoa jasho.

    Ghana nayo ilizidisha machungu ya waafrika walipocheza na Marekani kwenye mchezo wa kundi G. Katika mechi hiyo Ghana ilicharazwa magoli 2-1. ushindi huo wa Marekani umeiwezesha kulipiza kisasi cha kufungwa na Ghana katika makombe mawili ya dunia. Ghana ilitolewa katika kombe la dunia miaka minne iliyopita huku ikilia, wakati Asamoah alipokosa penalty katika dakika za mwisho za muda wa nyongeza dhidi ya Uruguay na kukoa nafasi ya kuwa nchi ya kwanza ya Afrika kufikia nusu fainali. Hata hivyo katika mchezo huu wa tarehe 16 Ghana ilitaabika sana kujibu goli lililofungwa mapema na Clint Dempsey katika sekunde ya 29 baada ya kipenga cha kuashiria mpira kuanza kupulizwa. Nafasi nyingi ziliangukia kwa Asamoah lakini alishindwa kumalizia, na ingawa hakupata lakini lakini amesaidia timu yake iweze kuingiza goli la kusawazisha baada ya Ayew kupiga mpira wa kisigino na kufanikiwa kuliona lango la Marekani. Hata hivyo ingawa Ghana ilionekana kuwa na muda wa kuweza kupata goli la pili lakini matumaini yalizimwa baada ya Marekani kuingiza la pili kupitia kona iliyopigwa na mchezaji wake Graham Zusi.

    Hebu tumalizie kwa kuingalia timu ya Ivory Coast ambayo ipo kwenye kundi C. jumapili iliyopita ilikuwa ni siku ya faraja kwa Waivory Coast na waafrika kwa ujumla baada ya Miamba hiyo ya soka barani Afrika kutoka nyuma na kuibamiza bila huruma Japani kwa mabao 2-1. katika mchezo huo uliosakatwa tarehe 15 Ivory Coast ilijipatia mabao yake kupitia wachezaji Wilfried Bony na aliyekuwa mchezaji wa Arsenal Gervinho huku Japan ikifunga kupitia mshambuliaji wake keisuke Honda. Ushindi huo wa Ivory Coast ni wa kwanza miongoni mwa timu za bara la Afrika.

    Mbali na mchezo huo wa tarehe 15, jana pia ilikuwa na mechi yake ya pili dhidi ya Colombia, mechi hiyo ilikuwa kali katika kundi lake C. hata hivyo Ivory Coast haikuonesha makeke yake kwani ilisalimu amri kwa kupachikwa mabao 2-1 na Colombia. Goli moja la Ivory Coast lilifungwa na Gervinho. Ingawa waivory coast walijitahidi kuwapa kibarua kigumu wacolombia lakini wapinzani wao hao walifanikiwa kulinda ushindi wao. Ivory Coast bado wana nafasi nzuri ya kufikia hatua ya mtoano kwa vile walishinda mechi yao ya ufunguzi, na baadaye watakabiliana na Ugiriki.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako