• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mji unaostawi kutokana na ujenzi wa reli

    (GMT+08:00) 2015-08-10 19:52:37
    Wahenga husema "treni ikinguruma, dhahabu inakuja". Msemo huo unazungumzia umuhimu wa sekta ya uchukuzi katika kuhimiza maendeleo ya uchumi.

    Mji wa Zhengzhou unajulikana kama "mji ulioletwa na treni", ikimaanisha kwamba maendeleo ya mji huo yanahusiana kwa karibu na shughuli za uchukuzi kwa njia ya reli, na pia inaonesha umuhimu wa kijiografia wa mji huo katika sekta ya uchukuzi nchini China. Reli inayounganisha miji ya Beijing na Wuhan ambayo ilifunguliwa katika miaka ya 20 ya karne iliyopita inapita kwenye mji wa Zhengzhou, na kutia nguvu mpya ya uhai kwenye mji huo uliopo tangu zamani.

    Kama Bonde la Ufa na Ikweta zinavyokutana nchini Kenya, Reli ya Beijing-Guangzhou inayounganisha sehemu za kaskazini na kusini mwa China na Reli ya Lanzhou-Lianyungang inayounganisha sehemu za magharibi na mashariki mwa China zinakutana mjini Zhengzhou. Ukiwa kwenye makutano ya reli hizo mbili muhimu, mji wa Zhengzhou una kituo kikubwa zaidi barani Asia cha upangaji wa mabehewa ya treni, kituo kikubwa zaidi nchini China cha kupakia mizigo ya treni na kituo cha kipekee nchini China kinachokutanisha reli za treni yenye mwendo kasi wa kilomita 350 kwa saa.

    Kituo cha treni cha Zhengzhou Kaskazini ni kituo chenye pilika nyingi zaidi duniani ambacho kinapitisha treni 500 kwa siku. Hali ya kituo hicho ni mfano tu wa pilika za sekta ya usafiri kwa njia ya reli nchini China. Aidha mji wa Zhengzhou unaendelea kujitokeza kama kituo muhimu cha kiuchumi katika reli mpya ya kimataifa inayounganisha Asia na Ulaya (kutoka Lianyungang, China hadi Rotterdam, Uholanzi). Pia mji huo unaendelea kuonesha umuhimu wake ukiwa kituo muhimu cha uchukuzi wa mizigo na usafiri wa abiria kinachokutanisha usafiri wa reli na barabara.

    Mtandao wa reli ya treni ya kasi nchini China unaendelea kuundwa na kitovu chake kipo mjini Zhengzhou, huku kituo cha ugavi cha kimataifa kinachojumuisha reli, barabara na viwanja vya ndege kikiibuka katika mji huo.

    Tarehe 28 Desemba mwaka jana treni ya kasi kati ya Zhengzhou na Kaifeng, mji mwingine mkoani Henan ilianza kutoa huduma. Huduma hiyo ikiwa pamoja na huduma nyingine za reli, imerahisisha zaidi usafiri kati ya mji wa Zhengzhou na miji mingine mkoani humo.

    Ukiwa mji unaostawi kutokana na maendeleo ya reli, Zhengzhou unaendelea kuwa kifua mbele na kuikumbatia dunia, huku ukiendelea kutoa mchango kwa maendeleo ya sekta ya reli nchini China.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako