• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • SHANGHAI IPO CHINA LAKINI NI DUNIA MCHANGANYIKO

  (GMT+08:00) 2016-08-11 16:50:32

  Unaweza kufikiria kwamba labda sasa haupo tena ndani ya China bali upo katika nchi tofauti kulingana na muingiliano mkubwa wa watu wa aina zote.

  Shanghai ni jiji lenye idadi ya watu zaidi ya milioni 24 kwa takwimu za mwaka 2014. Pamoja na kwamba leo hii Beijing ndipo yalipo makao makuu ya serikali lakini bado muingiliano wake na watu wa mataifa mengine hauwezi kulinganishwa na ule wa Shanghai kwa sababu hapo wapo wazungu wengi waliozaliwa hapo na kukulia hapo ikiwa ni uzao wa tatu.

  Wazungu hao wanaongea lugha ya Kichina (Mandarin) bila mkwaruzo wowote na baada ya hapo wanaongea lugha zao za asili. Lakini pia ni mahali nilipoona kwamba Mchina na Mzungu wanafanya kazi katika chumba kimoja cha habari.

  Mazungumzo yetu na uongozi wa gazeti la "The Paper" yakatudokezea kwamba mfumo wa habari katika chombo hicho ni wa kimataifa zaidi na ndiyo maana watu hawa wanaweza kufanya kazi kwa pamoja, lengo la gazeti hilo ambalo kwa sasa limejikita katika habari za mitandaoni zaidi.

  Wakazi wa Shanghai wamezoea kuishi na watu wa mataifa ya magharibi lakini kadri siku zinavyosonga mbele ndivyo wageni wanaongezeka na ni watu wenye mitaji mikubwa na hivyo wenyeji wanalazimika kuanza kusogea pembeni kidogo pale wanapoona kwamba maisha ya mjini ni magumu kwao.

  Hata hivyo kulingana na maelezo ya wenyeji wetu halijaharibika jambo kwa wale walioamua kusogea pembeni kwa sababu huduma zote zinafika huko sawia. Huduma ya benki kwa kutumia intaneti.

  Na hata manunuzi kwa njia hiyo vimerahisisha huduma na kuna gari ndogo zinazopita huku na kule zikitoa huduma ikiwa ni pamoja na kuchukua mazao ya kilimo vijijini na kuyapeleka mijini na vile vile kubeba vifurushi vyenye bidhaa mbali mbali na kuvipeleka vijijini.

  Wafanyakazi wenye taaluma zao kwao ujio wa wageni wawekezaji ni habari njema kwa sababu ya kupanuka kwa ajira na hata uboreshwaji wa huduma.

  Utalii ndani ya maji nyakati za usiku ni kivutio cha kipekee kutokana na majengo yanayotoa mwanga wenye rangi mbali mbali na kubadilika mara kwa mara lakini hata kwa vyombo vyenyewe vinavyosafiri ndani ya maji hubadilika badilika rangi kutokana na taa zilizofungwa katika vyombo hivyo.

  Nyakati za jioni ambapo kwa kawaida watu wengi huelekea majumbani kupumzika inakuwa ndiyo wakati wa kuanza aina mpya ya burudani kwa wenyeji na wageni wa mji huu wakipita huku na kule kutafuta vyakula mbali mbali lakini pia kupanda katika mashua au kuingia katika kumbi za burudani.

  Tofauti na ilivyo kwa nchi kama Tanzania ambapo starehe kubwa ni bendi za muziki katika miji mikubwa, hapa ni sanaa za maonesho hususani sarakasi na nyimbo za kitamaduni.

  Vikundi vya sanaa vimetoa ajira kubwa kwa sababu kikundi kimoja kinaweza kuwa na waajiriwa hadi 300. Wasanii wa vikundi vya ngazi za kitaifa na kimkoa hulipwa mishahara kama ilivyokuwa kwa mfanyakazi mwingine yeyote serikalini.

  Kwa bahati mbaya kwa wasanii katika nchi za Afrika wengi hujitafutia mafunzo kila mmoja na njia zake, na ni wachache tu waliopata mafunzo maalumu ya sanaa vyuoni.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako