• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Amepanda mti wa uzima nchini Sierra Leone

    (GMT+08:00) 2015-03-24 16:31:23

    Katika pwani ya Sierra Leone, kuna mti unaoitwa "mwavuli", ambao huvumilia maji ya chumvi na ukame, na unawakinga watu dhidi ya mvua kali na upepo. Katika ardhi hiyo hiyo kuna wachina wanaofanana na mti huo. Wao ni madaktari wa China wanaotoa msaada nchini Sierra Leone.

    Katika miaka 42 iliyopita, toka mwaka 1973 kikundi cha kwanza cha madaktari wa China kilipokwenda nchini humo, madaktari wa China walikuwa wanatoa huduma za matibabu. Bw. Wang Yu ni mmoja wa madaktari hao nchini Sierra Leone.

    Mwezi Aprili mwaka 2013, akiwa na mawazo ya "kupanua upeo wake", Wang Yu alipanda ndege ya kuelekea Afrika. Huko alianza kazi ya kutoa misaada ya matibabu katika hospitali ya kiserikali ya Kingharman Road mjini Freetown kwa miaka miwili. Kutokana na vita vya ndani vilivyodumu kwa muda mrefu, miundo mbinu nchini Sierra Leone iliharibiwa vibaya, uchumi wa nchi hiyo ukaelekea kuanguka, mfumo wa matibabu ya umma ukawa dhaifu. Katika nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 6.1, idadi ya madaktari waliojiandikisha haikufikia 100. Daktari Wang Yu anasema ingawa hospitali ya Kingharman Road ilikuwa ni moja ya hospitali nzuri zaidi ya kiserikali mjini Freetown, ilikabiliwa na taabu za kukatika kwa maji na umeme mara kwa mara, kiasi kwamba umeme ulikatika wakati upasuaji unaendelea, na hivyo iliwabidi watumie tochi. Wakati mwingine pia mashine za usafi hazikuweza kufanya kazi kutokana na ukosefu wa maji. Kutokana na hali mbaya ya matibabu, hata kama magonjwa yasiyo makubwa yangeweza kuwasumbua sana wenyeji. Ingawa alikuwa amejiandaa kwa kiasi fulani, lakini baada ya kuanza na kazi, Wang Yu alibadilisha maoni yake juu ya kazi za kutoa misaada ya matibabu barani Afrika.

    "Baada ya kuanza kazi barani Afrika, nilijihisia kihalisi kazi hiyo siyo tu inanisaidia kupanua upeo wangu, bali imeniletea jukumu. Nilipoonana macho kwa macho na wagonjwa, nahisi jukumu zito. Na wakati huo huo, niliona uamuzi wangu wa awali ulikuwa ni sahihi, Afrika inatuhitaji, tunapaswa kufanya juhudi kubwa kadiri ya uwezo wetu kuwasaidia watu wa Afrika."

    Akitambua maana ya jukumu lake la kuwasaidia Waafrika, daktari Wang Yu alikuwa mchangamfu zaidi kazini. Imefahamika kuwa, mbali na kikundi cha madaktari wa China, kuna madaktari wawili tu wa Sierra Leone na wauguzi kadhaa katika hospitali hiyo ya Kingharman Road. Kwa hiyo madaktari wa China wanabeba kazi nyingi. Wanafanya kazi kwa siku sita kwa wiki. Akiwa daktari wa matibabu ya ndani, Wang ana kazi nyingi zaidi kuliko wenzake. Anawapokea wagonjwa zaidi ya 20 kwa siku, na katika miaka miwili, idadi ya wagonjwa aliowatibu imezidi elfu tano. Ingawa wagonjwa wako wengi na kazi ni nzito, Wang Yu siku zote ni mwangalifu, mvumilivu na mwenye makini kwa kila mgonjwa. Yeye ni wa mwisho kuondoka kazini kila siku, wakati fulani alichelewa kula chakula. Wang Yu anasema, ingawa alichoka sana alipokuwa kazini, furaha yake kubwa ni kuona wagonjwa wakiondoka kwa tabasamu.

    Sierra Leona ni moja ya nchi zilizoko nyuma kimaendeleo zaidi duniani, watu wake ni maskini sana, baadhi yao hawana pesa za kutosha za huduma za matibabu. Akiwapokea wagonjwa kama hao, Wang Yu hujitahidi kupunguza gharama zao za matibabu, hata kuwapatia dawa bure. Na kwa wale wanaohitaji kutibiwa mara moja lakini hawana uwezo wa kulipia matibabu, daktari Wang alitumia pesa zake mwenyewe. Wang anasema, kuwatibu wagonjwa ni wajibu wa madaktari na wanapaswa kuwaheshimu maisha ya wagonjwa bila kujali kama wao ni matajiri au maskini. Bw Wang Yu amepata uaminifu na kukaribishwa na wakazi wa huko kupitia vitendo vyake halisi, na wenzake wote wanamuunga mkono, wamezoea kumwita kwa jina lake la Kiingereza David. Mwuguzi wa hospitali ya Kingharman Road Bibi Veronica Lansana anasema:

    "Daktari David ni daktari hodari zaidi katika hospitali yetu. Yeye ni mwangalifu sana kwa wagonjwa, kila anapowapatia dawa anawaelezea kwa makini, ili kuhakikisha wanazitumia kwa usahihi. Kuna siku tulikuwa na mgonjwa aliyeumwa sana, lakini hakuwa na pesa za kununua dawa, daktari David alitoa pesa zake mwenyewe. Wakati mgonjwa huyo alipolazwa, mbali na sisi wauguzi kumtunza, daktari David alikwenda wodini kumpima na kumwuliza hali yake mara kwa mara hadi alipopona na kutoka hospitali. Daktari David anajali sana wagonjwa wake, afya yao ni jambo analofuatilia zaidi. Hivyo wananchi wenzetu wakija hospitali kwetu, walipendelea kutibiwa naye. Hata yeye huongea na wagonjwa kwa upole, na kuwachukulia kama familia yake."

    Mwezi Mei mwaka jana, ugonjwa wa Ebola ulianza kuambukizwa nchini Sierra Leone. Wang Yu pamoja na wenzake walishiriki kwenye mapambano dhidi ya mambukizi hayo. Awali idadi ya wagonjwa waliokwenda hospital ya Kingharman Road haikupungua, miongoni mwao huenda kulikuwa na watu waliotoka maeneo yenye maambukizi ya Ebola. Na wakati ule mavazi ya kukinga virusi vya Ebola yalikuwa hayajafika hospitali, iliwabidi madaktari wa China wavae glovu na barakoa, kama hatua rahisi za kujikinga dhidi ya kuambukizwa na virusi vya Ebola. Tarehe 22 mwezi Julai Wang Yu alimpokea mwanamke aliyeugua tumbo. Lakini matokeo ya upimaji yaliyotolewa siku iliyofuata yalionesha kuwa mgonjwa huyo ana virusi vya Ebola. Yeye alikuwa mgonjwa wa kwanza wa Ebola kuthibitishwa mjini Freetown, na kwa bahati mbaya alikufa siku ya tatu njiani alipopelekwa kwenye hospitali iliyowatibu wagonjwa wa Ebola. Dereva aliyepeleka mgonjwa huyo hospitali vilevile alikufa kutokana na kuambukizwa Ebola.

    Daktari Wang Yu aliwekwa kwenye chumba cha karantini kwa siku 21, na kwa bahati nzuri afya yake ikaendelea kuwa kama kawaida, na akarudi kazini. Wang Yu alisema, mara alipopata habari ya mgonjwa aliyemtibu kuwa na virusi vya Ebola, alisikia kama kupigwa na umeme, kwani anaelewa vizuri kwamba ana nafasi kubwa ya kuambukizwa kutokana na kuwa karibu na mgonjwa. Katika siku 21 alipowekwa karantini, alikuwa na wasiwasi na huzuni, lakini ni upendo wa familia yake, wafanyakazi wenzake wa China na Sierra Leone uliompa moyo wa kukabiliana na hofu na upweke. Alisema baada ya kipindi hicho maalum, anachukulia kwa uzito mkubwa fursa ya kuwaponya wagonjwa na kuokoa maisha ya wale walio kwenye hatari ya kufa.

    "Mimi ni daktari, katika kukabiliana na maambukizi ya Ebola, la kwanza napaswa kufanya ni kuwaokoa wagonjwa, siwezi kujiepusha kama wengine. Ni sawa na wanajeshi wanaokwenda vitani, milio ya risasi ikisikika au kuna sehemu inayopaswa kuikalia, ni lazima wasonge mbele kupambana na maadui. Naona hii ni hali ya kawaida. Sisi madaktari tunapaswa kwenda mstari wa mbele wakati huu, huu ni wajibu wetu."

    Uchangamfu na ukarimu vinampatia Wang Yu marafiki wengi nchini Sierra Leone. Wakazi humsalimia kwa ukarimu kwa kumwita jina lake la Kiingereza "Jambo, daktari David." Pia hualikwa kwenye karamu zinazoandaliwa na wafanyakazi wa hospitali, mezani mwake ofisini huwa na bidhaa za kienyeji, na anapokumbwa na tatizo wakazi wengi hujitolea kumsaidia. Mwenzake daktari Wang Guohong anasema:

    "Anawasaidia marafiki waafrika, hususan wauguzi, wafanyakazi, watu wanaozalisha umeme na madereva wa hospitali yetu, wao ni marafiki wakubwa. Hii inasaidia kuhimiza urafiki kati ya China na Afrika, na kuongeza uelewa wa watu wa Afrika kuhusu kikundi chetu cha matibabu, na madaktari wa China."

    Wakati wa muda wake binafsi, Wang Yu anakuwa na shughuli nyingi za kushughulikia zaidi ya miti 100 aina ya mwavuli, aliyopanda kando ya pwani. Alisema hiyo inatia mizizi chini ya ardhi yenye hali mbaya ya ukame, lakini inaweza kukua na kuleta kivuli, pia kuboresha mandhari ya pwani. Anaona madaktari wa China wana sifa inayofanana na miti hiyo. "Historia yetu ya kutoa misaada ya matibabu barani Afrika imekuwa na miaka 50 ambapo madaktari na wauguzi wa China wanaendelea kutoa huduma kwa watu wa Afrika katika hali ngumu, watu 50 kati yao wamepoteza maisha yao wakiwa kazini. Moyo huu wa kushikilia na kujitolea unatutia moyo, sisi madaktari wa China tunatoa mchango kwa Afrika kama mti wa mwavuli unavyohudumia watu kwenye mazingira ya chumvi na ukame. Naona ingawa kuja kwetu hapa hakuwezi kubadilisha kabisa hali duni ya mfumo wa huduma za matibabu nchini Sierra Leone, lakini tunaweza kuchangia uwezo wetu, na kuwaonesha wenyeji upendo wetu na matumaini."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako