• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mwaka 2015: Mwaka wa Mbuzi

    (GMT+08:00) 2015-02-11 14:40:27

     

    Kwa mujibu wa kalenda ya kilimo ya China, leo ni siku ya pili ya mwaka mpya wa 2015, ambao pia ni mwaka wa Mbuzi. Katika kipindi hiki, tutazungumzia kuhusu mzunguko wa miaka na chanzo cha mwaka wa mbuzi katika kalenda hiyo ya jadi ya China.

    Katika utamaduni wa Kichina, kundi la wanyama 12 linatumika katika kuhesabu mwaka. Kila mnyama anawakilisha mwaka mmoja, na kila baada ya miaka 12 mzunguko huo unarudia. Utaratibu wa Wanyama hao 12 ni panya, ng'ombe, chui, sungura, dragoni, nyoka, farasi, mbuzi, kima, kuku, mbwa, na nguruwe.

    Njia hiyo ya kuhesabu mwaka ilianza kutumika Enzi ya Han Mashariki, yaani mwaka 25 hadi mwaka 220 baada ya Kristo, hadi leo imekuwa na historia ya karibu miaka elfu 2, na bado inatumiwa na wachina kuhesabu mwaka na umri.

    Kuna hadithi nyingi zinazoeleza vyanzo vya utaratibu huo, moja kati yao inasema hivi: Zaidi ya miaka 4700 iliyopita, wakati mfalme wa asili wa wachina Huangdi alipotaka kuchagua wanyama 12 kuwa walinzi wa kasri, paka alimwomba panya kumsaidia kujiandikisha, lakini panya alisahau, hivyo paka hakuchaguliwa, kwa hiyo kuanzia hapo paka na panya wakawa maadui. Tembo pia alikwenda kushiriki shindano hilo, lakini paka aliingia kwenye pua yake, hivyo tembo alifukuzwa. Wanyama wengine mwanzoni walimchagua ng'ombe kuwa wa kwanza kwenye safu, lakini panya aliruka kwenye mgongo wa ng'ombe, na nguruwe alitembea polepole, ndiyo maana panya alichukua nafasi ya kwanza, nguruwe akawa wa mwisho. Chui na dragon walikuwepo na kupangwa nyuma ya panya na ng'ombe. Naye Sungura pia alikwenda kugombea, akashindana mbio na dragoni, na hatimaye kumshinda dragoni. Mbwa alitaka kuangalia shindano hilo, alimwuma sungura hivyo aliadhibiwa na kushika nafasi ya pili kutoka mwisho. Nyoka, farasi, mbuzi, kima, na kuku pia walishindana, na mpango wa mwisho wa safu hii, ukawa kama ifuatavyo, panya, ng'ombe, chui, sungura, dragoni, nyoka, farasi, mbuzi, kima, kuku, mbwa na nguruwe.

     

    Hadithi nyingine inayoeleza kwa nini mbuzi alichuguliwa kwenye safu hii inasema hivi:

    Katika zama za kale, katika ulimwengu wetu hakukuwa na nafaka, binadamu waliishi kwa kula mboga za majani na nyasi, kwa hiyo walikumbwa na njaa kali na utapiamlo.

    Siku moja katika majira ya Mchipuko, mbuzi mmoja alitoka peponi na kushuka chini, na kugundua maumivu yanayowasumbua binadamu. Alipouliza sababu akaambiwa kuwa binadamu hawakujua kupanda mimea ya nafaka. Kutokana na moyo wake mwema, mbuzi huyo aliahidi kuleta nafaka kidogo safari ijayo. Kumbe wakati huo, nafaka zilipatikana tu kwenye mashamba ya kasri la peponi, lakini mfalme wa peponi hakutaka kutoa nafaka hizo kwa binadamu. Baada ya mbuzi huyo kurudi peponi, usiku mmoja aliingia kisirisiri kwenye mashamba, akaiba nafaka za aina tano na kuzificha mdomoni, kabla ya kucha akashuka tena ulimwenguni kuwapatia binadamu mbegu za nafaka hizo, na kuwafahamisha namna ya kuzipanda.

    Kwa kufuata maelekezo ya mbuzi huyo, binadamu wakapanda mbegu hizo na baada ya miezi kadhaa wakavuna nafaka. Ili kumshukuru mbuzi huyo, watu wakaamua kufanya sherehe kubwa ya kumkumbuka, na desturi hiyo bado inafuatwa kwenye baadhi ya sehemu za vijijini nchini China.

    Lakini sherehe hizo kubwa zikagunduliwa na mfalme wa peponi, baada ya kujua sababu yake, mfalme akakasirika sana na kuwataka walinzi wake wamchinje mbuzi huyo na nyama yake kuwapa binadamu wale.

    Mwaka wa pili, katika mahali ambako mbuzi huyo alichinjwa, nyasi zilianza kukua na halafu kulikuwa na mbuzi wadogo, na baada ya hapo, mbuzi wakaanza kuwepo ulimwenguni na kuishi kwa kula nyasi, na wanatoa sadaka nyama na maziwa yao kwa biandamu.

    Wakati binadamu waliposikia mpango wa mfalme wa peponi wa kuchagua wanyama 12 maalum na kuwapatia hadhi ya miungu, binadamu wote walimpendekeza mbuzi, na hatimaye mbuzi akawa mnyama wa nane katika safu hii.

     

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako