• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Nchi zenye nafasi ya kuendelea mbele kwenye hatua ya mtoano

    (GMT+08:00) 2014-06-27 16:51:03

    Wiki iliyopita katika kipindi hiki cha Jamvi uchambuzi wa timu za Afrika zinazocheza kombe la dunia nchini Brazil, tulizizungumzia timu za taifa za nchi zote tano zinazoshiriki michuano hiyo. Na vile vile tukaona nchi gani iliyofanya vizuri au kujitahidi lakini pia tulizungumzia nchi zile zilizofanya vibaya na ambazo zilikuwa hatarini kufungashwa virago kwenye michuano hii. Na leo hii pia tutaendelea kuzijadili nchi hizo na kujua zipi zenye nafasi ya kuendelea mbele kwenye hatua ya mtoano na zipi zilizofurushwa kwenye michuano hiyo.

    Tuanze na kipindi kwa kuiangalia timu ya Cameroon ambayo imeshacheza mechi zote tatu katika kundi lake A na bahati mbaya imeshaaga michuano hiyo kwani imetoka ikiwa mkiani tena haikupata pointi hata moja, hii inamaanisha kuwa haikutoka sare wala kushinda kwenye michuano. Mechi yake ya mwisho ilikuwa ni ile ya tarehe 23 dhidi ya Brazil ambayo angalau wameambulia goli moja, la kufutia machozi. Lakini mechi kati yake na Mexico waliambulia patupu kwa kufungwa 1-0 na ile waliyocheza na Croatia walifungwa bila huruma magoli 4-0. Cameroon imemaliza mechi zake zote tatu ikiwa mkiani kabisa yaani nafasi ya 4, huku ikifungwa jumla ya mabao 9 kwa jumla na kuondoka na zawadi ya bao 1 tu iliyolipata ilipocheza na Brazil.

    Kutokana na kufanya vibaya kwenye michuano ya kombe la dunia rais wa Cameroon Paul Biya ametaka ufanyike uchunguzi wa kina. Kwani The Indomitable Lions walifanya majanga makubwa mbali na lile la kushindwa mechi zote tatu za makundi, pia wachezaji walitolewa na wengine kugombana kiwanjani wakati wa mechi inaendelea. Waziri mkuu Philemon Yang naye ameamuru ufanywe uchunguzi ili kujua sababu ya yote hayo. Juu ya yote hayo Alex Song alioneshwa kadi nyekundu kwa kumpiga kiwiko cha nguvu mshambuliaji wa Croatia Mario Mandzukic kosa ambalo limepelekea kufungiwa mechi tatu na Fifa. Kwa mujibu wa taarifa waziri mkuu atatoa matokeo ya uchunguzi ndani ya mwezi mmoja na kutoa mapendekezo ya kuijenga tena timuya taifa ya nchi hiyo.

    Timu nyingine ya Afrika ambayo imeyaaga mashindano hayo ni Ivory Coast. Timu hiyo imeondoa kabisa matumaini ya bara la Afrika kuwakilishwa katika raundi ya pili kwenye kombe la dunia huko Brazil kwani ilikuwa inahitaji sare tu ili kufuzu raundi hiyo na badala yake iliambulia kichapo cha 2-1 kutoka Ugiriki. Hata hivyo Ivory Coast itajilaumu kwa kushindwa kusonga mbele kwenye mechi hiyo kwani walipata nafasi nzuri ya kufanya mashambulizi lakini iliboronga . Ivory Coast tayari imeshacheza mechi zake zote tatu za kundi C na imemaliza ikiwa nafasi ya tatu kwenye kundi lake huku wapinzani wao Ugiriki wakiwa nafasi ya pili. Hadi inamaliza mechi kwenye kundi lake imefungwa jumla ya mabao 5 na kufunga 4 na haikupata pointi hata 1. Mara tu baada ya kutolewa kwenye michuano hiyo kocha wa Ivory Coast Sabri Lamouchi alijiuzulu ukocha wa kikosi hicho baada ya Ivory Coast kufanya vibaya na kushindwa kufikia hatua ya mtoano kwenye kombe la dunia.

    Baada ya kupata habari mbaya na za kusikitisha kuhusu timu za Afrika zilizoondolewa kwenye michuano hii, sasa tupate furaja kidogo kwa kukiangalia kikosi cha Nigeria. The Elephant wameingia katika raundi ya timu 16 bora, ingawa kwa taabu, kwani mechi ya mwanzo ya makundi waliyocheza dhidi ya Iran haikuwafurahisha waafrika hata kidogo, na kukatisha tamaa mashabiki hadi kuanza kuhoji kama Nigeria itafika popote, hata hivyo wahenga wanasema Mungu si mzee mkumba kwani mechi ya pili waliyocheza na Bosnia katika kundi lake F, ilijitahidi angalau ikapata ushindi wa goli moja. Hata hivyo bado ilikuwa imekalia kuti kavu kwani mechi yake dhidi ya Argentina alilazimika kushinda au Bosnia Kuifunga Iran ndio iweze kufuzu raundi pili. Hata hivyo ingawa ilishindwa na Argentina, Iran iliipa nafasi Nigeria ya kusonga mbele baada ya kucharazwa magoli 3-1 na Bosnia. Hadi mechi zote tatu zinakamilika Nigeria imemaliza ikiwa nafasi ya pili na kuwa na magoli 3 na zawadi ya pointi 4. sasa tusubiri Jumatatu watakapovaana na Ufaransa katika raundi ya timu 16, hapo tutajua kama wanatosha mboga au la.

    Kwa upande wa timu ya Ghana nayo haikufanya vizuri ingawa ilikuwa na nafasi nzuri. Katika mechi yake ya mwisho ya makundi iliyocheza jana, Ghana ilifungwa kwa mabao 2-1 na Urusi. Ghana itajilaumu kwa kushindwa kupata ushindi uliohitajika kuihakikishia nafasi katika 16 bora baada ya John Boye alipojifunga mwenyewe. Asamoah Gyan alifunga bao la kuisawazishia Black stars lakini haikutosha kuifufua kampeni yao kwani walihitaji ushindi wa aina yeyote huku wakiomba Ujerumani iishinde Marekani ili waweze kufuzu kama washindi wa pili katika kundi G. Mbali na hayo saa kadhaa kabla Ghana haijatolewa kwenye mashindano ya kombe la dunia, nchi hiyo iliamua kuwafurusha Sulley Muntari na Kevin-Prince Boateng kwenye kikosi hicho kwa madai ya kutokuwa na nidhamu. Boateng alitoa matamshi machafu yaliyomlenga kocha Kwesi Appiah na Muntari ametimuliwa kwa kumshambulia mjumbe wa kamati kuu ya timu hiyo Moses Armah. Hayo yote yanajiri siku moja tu baada ya serikali ya Ghana kutuma dola milioni 3 nchini Brazil ili kuwalipa wachezaji wa timu hiyo fedha zao za kushiriki katika michuano ya kombe la dunia. Awali wachezaji wa Black Stars walisusa kucheza mechi kati yake na Ureno kama hawakupewa fedha hizo swala lililoilazimu serikali kuingilia kati. Ghana imemaliza ikiwa na pointi 1 na kufungwa magoli 6 pia imeondoka ikwa na zawadi ya magoli manne mkononi.

    Tumalizie uchambuzi kwa kuiangalia timu ya Algeria. Kwa mara ya kwanza katika historia timu ya taifa ya Algeria imefuzu kucheza raundi ya pili katika kombe la dunia. Mbweha wa Jangwani waliokuwa nyuma kwa bao moja kwa nunge dhidi ya Urusi katika kipindi cha kwanza walifanikiwa kusawazisha na hivyo kufuzu kama mshindi wa pili katika kundi H nyuma ya Ubeljiji. Hii ni mara yao ya kwanza kuvuka raundi ya kwanza. Algeria itaingia katika kumbukumbu za historia ya Soka Afrika kuwa mwakilishi wa 6 kuwahi kufuzu kwa raundi hiyo ya 16 bora huku timu nyingine zikiwa ni pamoja na Cameroon, Ghana Nigeria, Morocco na Senegal. Katika mechi tatu za hatua ya makundi Algeria imefungwa mara moja, imetoka sare mara moja na imeshinda mara moja. Hadi inamaliza hatua hiyo ya makundi Algeria ina pointi 4, na kufunga magoli 6.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako