• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Siku ya kwanza ya mwaka mpya wa jadi wa China

    (GMT+08:00) 2015-02-11 14:33:07

     

    Sikukuu ya Spring ni mwaka mpya kwa kalenda ya jadi ya China, ambayo ni sikukuu kubwa kabisa katika jamii ya Wachina walioko kila pembe ya dunia. Sikukuu ya Spring ni ishara ya kumalizika kwa muda mrefu wa siku za baridi kali na kuwadia kwa majira ya Spring, ambapo uhai na ustawi hurudi katika sehemu ya kaskazini ya dunia hii. Baada ya kuishi na baridi kali kwa zaidi ya miezi mitatu, binadamu wanaokaa sehemu ya kaskazini mwa dunia wanatamani sana majira ya Spring yafike, majira ambayo baridi huanza kupungua, mimea ya kila aina inachipuka na maua yanachanua. Nchi inayotegemea kilimo kama China, majira ya Spring pia ni mwanzo wa shughuli za kilimo kila mwaka, wakulima wanaanza kupanda mbegu mashambani ili wapate mavuno mazuri baadaye. Hivyo wachina wana mila na desturi ya kusherehekea sikukuu hiyo kwa shamrashamra.

     

    Sikukuu hiyo ina historia ndefu. Inasemekana kuwa hadi sasa Sikukuu ya Mwaka mpya wa jadi wa China imekuwa ikiadhimishwa kwa miaka elfu nne nchini China. 

    Wachina wana kalenda yao iitwayo kalenda ya kilimo, ambayo inatungwa kwa majibu wa mzunguko wa mwezi na mzunguko wa jua. Katika jamii ya Wachina, maandalizi ya sikukuu ya Spring huwa yanaanza baada ya kuingia mwezi wa 12 kwa kalenda ya kilimo, haswa pilikapilika nyingi zinafanyika katika kipindi kuanzia tarehe 23 hadi 30, yaani siku ya mkesha wa sikukuu. Katika kipindi hicho, wachina wana desturi ya kufanya usafi na kununua vitu mbalimbali ili kuukaribisha mwaka mpya. Watu wanasafisha nyumba, kufua nguo, mifarishi, mashuka ya kitandani, mapazia. Halafu, wanaanza kupamba nyumba. Wanapenda kubandika karatasi nyekundu zenye maandishi ya baraka mlangoni, picha maalumu za mwaka mpya madirishani, na kutundika taa kubwa nyekundu. Wachina wanapenda kubandika andiko la neno la kichina "FU", maana yake ni baraka, na pia wanabandika picha ya mungu wa jiko milangoni. Yote hayo yanaonesha hali ya furaha ya sikukuu.

     

    Vilevile kila familia inafanya manunuzi makubwa kwa ajili ya sikukuu hiyo. Watu hununua vyakula vya aina mbalimbali, zawadi kwa jamaa na marafiki, na nguo mpya kwa ajili ya watoto.

    Sherehe zinaanza rasmi katika siku ya mkesha wa mwaka mpya. Siku hiyo watu wote wa familia wanakusanyika pamoja, hata wale wanaofanya kazi au kusoma katika miji mingine hurudi nyumbani kukutana na wazazi na ndugu zao ili kusherehekea pamoja sikukuu hiyo. Kwa hiyo mkesha wa mwaka mpya pia unaitwa usiku wa kukusanyika kwa wanafamilia. Siku hiyo Wachina wa kaskazini wana desturi ya kula Jiaozi, chakula inachofanana na maandazi, lakini kilipikwa kwa kuchemshwa, na wachina wanaoishi sehemu ya kusini wana desturi ya kula Nian'gao, chakula kinachotengenezwa kwa unga wa wali. Wazee wanawazawadia watoto pesa kama ishara ya baraka. Ifikapo alfajiri ya siku ya kwanza ya mwaka mpya, watu wanatoka nje kulipua fataki na kuukaribisha mwaka mpya wa jadi wa China.

    Hadithi ya "Nian"

     

    Katika enzi za kale, kuna mnyama wa kutisha aitwaye "Nian", anapenda kula vitu vyote vyenye uhai, ndege, wanyama, wadudu, hata binadamu. Watu walimhofia sana. Lakini watu wakagundua huyu "Nian" anakwenda sehemu yenye watu wengi kila baada ya siku 365, anakuja baada ya jua kuzama na kuondoka mara jua likichomoza. Katika siku anayokuja "Nian", watu wanaandaa chakula mapema, kuwahifadhi kuku na ng'ombe, na kufunga milango. Watu wote wa familia wanakusanyika pamoja na kula pamoja. Baada ya chakula, hawathubutu kulala, wanaongea na kutiana moyo. Desturi hiyo ikarithiwa hadi leo katika mkesha wa mwaka mpya.

    Wakati wa siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza watu huvalia rasmi kuwasalimia wazee wa familia, na kuwatakia afya njema na maisha marefu. Katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa jadi wa China, watu hawatembeleani. Kuanzia siku ya pili wanakwenda kuwatembelea jamaa na marafiki. Wanapokutana huamkiana "Heri ya Mwaka Mpya", au "Heri ya Sikukuu ya Spring" na kuwakaribisha ndani kwa peremende, chai na vitafunwa na kuulizana hali ya maisha. Kama majirani walikuwa na mkwaruzano katika mwaka uliopita, wanapaswa kuondoa kinyongo na kutembeleana katika sikukuu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako