• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Timu zilizoingia nusu fainali

    (GMT+08:00) 2014-07-14 16:22:37

    Wiki iliyopita katika kipindi hiki cha Jamvi uchambuzi wa timu zinazocheza kombe la dunia nchini Brazil, tulizizungumzia timu za taifa za nchi mbili za Afrika zilizoshiriki michuano hiyo hadi hatua ya mtoano. Timu hizo ni Nigeria na Algeria. Na vile vile tukaona jinsi zilivyofanya kwenye hatua hiyo, ambapo tulisema Algeria ilitolewa lakini ilijikaza kiume baada ya kufungwa na Ujerumani kwa mabao 2-1. lakini mbali na Algeria pia tuliichambua Nigeria iliyocheza na Ufaransa katika hatua hiyo ya timu 16 bora, ambayo nayo ilitolewa kwa kufungwa magoli 2-0, na kuhitimisha ushiriki wan chi za Afrika katika michuano hii mikubwa. Leo hii tutaziangalia timu zilizoingia nusu fainali na kuangalia kidogo matokeo ya robo fainali.

    Sasa tuanze kuangalie kidogo hatua ya robo fainali ilikwendaje halafu tutaanza kuzichambua timu zilizocheza nusu fainali. Katika hatua ya robo fainali jumla ya timu 8, ambapo Ufaransa ilicheza na Ujerumani ambayo ilitoka kifua mbele kwa bao 1-0, vile vile Brazil ilivaana na Colombia, lakini bahati mbaya Colombia ilitolewa nje ya michuano hiyo baada ya kufungwa mabao 2-1, pia Argentina ilikwaana na Ubelgiji, ambapo Argentina ilisonga mbele kwa kuichabanga Ubelgiji bao 1-0, na hatimaye robo fainali ikaishia baada ya kushuhudia mechi kati ya Uholanzi na Coratia ambapo Coratia ilitolewa kwa njia ya mikwaju ya penalti 4-3. kwa hiyo kwa ujumla baada ya mechi hizo timu nne zikasonga mbele ambapo Jumanne na Jumatano zilicheza mechi za nusu fainali.

    Katika hatua ya nusu fainali tulishuhudia maangamizi makubwa zilipocheza Brazil na Ujerumani, kwani ndoto ya Brazil ya kombe la dunia ilimalizika kwa njia ya kutia aibu kubwa na ya kikatili, baada ya Ujerumani kuwavuruga vibaya wenyeji hao katika mechi ya nusu fainali. Wingu la simanzi liliigubika Brazil, hususan baada ya pale Ujerumani ilipoanza kuporomosha mvua ya magoli matano ndani ya dakika 29 za mwanzo mbele ya umati wa mashabiki ambao hawakuamini macho na masikio yao uwanjani hapo.

    Katika kipindi cha pili cha mauaji hayo kwa Brazil Ujerumani ilihitimisha kwa kuongeza mabao mawili, na baada ya fedheha kubwa mashabiki wa Brazil waliamua kuanza kushangilia kila pasi ya Ujerumani. Matokeo hayo yaliwashtua na kuwaliza mashabiki wengi na wengi waliamua kukimbia muadhara uwanjani kabla hata mechi haijamalizika. Brazil walijua ndoto yao ya kombe la dunia inaweza kumalizika lakini hakuna aliyetarajia kwamba itamalizika namna hii. Katika dakika ya 90 Oscar aliamua kupunguza jazba na machozi ya mashabiki wa Brazil kwa kuingiza goli ambalo halikufaa chochote mbele ya Ujerumani. Hadi kipenga cha mwisho kinapulizwa matokeo yalikuwa 7-1.

    Katika nusu fainali hiyo kati ya Brazil na Ujerumani ingawa mambo yalienda kombo kwa Brazil lakini Ujerumani iling'ara sana. Kwani iliweka historia kubwa ambayo haitasahaulika milele ya kuichabanga magoli saba Brazil, lakini mbali na hilo pia katika mechi hiyo tukio jingine kubwa lilitokea baada ya Mshambuliaji wa Ujerumani Miroslav Klose kuvunja rikodi ya kuwa mchezaji aliyefunga magoli mengi zaidi katika historia ya kombe la dunia kwa kuingiza goli lake la 16. Klose ambaye alikuwa na magoli 15 yaliyokuwa sawa na mshambuliaji wa zamani wa Brazil Ronaldo wakati alipoifunga Ghana mapema kwenye michuano hii mikubwa, sasa ameshampita na kuchukua nafasi ya kileleni kabisa.

    Nusu fainali nyingine iliyochezwa juzi ni kati ya Uholanzi na Argentina. Timu zote mbili zilicheza zikiwa makini mno na kupelekea hadi dakika 120 yaani muda wa kawaida na ule wa ziada unamalizika hakuna timu iliyoona lango la mwenzake. Hata hivyo kwa vile ni lazima apatikane mshindi kwenye mechi hiyo, hivyo ililazimika mechi hiyo kuamulia kwa mikwaju ya penalti ambapo mlinda mlango wa Argentina Sergio Romero alikuwa kama kuku anayelinda watoto wake kwani alililinda lango lake na kufanikiwa kuzuia mashuti mawili ya penalti yaliyopigwa na Ron Vlaar na Wesley Sneijder na kuifanya nchi yake iondoke kifua mbele huku ikijikatia tiketi ya kucheza fainali siku ya jumapili ambapo itavaana tena na Ujerumani kama vile mwaka 1986 na 1990 ambako wakati huo ilikuwa Ujerumani Magharibi. Argentina imewathibitishia watu kuwa hawako sahihi kwani walikuwa hawajafikiria kama nchi hiyo itaweza kufika fainali, lakini sasa imefika kwa mara ya tano na huku wakiwania kupata taji kwa mara ya tatu.

    Kwa upande wa Uholanzi ambayo sasa imeshindwa kutwaa kombe la dunia hata baada ya kufuzu kwa nusu fainali tatu mfululizo itachuana dhidi ya wenyeji Brazil siku ya jumamosi kuamua mshindi wa tatu. Hata hivyo inaonekana kuwa mechi hiyo haifagiliwi sana kwani Kocha wa Uholanzi Louis Van Gaal amesema mechi ya kumtafuta mshindi wa tatu katika kombe la dunia sio jambo la haki kabisa. Amesisitiza kuwa kwa miaka 10 sasa anongelea suala la mechi hii kwamba haipaswi kuchezwa kwani kitu kibaya zaidi kuna hatari ya kushindwa mara mbili kwenye nusu fainali na mshindi wa tatu. Van Gaal anaamini kuwa kuna zawadi moja tu yenye maana kwenye michuano hii ambayo ni kuvishwa taji la ubingwa.

    Argentina imejikatia tiketi ya kucheza mechi ya fainali siku ya jumapili baada ya kuilaza Uholanzi kwa njia ya mikwaju ya penalti katika mechi ya nusu fainali huko mjini Sao Paulo. Argentina na Ujerumani sasa zimerejesha historia ya kucheza fainali kama mwaka 1986 na 1990 ambapo wakati huo ilikuwa Ujerumani Magharibi. Hii ni mara ya tatu Ujerumani na Argentina kukutana katika fainali ya kombe la dunia, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1986 nchini Mexico, Argentina ikashinda 3-2 kisha wakapatana tena mwaka 1990 nchini Italia na Ujerumani ikalipiza kisasi kwa kuinyoa Argentina bao 1-0. Kwa sasa Ujerumani inapewa nafasi kubwa ya kuondoka na kombe baada ya kuiharibu Brazil, na vilevile kuonekana kwamba kikosi cha safari hii kiko imara zaidi. Argentina nao wanataka kuuthibitishia ulimwengu kwamba bado wanatosha mboga kwani wengi hawakufikiria kama timu hiyo kama hata itafika fainali.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako