(New York, 26 Septemba 2015)
Mwenyekiti mwenza,
Waheshimiwa wenzangu,
Nina furaha kubwa kuhudhuria mkutano wa leo. Ikiwa Umoja wa Mataifa unaadhimisha miaka 70, hii ni fursa muhimu nay a kipekee kwa viongozi wa dunia kukutana pamoja mjini New York kuratibu mwelekeo wa maendeleo ya baadaye.
Maendeleo yanabeba matumaini na maisha halisi ya watu wa nchi zote. Inajumuisha uhalisia wa hadhi zao na haki zao. Ni katika mtazamo huo ndipo tuliweka Malengo ya Maendeleo ya Milenia miaka 15 iliyopita katika juhudi za kuboresha maisha ya mamilioni ya watu.
Katika miaka hiyo, tumeshuhudia ukuaji endelevu duniani na athari mbaya za mgogoro wa fedha duniani. Tumeona kuibuka kwa kasi kwa nchi zinazoendelea na ukosefu wa uwiano uliopo kati ya Kaskazini na Kusini. Wakati tukifurahia ukweli kuwa zaidi ya watu bilioni 1.1 wameondokana na umasikini, hatuwezi kuacha kuwa na wasiwasi mkubwa kuwa zaidi ya watu milioni 800 bado wanalala njaa kila siku.
Katika ngazi ya kimataifa, amani na maendeleo vinaendelea kuwa mambo muhimu ya wakati huu. Ili kukabiliana vizuri na changamoto mbalimbali tunazokumbana nazo, ikiwemo mgogoro wa hivi karibuni wa wakimbizi barani Ulaya, hakuna suluhisho muhimu kuliko kutafuta amani na maendeleo. Kutokana na kukabiliwa na ongezeko la changamoto na matatizo, tunatakiwa kushikilia kithabiti maendeleo kama ufunguo wetu muhimu, kwa kuwa ni kwa kupitia maendeleo ndio tunaweza kutatua chanzo cha migogoro, kulinda haki za kimsingi za binadamu, na kutimiza matumaini ya wananchi wetu ya maisha bora ya baadaye.
Mwenyekiti mwenza,
Waheshimiwa wenzangu,
Ajenda ya Maendeleo baada ya mwaka 2015 iliyopitishwa kwenye mkutano huu inatoa mpango makini wa maendeleo ya dunia na kutoa fursa mpya kwa ushirikiano wa kimataifa. Tunatakiwa kuchukulia hili kama sehemu mpya ya mwanzo, kuandaa mpango ulio wa usawa, wazi, jumuishi na unaoongozwa na maendeleo ya uvumbuzi, na kutafuta kutimiza maendeleo ya pamoja ya nchi zote.
-Tunahitaji kuhakikisha usawa wa maendeleo. Nchi zote zinatakiwa kuwa na haki sawa kama washiriki kwenye, na wachangiaji kwa, na kunufaika na maendeleo ya dunia. Hii haitakiwi kuwa fursa inayopatikana tu kwa nchi moja au nchi kadhaa, na kukosekana kwa nyingine nyingi. Nchi zinaweza kutofautiana katika uwezo wao kwa maendeleo na maendeleo waliyofikia katika kutimiza malengo, lakini wana nia ya pamoja, na wana gazi sawa, ingawa majukumu tofauti, ya kuwajibika. Ni muhimu kuimarisha usimamizi wa uchumi wa dunia, kuzidisha uwakilishi na sauti ya nchi zinazoendelea, na kutoa haki sawa kwa nchi zote kushiriki kutoa maamuzi ya kimataifa.
-Tunakiwa kuhakikisha maendeleo ya wazi, na kugawa faida zake kwa pande zote. Kutokana na mwelekeo thabiti wa utandawazi wa kiuchumi duniani, nchi zote zinatakiwa kufungua milango yao na kuruhusu vyanzo vya uzalishaji kutiririka kwa uhuru na utaratibu duniani kote. Ni muhimu kwa nchi zote kushikilia utaratibu wa kibiashara wa pande nyingi, kujenga uchumi wa wazi, na kugawana faida kupitia mashauriano na uratibu wa pamoja. Tunapaswa kuheshimu uamuzi wa kila mmoja wa njia ya kujipatia maendeleo, kujifunza kutokana na uzoefu wa mwingine, na kuleta njia hizi tofauti pamoja katika mafanikio, na hivyo kutoa matunda mazuri ya maendeleo kwa watu wote.
-Tunatakiwa kuhakikisha maendeleo yapande zote ili kuifanya misingi kuwa thabiti zaidi. Maendeleo hatimaye yatawasaidia watu. Wakati tunatafuta kuondoa umasikini na kunua kiwango cha maisha, ni muhimu kwetu kushikilia usawa na haki ya jamii na kuhakikisha kuwa kila mmoja anapata fursa na faida za maendeleo. Juhudi zinatakiwa kufanywa ili kuleta uwiano kwa maendeleo ya uchumi, jamii, na mazingira, na kutimiza mwingiliano wa maisha ya amani kati ya binadamu na jamii na kati ya binadamu na mazingira ya asili.
-Tunatakiwa kuhakikisha maendeleo yanayoongozwa na uvumbuzi ili kufikia upeo wa juu zaidi. Uvumbuzi ni kichocheo kikubwa. Matatizo yanayotokana na mchakato wa maendeleo yanaweza tu kutatuliwa kupitia maendeleo zaidi. Nchi zote zinapaswa kuangalia mageuzi na uvumbuzi kama njia za kufikia uwezo wao wa juu, kujenga injini zenye nguvu za ukuaji, na kunoa uwezo wao wa ushindani kwa kiasi cha juu.
Mwenyekiti mwenza,
Waheshimiwa wenzangu,
Ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 ni orodha kuu ya mpango unaobeba ahadi zetu za dhati. Kuna msemo kuwa thamani ya mpango wowote uko kwenye utekelezaji wake. Hivyo basi, ninatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza zaidi juhudi zake za pamoja katika kutimiza utekelezaji wa pamoja wa Ajenda ya Maendeleo baada ya mwaka 2015, na kufanya kazi ya kutimiza lengo letu.
Kwanza, kujenga uwezo kwa ajili ya maendeleo. Maendeleo, katika tathmini ya mwisho, ni kazi ya kila nchi. Sisi Wachina tunasema. "kula kutokana na ukubwa wa tumbo lako na vaa kutokana na umbo lako" Hivyo, ni lazima kwa kila nchi kuunda mikakati yake ya maendeleo inayoendana na uwezo wake na hali ya taifa lake. Jumuiya ya Kimataifa ina kazi ya kusaidia nchi zinazoendelea kukuza uwezo wake na kuwaunga mkono pamoja na kuwapa msaada kulingana na mahitaji yao.
Pili, Kuboresha mazingira ya kimataifa kwa maendeleo. Amani na maendeleo vinakwenda sambamba. Nchi zinapaswa kushirikiana pamoja katika kuimarisha amani ya kimataifa, kuendeleza maendeleo ya amani na kupata amani kupitia maendeleo. Mazingira ya nje ya kimuundo yanahitajika katika maendeleo endelevu. Kwa hiyo taasisi za kimataifa za Fedha zinatakiwa kupanga mageuzi ya utawala wao, na mashirika ya maendeleo ya kimataifa yanahitaji kuongeza usambazaji wao wa rasilimali.
Tatu, kuboresha ushirikiano kwa ajili ya maendeleo. Nchi zilizoendelea zinapaswa kuheshimu ahadi zao na kutekeleza majukumu yao kwa wakati. Jumuiya ya Kimataifa, ikiwa inaendeleza jukumu lake la ushirikiano wa Kusini na Kusini kama njia kuu, inapaswa kufanya kazi ya kuimarisha ushirikiano wa Kusini na Kusini na pande tatu, na kuhimiza sekta binafsi na wadau wengine kubeba jukumu kubwa katika ushirikiano huu.
Nne, kuimarisha mfumo wa ushirikiano kwa ajili ya maendeleo. Nchi zinahitaji kuongeza ushirikiano wa sera zao za kiuchumi ili kuepuka kadiri iwezekanavyo athari mbaya za ziada. Mashirika ya kikanda yanapaswa kuongeza ushirikiano wao na kuongeza nguvu ya ushindani wao wa jumla kwa kutumia nguvu za ndani ya kanda. Umoja wa Mataifa lazima uendelee kutimiza jukumu lake la uongozi.
Bw. Mwenyekiti Mwenza,
Waheshimiwa wenzangu,
Katika miaka zaidi ya 30 na zaidi tangu China ianze kufanya mageuzi na kufungua mlango, nchi yetu imefuata njia ya maendeleo yenye umaalumu wa Kichina – njia ambayo imechaguliwa kwa kufuata hali ya taifa letu. Kupitia mafanikio yetu na kuwaondoa watu milioni 439 kwenye umasikini na maendeleo ya kupigiwa mfano tuliyoyapata katika maeneo kama vile ya elimu, afya na mambo ya wanawake, tumefikia kimsingi Malengo yetu ya Maendeleo ya Milenia. Maendeleo ya China sio tu yameboresha maisha ya wachina bilioni 1.3 na zaidi, bali pia yametoa msukumo mkubwa duniani.
Zaidi ya miongo sita, China imeshiriki kikamilifu katika ushirikiano wa kimataifa. Tumezipatia nchi 166 na mashirika ya kimataifa karibu RMB bilioni 400 kwa ajili ya usaidizi wa maendeleo na kupeleka zaidi ya wafanyakazi wa misaada 600,000, ambapo zaidi ya 700 wamepoteza maisha yao wakati wanasaidia maendeleo ya nchi nyingine.
Tukiangalia siku za mbele, China itaendelea kuimarisha uwiano wa kimaadili kati ya haki na maslahi yake kwa kuweka mbele haki kabla ya maslahi. Tutaunganisha nguvu zetu pamoja na za nchi nyingine katika juhudi za makusudi za kutambua Ajenda ya Maendeleo baada ya mwaka 2015. Kutokana na hayo, ningependa kutangaza yafuatayo:
- China itaanzisha mfuko wa usaidizi kwa ajili ya ushirikiano wa Kusini na Kusini, ukiwa na msingi wa dola za Kimarekani bilioni 2 ili kusaidia nchi zinazoendelea katika utekelezaji wao wa Ajenda ya Maendeleo baada ya mwaka 2015.
- China itaendelea kuongeza uwekezaji katika nchi zenye maendeleo madogo, ikilenga kupata kiwango cha dola Bilioni 12 za Kimarekani ifikapo mwaka 2030.
- China itasamehe madeni ya mikopo isiyo na riba kwa serikali za nchi mbalimbali ambayo inapaswa kulipwa hadi mwishoni mwa 2015 inayo zidai nchi zenye maendeleo madogo, nchi zinazoendelea zisizokuwa na bandari, na nchi zinazoendelea za visiwa vidogo.
- China itaanzisha kituo cha maendeleo ya elimu cha kimataifa ili kurahisisha masomo kati ya nchi kuhusu kubadilishana nadharia na mazoezi ya maendeleo yanayoendana na hali za nchi zao husika.
- China itapendekeza majadiliano juu ya kuanzisha mtandao wa nishati ya dunia ili kurahisisha juhudi za kufikia mahitaji ya umeme duniani kwa kutumia vyanzo mbadala visivyochafua mazingira.
China pia iko tayari kushirikiana na wadau wengine ili kuleta maendelo ya haraka kwenye utekelezaji wa juhudi za "Ukanda na Barabara", kuanzisha haraka Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia na uendeshwaji wa Benki ya Maendeleo Mapya ya BRICS, na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi zinazoendelea na hali ya maisha ya watu wake.
Bw. Mwenyekiti mwenza,
Waheshimiwa wenzangu,
Sisi, watu wa China, tunatoa ahadi: ya kuimarisha nia yetu katika kutekeleza Ajenda ya Maendeleo baada ya mwaka 2015 kuwa jukumu letu kubwa, kushirikiana pamoja na Dunia kama moja, na kujitahidi kueleta maendeleo zaidi katika maendelo ya dunia.
Asante.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |