• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mila na desturi kuhusu vyakula wakati wa mwaka mpya wa jadi wa China

    (GMT+08:00) 2015-02-11 15:14:20

     

    Katika jamii ya Wachina, kuna mila na desturi mbalimbali kuhusu vyakula wakati wa kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya, yaani sikukuu ya Spring. Na nyingi zinatokana na hadithi maelfu ya miaka iliyopita, na hadithi hizo zinapokezana na wachina wa kizazi baada ya kizazi.

    Wakati wa enzi ya Chunqiu, zaidi ya miaka 2,000 iliyopita, ofisa mwandamizi wa dola la Wu aitwaye Wu Zixu kabla ya kufariki aliwaambia wafuasi wake kuwa, "baada ya mimi kufariki, kama dola letu likikumbwa na taabu, na watu wetu wakikosa chakula, nendeni kwenye kuta za mlango wa Xiangmen na kuchimba chini futi tatu, mtaweza kupata chakula." Muda si mrefu baada ya kufariki kwake, dola la Wu lilishambuliwa na dola la adui, na mfalme alishindwa kwenye mapambano na kuzingirwa ndani ya mji mkuu, chakula kikaisha na wanajeshi na watu wakafa kutokana na kukosa chakula.

    Wakati huohuo, wafuasi wa Wu Zixu wakafuata aliyosema marehemu na kwenda mlango wa Xiangmen kuchimba chini, na kweli walipata chakula ambacho kina sura inayofanana na matofali yaliyojengwa kuta zilizolinda mji. Kumbe hii ni mbinu ya marehemu Wu Zixu ya "kuweka akiba ya chakula ili kukabiliana na taabu" wakati aliposimamia ujengzi wa mji. Baadaye kila mwaka, familia zote huko zinapika chakula hiki ili kumkumbuka Wu Zixu.

     

    Je, mnajua hiki ni chakula gani? Kwa Kichina kinaitwa "Niangao". Katika sikukuu ya Spring, Wachina wanaoishi katika sehemu ya kusini wana desturi ya kula Niangao. Baadhi ya watu wanasema, desturi hiyo ilianzia enzi ya Zhou, na hadi sasa imekuwa na historia ya miaka zaidi ya 3,000. Lakini kweli ilianzia lini na kuvumbuliwa na nani, sasa haijulikani.

    Katika sehemu ya kusini ya China, watu wanaandaa Niangao kwa ajili ya Sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China.

    "Matamshi ya Niangao ni sawa na neno lingine lenye maana nzuri ya kutakia mafanikio makubwa zaidi mwaka baada ya mwaka. Licha ya kuwa na maana nzuri, chakula hicho pia ni kitamu sana. Kinatengenezwa kwa unga wa mchele unaonata, nakumbuka mama yangu pia anatia karanga na jujube ndani ya unga wa mchele, halafu anapika kwa mvuke kwa saa kadhaa, hadi leo nakumbuka kuwa nilikuwa nikiomba kuonja mara baada ya kusikia harufu."

     

    Jiaozi ni aina ya chakula chenye umbo unaofanana na maandazi. Katika sehemu ya kaskazini ya China, kula Jiaozi ni desturi muhimu wakati wa Sikukuu ya Spring, lakini desturi hiyo ina tofauti katika sehemu mbalimbali. Katika baadhi ya sehemu wanakula Jiaozi katika siku ya mkesha wa mwaka mpya, katika baadhi ya sehemu wanakula Jiaozi katika siku ya kwanza ya mwaka mpya kwa kalenda ya kilimo ya China, na katika baadhi ya sehemu za milimani kaskazini mwa China wana desturi ya kula Jiaozi kila asubuhi kuanzia tarehe 1 ya mwaka mpya hadi tarehe 5.

    "Mimi ni mwenyeji wa Beijing. Tunakula Jiaozi katika siku ya mkesha wa mwaka mpya. Wanafamilia wote tunashiriki kutengeneza Jiaozi, na hivi ndivyo Jiaozi inavyotengenezwa: kwanza kanda unga wa kutengeneza vifungio vya Jiaozi, halafu funga vijazo, ambavyo ni vya aina mbalimbali, kama nyama, mayai, chakula cha baharini na mboga za majani. Njia ya kawaida ya kuandaa Jiaozi ni kuichemsha kwenye maji, na baadaye kuitoa na kuila kwa sosi iliyochanganywa na siki, kitunguu swaumu na mafuta ya ufuta. Pia kuna njia za kukaanga na kuoka Jiaozi."

    Kama Niangao, Jiaozi pia ina maana yake nzuri. Matamshi ya Jiaozi ni sawa na neno lenye maana ya mpito kati ya mwaka wa zamani na mwaka mpya. Aidha, kwa kuwa umbo la Jiaozi linafanana na sarafu ya kale ya China, kwa hiyo mabakuli ya Jiaozi yanayowekwa mezani yana mithilisha "kupata utajiri katika mwaka mpya".

     

    Wakati Sikukuu ya Spring inapowadia, watu ambao wako mbali na maskani yao wanarudi makwao, na kujumuika na jamaa zao. Kula chakula cha usiku cha mkesha wa mwaka mpya ni muda wa furaha zaidi kwa kila familia katika Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi. Katika mkesha wa mwaka mpya, vitoweo vingi vizuri vilivyoandaliwa kwa ajili ya mwaka mpya vinawekwa mezani, na wanafamilia wote wanakaa kuzunguka meza kula pamoja. Faraja iliyojaa mioyoni mwao haielezeki. Wanafurahia chakuka kitamu na mazingira ya furaha. Kuna vyakula vya aina mbalimbali, vya baridi, vya kuchoma, na viburudisho, lakini kuna vitu viwili ambavyo kwa wakati huo haviwezi kukosekana: cha kwanza ni chungu cha kujipikia chakula mezani, na kingine ni samaki. Chungu cha kujipikia chakula mezani kinachemka na kutoa mvuke na joto, ambapo inaonesha hali motomoto. Samaki kwa Kichina anaitwa Yu, na matamshi yake yanafanana na matamshi ya neno lingine lenye maana ya kubaki, hivyo linamithilisha "ziada baada ya mwaka', yaani "kuwa na zaidi ya unachohitaji kila mwaka". Watu wengine pia wanaita figili "Caitou", matamshi yake yanafanana na yale ya neno lenye maana ya kila la heri, hivyo figili pia hukaribishwa sana kwenye meza ya chakula wakati wa mkesha wa mwaka mpya wa jadi wa China. Watu pia wanapenda sana vyakula vinavyokaangwa kama vile kamba mti na kombe wa kukaangwa, wanataka kumaanisha ustawi kama "moto unaowaka na mafuta yanayochemka". Kitoweo cha mwisho mara nyingi ni kitindamlo, ikiwa na maana ya kutakiana maisha matamu yenye furaha katika siku za usoni.

    Wakati wa sikukuu hii ya kufurahi, mtoto mmoja anayeitwa Wu Yulun pia anatoa salamu ya mwaka mpya wa jadi. "Mimi ni Wu Yulun, jina langu la Kiingereza ni pink rabbit, napenda kula mboga na karoti, wakati wa sikukuu ya Spring, kumbuka kula mboga, na msile nyama nyingi, kwani si vizuri kwa afya yenu, nawatakia muwe na afya nzuri!"

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako