• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mtindo mpya wa kusherehekea mwaka mpya wa jadi wa China

    (GMT+08:00) 2015-02-11 14:55:25

    Siku ya mwaka mpya wa jadi wa China ni sikukuu ya jadi inayothaminiwa sana na wachina. Katika miaka zaidi ya elfu moja iliyopita, wachina walikuwa na mila na desturi mbalimbali za kusherehekea sikukuu hiyo, lakini kutokana na maendeleo ya jamii na uchumi, mila na desturi hizo pia zimebadilika. Hasa baada ya China kutekeleza sera ya Mageuzi na ufunguaji mlango mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita, uchumi wa China uliendelezwa haraka, bidhaa mbalimbali za kielektroniki zimeingia katika maisha ya kila siku ya wachina, na zimeleta urahisi kwa maisha ya watu na pia kuathiri mtindo wa jadi wa kusherehekea sikukuu. Mbali na hayo, wachina hivi sasa wana pesa zaidi kuliko zamani, hivyo wana uwezo ziadi wa kuchagua jinsi ya kusherehekea sikukuu hiyo muhimu. Vijana waliozaliwa baada ya mwaka 1980, wamekua katika kipindi cha utekelezaji wa sera ya mageuzi na ufunguaji mlango, hivyo ni rahisi kwao kupokea jambo au wazo jipya ikilinganishwa na wazazi wao. Vijana hao waliolewa na teknolojia za kisasa wana mtindo wa kipekee wa kusherehekea sikukuu hiyo.

     

    Kwenye mila na desturi ya jadi ya China, siku ya mkesha wa mwaka mpya wa kichina, kwa kawaida wachina wanajumuika pamoja kutazama sherehe ya mwaka mpya wa kichina inayoandaliwa na kituo cha televisheni ya taifa, CCTV. Lakini siku hizi vijana hawaridhiki na mtindo huo wa zamani , wanaona kuwa hauvutii tena, na hauna ubunifu wowote, hivyo wanatafuta burudani nyingine kwenye mtandao wa Internet. Kuna tovuti nyingi za mtandao wa Internet zinazoandaa sherehe zao, ambazo zinashirikisha watumiaji wa mtandao huo. Watu wanaweza kuamua kuangalia wanachopenda, kupiga kura na kutoa maoni moja kwa moja kwenye tovuti hiyo, pia vijana wengine wanachagua kuangalia filamu au tamthilia usiku kucha.

    Zamani kila ilipofika sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa kichina, wachina walikuwa wanatembeleana na kupeana salamu ya mwaka mpya, lakini baada ya simu za mezani na simu za mikononi kuanza kutumika, watu wanapigiana simu na kupeana salamu hizo. Siku hizi vijana hawapigiani simu wala hawatumiani ujumbe mfupi, wanapenda kupeana salamu kupitia vifaa vya mawasiliano kwenye simu za mikononi ikiwemo Wechat, ambayo ni maarufu nchini China na pia katika nchi nyingi. Watu wanaweza kutuma ujumbe kwa maandishi, sauti, picha hata video fupi kwa marafiki na jamaa, pia wanaweza kuonana kupitia kifaa hicho. Kama tujuavyo, wachina wanawapa watoto bahasha nyekundu iliyowekwa pesa ndani ili kuwapa salamu zao. Kuanzia sikukuu ya mwaka mpya wa jadi mwaka jana, watu wanaweza kutumia Wechat kuwatumia marafiki bahasha nyekundu. Wanaopewa bahasha nyekundu wanaweza kuhifadhi pesa hizo kwenye kadi yake ya Benki.

    Utalii umekuwa mtindo mpya wa kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya wa jadi hapa China. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na idara ya utalii ya taifa, katika kipindi cha mwaka mpya wa jadi mwaka jana, sehemu mbalimbali za China zilipokea watalii milioni 231, ambayo iliongezeka kwa asilimia 14 ikilinganishwa na ya mwaka juzi. Kwa upande wa safari za nje ya nchi, idadi ya watalii wanaoshiriki kwenye safari za makundi ya utalii zilizoandaliwa na mashirika ya utalii ilifikia milioni 4.725, ambayo iliongezeka kwa asilimia 18.

     

    Kati ya watalii walioenda nje ya China katika kipindi cha sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China, wengi walikwenda na familia, na wachina wenye umri wa miaka kati ya 35 hadi 45 wanaonekana wakipenda zaidi kutalii nje ya China kuliko wachina wa umri mwingine. Safari visiwani bado inapendwa zaidi na watalii, visiwa vinavyochaguliwa zaidi ni vile vilivyoko nchi za Asia ya kusini mashariki kama vile kisiwa cha Phuket, kisiwa cha Bali, kisiwa cha Jeju na kisiwa cha Boracay. Mkuu wa taasisi ya utalii ya China Dai Bin anasema, familia nyingi zinaamua kusafiri katika sikukuu hiyo muhimu, jambo ambalo linasaidia kuongeza mawasiliano na kupendana kati ya wanafamilia. Takwimu zilizopatikana kwenye soko la Utalii pia zimeonesha mabadiliko, watu wa sehemu ya mashariki mwa China wanapendelea kusafiri nchini Japani na Korea Kusini, na watu wa sehemu nyingine wanapenda zaidi Singapore, Malaysia na Thailand. Hivi sasa nchi nyingi zaidi zimefikia makubaliano na China ya kutoa visa za muda mrefu au kurahisisha utaratibu wa kuomba visa, ili kuwavutia watalii wengi zaidi kutoka China.

     

    Sikukuu hii ya mwaka mpya wa jadi wa kichina ni sikukuu muhimu inayokutanisha familia nchini China, lakini katika miaka ya hivi karibuni, gharama ya kusherehekea sikukuu hiyo inazidi kupanda, hali ambayo imeleta kero kwa vijana ambao hawana nguvu imara ya kiuchumi.

    Zhao Tianwei ni kijana kutoka Harbin anayefanya kazi hapa Beijing. Kila ifikapo mwaka mpya wa jadi, anatumia sehemu ya mapato ya mwaka mmoja kulipia gharama za kusherehekea sikukuu hiyo akirudi maskani. Zhao alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, gharama hiyo kubwa inaifanya furaha ya kurudi nyumbani iwe furaha yenye shinikizo. Alisema, kwa kawaida aliporudi maskani alitakiwa kupeleka zawadi kwa jamaa zao na kununua vyakula na zawadi kwa familia yake. Katika kipindi cha sikukuu hiyo, alitakiwa kutembelea jamaa na marafiki na kuwaalika chakula. Kwa ufupi tu ni kwamba, pesa imekuwa kiini cha sikukuu hiyo. Zhao anasema, kwa kawaida gharama hiyo inafika Yuan elfu 20 ambayo ni sawa na dola elfu 3.7 za kimarekani.

    Hata hivyo vijana wengi wanaonesha hamu ya kurudi nyumbani. Kama wimbo moja unaojulikana hapa China ulivyoimba, "Kila mmoja anatakiwa kurudi nyumbani kusherehekea mwaka mpya bila ya kujali kama ana pesa au la." Kwa vijana wanaofanya kazi mbali na makwao, kurudi nyumbani kusherehekea sikukuu pamoja na wazazi ni jambo muhimu zaidi katika mwaka mzima.

    Kuhusu hali hiyo, wataalamu wanaona kuwa sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China ni mila na desturi ya jadi ya China, maana yake ni ndugu na jamaa kujumuika kwa pamoja. Na baadhi ya vijana wanataka kuonesha upendo wao kwa wazazi, hivyo huenda wakafanya manunuzi yanayozidi uwezo wao na kujiwekea shinikizo kubwa. Lakini ukweli ni kwamba wazazi hawazingatii watoto watatoa zawadi gani au pesa ngapi, wanachotaka ni kusherehekea sikukuu hiyo pamoja na watoto wao.

     

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako