• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Hatua ya mtoano kwa Algeria na Nigeria

    (GMT+08:00) 2014-07-04 10:28:22
    Wiki iliyopita katika kipindi hiki cha Jamvi uchambuzi wa timu za Afrika zinazocheza kombe la dunia nchini Brazil, tulizizungumzia timu za taifa za nchi zote tano zinazoshiriki michuano hiyo. Na vile vile tukaona nchi gani iliyoingia hatua ya mtoano na ipi iliyofungasha virago baada ya mechi za hatua ya makundi. Jumla ya nchi tatu zilitolewa katika hatua ya awali au ya makundi zikiwemo Ghana, Ivory Coast na Cameroon. Na nchi mbili zilizoendelea mbele katika hatua ya mtoano zilikuwa ni Algeria na Nigeria, sasa leo hii tutazungumzia hatua ya mtoano ilikuwa vipi kwa nchi hizo mbili.

    Kama tulivyosema awali nchi mbili tu za Afrika ndizo zilivuka hatua ya makundi na kucheza mechi za mtoano. Mechi zote mbili zilichezwa siku ya jumatatu ambapo Nigeria walivaana na Ufaransa na Algeria wakicheza na Ujerumani. Hata hivyo katika mechi zote mbili matokeo hayakuwa mazuri kwa waafrika kwani matumaini yalikwisha kabisa baada ya timu zote mbili kutolewa kwenye michuano hii.

    Sasa tuiangalie Nigeria ambayo jumatatu ya tarehe 30 ilicheza na Ufaransa kwenye hatua ya mtoano. Katika mechi hiyo Nigeria ilichabangwa magoli mawili kwa bila tena katika dakika 11 za mwisho, matokeo hayo yanaumiza moyo sana hususan ikizingatiwa kuwa Nigeria ilionekana kumiliki mpira katika kipindi cha pili. Lakini tunaweza kusema kuwa matayarisho ya Nigeria katika hatua hiyo ya timu 16 bora, yalikuwa yameingiliwa na mambo mengi. Kwanza ni posho wanalodai kutoka kwenye chama cha soka cha nchi hiyo, vilevile ushindi dhidi ya Bosnia- Hercegovina ambao ni wa pekee kwenye kundi lao F na pia kati ya mechi 11 za kombe la dunia. Hivyo kuingia kwao tunaweza kusema kuwa ni kwa mashaka ambako kulizua wasiwasi kuhusu kama kweli itafanikiwa kufuzu na kuendelea hatua ya robo fainali.

    Kama tulivyosema awali timu ya Nigeria safari hii haikuwa na ari na mshikamano ule unaoneshwa na timu zinazocheza michuano mikubwa kama hiyo. Kwanza kocha wa timu Stephen Keshi alikuwa akilalamika sana kwamba hauingwi mkono kabisa na wananchi na baadhi ya wachezaji, lakini mbali na hayo huko nyuma pia alidai kuwa haheshimiwi hivyo mara tu baada ya michuano ya kombe la mataifa ya Afrika alitaka kujiuzulu, lakini waziri wa michezo wa nchi hiyo alimshawishi aendelee kuifunza timu hiyo. Kutokana na kufanya vibaya kwenye kombe hili la dunia sasa ameamua kujiuzulu kabisa. Kwa hiyo matatizo yalianzia ndani ya timu kabla hata ya kufika uwanjani.

    Mbali na kocha huyo kujiuzulu, nahodha wa timu Joseph Yobo naye amejiuzulu kucheza mechi za kimataifa, baada ya kuingiza mpira wavuni kwenye lango lake mwenyewe. Baada ya kuhisi amefanya kosa kubwa lililoigharimu nchi hiyo itolewe kwenye michuano katika hatua ya mtoano, akaamua kujiuzulu soka ya kimataifa. Nigeria imeshinda mechi moja tu kati ya mechi 12 za kombe la dunia, pia imeshindwa mara nane na kutoka sare mara tatu. Kama ilivyo kwa makocha wengi, baada ya mechi hiyo kocha wa Nigeria Keshi naye alilalamika kuwa refarii alifanya makosa mengi tu na kwa kiasi Fulani aliegemea upande wa Ufaransa.

    Kama ilivyo Nigeria, Algeria nayo pia wiki hii imeyaaga mashindano hayo baada ya Kung'olewa katika muda wa ziada ilipocheza na Ujerumani kwa mabao 2-1. ingawa imetolewa lakini tunaweza kusema kuwa Algeria imekufa kishujaa, kwani ilijitahidi kulinda lango lake huku ikihaha kuliona lango la Ujerumani, na ndio maana hadi mpira unamalizika katika muda wa kawaida yaani dakika 90, timu zote mbili hazikufanikiwa kuona lango la mwenziwe. Hata hivyo katika muda wa ziada ingawa Aljeria walijitahidi sana lakini kile kisasi kilichokuwa kikizungumzwa sana kilishindwa kutekelezwa baada ya kuzidiwa nguvu katika dakika 92 na 119. juu ya yote hayo Mbweha hao wa jangwani hawakukata tamaa na hatimaye walifanikiwa kuingiza bao moja na la pekee kwao.

    Hata hivyo kumekuwa na uvumi mwingi kuhusu Algeria kushindwa siku hiyo, kwa vile mwezi wa ramadhani umeanza na wachezaji wengi wa kikosi hicho ni waisalamu watu wakaanza kusema sababu ya kushindwa ni saumu, lakini kipa wa Algeria Rais M'Bolhi yeye amekanusha madai hayo kwamba walishindwa kwa kuwa walikuwa dhaifu kwa saumu. M'Bolhi amesisitiza kuwa Saumu haikuchangia hata kidogo wao Kushindwa kwani wao wamesha zoea kucheza hata wakiwa kwenye mfungo wa ramadhani. Mbali na hayo Kabla ya mechi hiyo kulikuwa na ubishi baada ya kocha wa Algeria Vahid Halilhodzic kukataa kuulizwa maswali kuhusiana na mfungo wa ramadhan. Na vilevile alikataa kutaja idadi ya wachezaji wake ambao wanafunga.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako