• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Magulio ya hekalu

    (GMT+08:00) 2015-02-11 15:20:08

     

    "Miaohui" ni maneno ya Kichina. Tukitafsiri moja kwa moja neno la "miao", maana yake ni hekalu, na neno "hui" maana yake ni gulio. Magulio ya hekalu ni mila na desturi ya kidini ya kabila la Wahan nchini China. Yanahusu shughuli za kidini, na hufanyika karibu na mahekalu katika sikukuu za kidini au siku maalum, kama vile mwaka mpya wa jadi wa China.

    Hapo zamani, magulio ya hekalu yalishughulika na mambo ya kidini tu. Katika zama za kale, China ilikuwa na dini ya Kibudha na dini ya Kidao ambayo ni imani ya kienyeji. Kila upande ulifanya juhudi zote kujitangaza na kushindana kuvutia waumini. Mbinu moja iliyotumiwa ilikuwa kujenga mahekalu mbalimbali. Mbali na hayo, kila upande uliingiza burudani katika shughuli za kidini, yakiwemo maonesho ya ngoma, michezo ya kuigiza na maonesho mengine yaliyowafurahisha watu. Shughuli hizo za burudani zilifanyika nje ya mahekalu.

    Kutokana na maendeleo ya uchumi na mahitaji ya mawasiliano ya watu, biashara ilianza kufanyika kwenye magulio hayo, na baadaye shughuli za burudani pia ziliongezwa. Shughuli hizo ziliwavutia watu wengi sana, hata ambao si waumini wa dini walipenda kutembelea matamasha hayo. Kutembelea magulio ya hekalu wakati wa mwaka mpya wa jadi wa China ni jambo muhimu kwa Wachina, hususan wanaoishi katika sehemu ya kaskazini ya China.

     

    Wimbi la watu liliwavutia zaidi wafanyabiashara ambao walianza kuuza vyakula na bidhaa mbalimbali kwenye magulio ya hekalu katika mwaka mpya wa jadi wa China. Kwa mfano, hapa Beijing vyakula vinavyouzwa kwenye magulio ni pamoja na mishikaki ya matunda yaliyozungukwa na sukari, utumbo wa kukaanga, mishikaki ya nyama ya mbuzi na kababu za nyama ya ng'ombe, kwa upande wa bidhaa, ni pamoja na vigurudumu vya kuzungushwa na upepo ambavyo ni vitu vya kuchezea watoto na sanamu za sungura.

    Watu wanaweza kujiburudisha kwa kushiriki kwenye michezo ya kurusha viringi na kulenga shabaha. Maonesho ya ngoma mbalimbali pia yanafanyika kwenye gulio la hekalu.

    Hivi sasa magulio ya hekalu hayahisiani kabisa na shguhuli za kidini, wala si lazima yafanyike nje ya mahekalu. Bali yamebadilika kuwa shughuli za burudani wakati wa mwaka mpya wa jadi wa China. Mwaka huu magulio ya hekalu yanafanyika katika bustani mbalimbali hapa Beijing, na kila moja lina umaalumu wake. Baadhi yao yanawaalika wasanii wa jamii wafanye maonesho ya sarakasi, ngoma za jadi, maonesho kuhusu utamaduni wa chai, sanaa ya maandiko ya Kichina n.k.

     

    Kwa mfano, kwenye gulio la hekalu linalofanyika katika bustani ya Ditan, watalii wanaweza kuangalia maonesho ya jadi ya mji wa Beijing, ikiwemo mchezo wa diabolo, maonesho ya mazingaombwe, na sanaa ya uongeaji, pia wanaweza kuangalia wasanii wakitengeneza vitu vya kisanii vikiwemo ufinyanzi, picha za kukatwa, vivuli vya picha zilizotengenezwa kwa ngozi na vitambaa vya jadi.

    Kwenye gulio la hekalu linalofanyika katika bustani ya Daguanyuan, watalii wanaweza kutazama michezo mingi ya kuigiza ambayo ni hadithi mbalimbali za riwaya maarufu ya "Ndoto katika Jumba Jekundu" iliyoandikwa na Bw. Cao Xueqin katika enzi ya Qing, miaka 200 iliyopita. Karibu filamu 200 zilikuwa zimechezwa katika bustani hii iliyojengwa kwa mujibu wa riwaya hii.

     

    Magulio ya hekalu yanayofanyika katika bustani za Chaoyang na Shijingshan ni tofauti kidogo, pamoja na kuonesha utamaduni wa jadi wa China, yanaonesha utamaduni, usanii na vyakula vya nchi mbalimbali duniani. Magulio hayo si kama tu yanawawezesha Wachina kuangalia mandhari ya mitindo ya nchi nyingine, kusikiliza muziki za kigeni, kuonja vyakula vyenye ladha ya nchi za nje, na kucheza michezo ya nchi za nje bila kwenda ng'ambo, bali pia yanawawezesha wageni wanaoishi hapa Beijing kusherehekea sikukuu ya kichina kwa furaha na kujisikia kama wako nyumbani. Kwenye bustani ya Shijinshan, watalii wanaweza kuonja vyakula mbalimbali vya mitindo ya nchi za nje ziwemo mapishi ya kifaransa ya nyama ya mbavu, chaza waliookwa kwa desturi ya kiingereza, upishi wa mishikaki wa Norway, nguruwe waliookwa kwa njia ya kijerumani, pizza, na chapati za mtindo wa kifaransa.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako