• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • KIVUTIO CHA JOTO JIMBO LA HAINAN, KARAHA INAPOGEUKA KUWA BARAKA

  (GMT+08:00) 2016-08-11 16:59:03

  Mwanzoni miaka michache iliyopita kulingana na maelezo ya wenyeji wetu, jimbo la Hainan hapa nchini China lilikuwa halina mvuto mkubwa kama yalivyokuwa majimbo mengine.

  Sababu kubwa ni kwamba halikuwa na hazina ya viwanda ambavyo vingeweza kuvutia wawekezaji wakubwa wa biashara. Na vile vile kulikuwa na joto kubwa tofauti na majimbo mengine, kwa kiwango kikubwa jimbo hili lilibakia kama sehemu ya makazi ya kawaida ya wanajamii.

  Hata hivyo mara baraka zikaanza kujitokeza kutokana na watalii waliokwepa baridi kali majimboni kwao ndani ya China na hata nje ya nchi hususani nchini Urusi kuanza kuhamia jimboni humo kwa muda kila wakati wa msimu wa baridi kali.

  Watu wakawa wanakuja ndani ya jimbo hilo wakiwa na mahema yao na wakati mwingine wenyeji wakawapokea watalii hao waliokwepa baridi katika makazi yao majumbani.

  Mara kuanzia mwaka 1998 hali ya jimbo hilo ikawa imebadilika kutokana na kupokea watalli wengi na kuwawekea mazingira mazuri ya makazi baada ya ujenzi wa hoteli za kitalii.

  Hata hivyo watalii hao hawakuendelea sana kula hotelini muda wote na hivyo nyakati za mchana na hata usiku walitafuta vyakula vya bei nafuu katika makazi ya watu. Hali hiyo ikasababisha Serikali ya China iwekeze katika ngoma za utamaduni ili kutoa burudani kwa watalii.

  Labda nikiinglinganisha hali hiyo na Tanzania nitasema ni katika makazi ya akina mama lishe maarufu kama 'mama n'tilie'. Hali hiyo ikaifanya Serikali ya China kufunguka macho na kuanza kuboresha hali za makazi za wananchi wa jimbo hilo hususani katika mji kuu wa jimbo hilo uitwao Haiko na hata Sanya.

  Uzoefu wa mwandishi wa makala hii baada ya kulitembelea jimbo hilo ni kwamba ghafla mfumo wa maisha umebadilishwa kutokana na kukua kwa sekta ya utalii.

  Leo wakazi wa mji wa Haiko katika maeneo yanayopendelewa na watalii wameamua kulima mazao ya chakula ambayo wana uhakika yatauzika katika msimu wa baridi.

  Pamoja na hali hiyo serikali imewajengea wananchi migahawa majumbani mwao kiasi kwamba hali ya usafi inaridhisha ikiwa ni pamoja na kugawiwa mafriji na mafriza ili waweze kuongeza kipato chao.

  Jimbo hilo limegeuka kuwa 'Hawaii ya China' ambapo katika Jiji la Sanya yamewahi kufanyika hata mashindano ya urembo ya dunia mara mbili mwaka 2010 na mwaka 2015. Hali iliyoufanya mji huo kupata hazina kubwa ya wageni na watalii katika nyanja mbali mbali.

  Serikali ya jimbo hilo imeweka masharti kwamba wawekezaji wawe na mashamba ambapo wanaweza kulima na kupata mazao ya chakula kwa ajili ya watalii na kwa matumizi yao wenyewe.

  Tayari baadhi ya wawekezaji wamechukua viwanja hivyo na kuweka hoteli na sehemu na kuchezia watoto na hata maduka ya jumla na sehemu za kufugia wanyama kama ng'ombe, mbuzi n.k.

  Itoshe hapa kusema kwamba lile joto ambalo halikupewa umuhimu wowote na hata jua lisilokatika ambalo lilikimbiwa na vijana waliokwenda katika miji mikubwa ili kutafuta maisha sasa limegeuka kuwa lulu!

  Kutokana na wimbi kubwa la watalii ilibidi kuhamisha hata uwanja wa ndege ili kutoa nafasi za uwekezaji wa hoteli za kitalii katika eneo la uwanja wa zamani, kwa hiyo Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Haikou au Haikou Meilan International Airport kama unavyofahamika zaidi ulianza kutumika mwaka 2013 ikiwa ni miaka miwili toka ulipoanza kujengwa mwaka 2011.

  Ipo miti na mazao ya ukanda wa tropiki ambayo yamehamishwa kutoka nchi za Afrika ikiwamo, kahawa na michaichai. Wenyeji wa eneo hilo wameandaliwa vyema kwa ajili ya kupokea wageni kutoka sehemu mbali na hasa katika huduma ya chakula katika migahawa iliyopo majumbani mwao.

  1. Ziara katika bustani kubwa ya miti, matunda na mboga zainazopatikana katika ukanda wa tropiki.

  2. Mwandishi wa makala hii (mwenye tai) anapojumuika na wenyeji katika kucheza ngoma za utamaduni

   

  3. Mwandishi wa makala hii akitoa ishara ya dole gumba akiwa na msanii ikiwa ni ishara ya kupata burudani tosha katika ngoma za jadi kwa watalii.

  4. Mwandishi wa makala hii akiwa na watoto waliotembelea mojawapo ya mashamba ya utalii katika Jimbo la Hainan.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako