• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • fainali iliyochezwa jana jumapili kwa huko Brazil

    (GMT+08:00) 2014-07-14 16:23:27

    Wiki iliyopita katika kipindi hiki cha Jamvi uchambuzi wa timu zinazocheza kombe la dunia nchini Brazil, tulizizungumzia timu za taifa za nchi zilizoingia hatua ya robo fainali na vile vile tukachambua kwa upana mechi za nusu fainali ambapo tulisema tulishuhudia maangamizi makubwa kwa Brazil ilipofungwa na Ujerumani. Pia tuliizungumzia Uholanzi ambayo nayo ilitolewa ingawa kwa taabu na Argentina na kupelekea mechi ya fainali kuvaana miamba miwili kutoka Amerika Kusini Argentina na Ulaya Ujerumani. Leo hii tutaangalia mechi ya kumsaka mshindi wa tatu ambayo ilichezwa jumamosi na hatimaye tutaiangalia fainali iliyochezwa jana jumapili kwa huko Brazil na leo hii kwa muda wa Beijing

    Kama tulivyosema awali kwanza tutupie mechi ya kumsaka mshindi wa tatu iliyochezwa jumamosi, mechi hii ilikuwa kati ya wenyeji Brazil na Uholanzi. Katika mechi hii Uholanzi ilimaliza ikiibuka na ushindi na kuchukua nafasi ya tatu katika kombe la dunia huko Brazil baada ya kushindilia msumari wa moto ndani ya donda la wenyeji Brazil walipowacharaza mabao 3-0 mjini Brasilia. Mashabiki wa Brazil waliwazomea wachezaji wao akiwemo kocha Luiz Fellipe Scolari kwa kufanya vibaya katika mechi hizi mbili za mwisho. Ingawa Brazil ilifungua mechi hiyo kwa kasi lakini ikafungwa bao la kwanza kwenye dakika ya pili kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Robin va Persie baada ya Nahodha Thiago Silva kumtega Arjen Robben nje ya eneo lakini refarii kutoka Algerian Djamel Haimoudi akaamua kumwadhibu kwa kadi ya njano na penalti dakika mbili tu baada ya mechi hiyo kuanza badala ya kumwonesha kadi nyekundu.

    Kwa upande wa Uholanzi mashambulizi yao yalizaa matunda katika dakika ya 15 baada ya David Luiz kuokoa mkwaju kwa kichwa uliokuwa unaelekea wavuni lakini ukamwangukia Daley Blind naye akaurejesha humohumo. Kila mtu uwanjani aliifurahia Brazil walipofanya mashambulizi kwenye lango la Uholanzi lakini kila mara walipofika katika eneo walikosa makali na kushindwa kupangua safu ya ulinzi ya Uholanzi. Lakini walichokifanya Uholanzi ni kuendelea kulinda ngome yao na kila walipopata fursa walifanya mashambulizi kwenye lango la Brazil ambao walionekana imara tofauti na walipocheza na Ujerumani. Jambo la kuhuzunisha ni kuwa katika mechi yao ya mwisho wakati jina la Scolari lilipotajwa baada ya kutajwa kikosi cha Brazil, alipokewa kwa kuzomewa wakati mechi hiyo dhidi ya Uholanzi ilipokuwa inaendelea kila alipoonekana kwenye skrini uwanjani hapo alizomewa.

    Kushindwa huko kwa Brazil kwenye mechi ya kumsaka mshindi wa tatu inamaanisha kuwa kwa mara ya kwanza Brazil imeshindwa mechi mbili mfululizo ikiwa nyumbani tangu mwaka 1940. Kocha wa Brazil ameelezea mechi mbili za mwisho kama ni tukio baya zaidi kumtokea maishani, ambapo hadi sasa kibarua chake bado kipo kwenye hali ya utata kwani hajajua kama chama cha soka cha nchi hiyo kitamuongezea muda wa kuendlea na kuwa na timu au kitamwachilia mbali na kusaka kocha mpya atakayerudisha hadhi na heshima ya Brazil kisoka. Katika michuano ya kombe la dunia Brazil imeshinda mara 3, imetoka sare mara 2, ambapo na Chile walishinda kwa penalti, na kushindwa mara 2.

    jana jumapili kombe la dunia lilifikia ukingoni, baada ya Ujerumani kutawazwa kuwa mabingwa wa dunia kwa mara ya nne. Timu zote mbili zilijipanga vizuri na kuhakikisha zinachukua ushindi huo ndio maana hadi muda wa kawaida unamalizika hakukuwa na majibu yoyote kwa pande zote mbili. Hata hivyo muda wa ziada ulizaa matunda kwa Ujerumani baada ya Mario Gotze kuonesha ufundi wake maridadi kabisa kwa kuingiza goli dakika saba tu kabla ya mpira kuingia kipindi cha hatua ya mikwaju ya penalti na kuweza kuwanyang'anya tonge mdomoni Argentina kwa kuwapa kichapo cha goli 1-0 kwenye fainali hiyo. Licha ya Argentina kumchezesha mchezaji mwenye kipaji Lionel Messi, lakini walishindwa kuwajibu wajerumani ambao wamechukua taji kwa mara ya kwanza tangu walipowashinda waargentina haohao huko Rome miaka 24 iliyopita.

    Mafanikio hayo yanaifanya timu ya Joachim Low kuwa ya kwanza kutoka Ulaya kunyakua taji hilo kubwa duniani katika Amerika Kusini. Ujerumani walilazimika kujipanga vizuri baada ya kumpoteza kiungo wao Sami Khedira kufuatia kujeruhiwa katika mazoezi ya kupasha viungo moto na badala yake nafasi hiyo ikachukuliwa na Christoph Kramer. Ni mafanikio makubwa kwa kocha Low ambaye sio tu ameweza kupeleka kombe nyumbani, bali pia ameondoa rikodi ya Ulaya ya kukosa mataji michuano ianpochezwa katika ardhi ya Amerika Kusini. Wajerumani ambao miaka minne iliyopita walifungwa kwenye hatua ya nusu fainali, sasa wamekamilisha mabadiliko kwa kuwa kikosi chenye wachezaji wanaoibukia kama vile Manuel Neuer, kiungo Mesut Ozil, mlinzi Mats Hummels, nahodha Philipp Lahm, Thomas Muller, Toni Kroos and hata Khedira aliyejeruhiwa.

    Jana pia kwenye michuano hiyo zilitolewa tuzo kwa wachezaji mbalimbali ambapo

    schambiliaji wa Colombia James Rodriguez ametunukiwa kiatu cha dhahabu baada ya kumaliza akiwa mfungaji mwenye magoli mengi katika kombe la dunia. Rodriguez mwenye miaka 23 ambaye anchezea klabu ya Monaco ameingiza magoli 6 kwenye jumla ya mechi 5 ilizocheza Colombia ambayo ilifikia hatua ya robo fainali na kutolewa na wenyeji Brazil. Rodriguez amemaliza mbele ya mshambuliaji wa Ujerumani Thomas Muller aliyeingiza magoli matano huku upande wake ukinyakua ubingwa wa dunia. Naye Lionel Messi aliyepata mpira wa dhahabu kwa kuwa mchezaji bora kwenye mashindano hayo, yupo nafasi ya tatu pamoja na Neymar wa Brazil na mshambuliaji wa Uholanzi Robin van Persie ambao wamefunga magoli manne kila mmoja. Magoli ya Rodriguez yameisaidia Colombia kusonga mbele zaidi kuliko ilivyokuwa kwenye michuano ya nyuma. Naye Manuel Neuer wa Ujerumani ameshinda glovu ya dhahabu kwa kuwa mlinda mlango bora, huku kiungo wa Ufaransa Paul Pogba mwenye miaka 21 akinyakua tuzo ya mchezaji bora mdogo. Kwa upande wa Afrika hakuna hata mchezaji mmoja aliyeteuliwa kuwania tuzo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako