• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Matembezi ndani ya 'jiji lililozuiliwa' yaani Forbidden City

    (GMT+08:00) 2016-08-12 10:30:34

    Na Elias Mhegera, Beijing

    Matembezi yangu mwezi Mei ndani ya kasri ya kifalme ambayo kwa sasa inaitwa Forbidden City yalinyanyua hisia zangu kutokana na kuwa nimefundisha somo la historia katika sekondari kwa miaka kadhaa iliyopita.

    Ndani ya jengo la kifalme ambalo kwa sasa ni sehemu ya vivutio vya utalii na kumbukumbu za kihistoria kuna majengo makubwa sita ambayo yalitumika kwa shughuli mbali mbali za utawala wa enzi ya Ming na Qing. Inasemekana kwamba ndani ya kasri hiyo ya kifalme waliishi hadi watu elfu kumi (10,000)

    Miongoni mwa hao walikuwa ni mfalme, malkia na pia wasaidizi wa mfalme katika shughuli za utawala, askari namaanisha wanajeshi, wataalamu wa itifaki na intelijensia, na pia walikuwamo vimada wa mfalme wasiozidi 72.

    Kwa mara ya mwisho tawala hizo ziliangushwa mwaka 1911 ingawaje mfalme na ukoo wake waliendelea kukaa hapo hadi mwaka 1924. Lakini baadaye walihofiwa kujipanga upya na kufanya mapinduzi ili warejee madarakani ndipo walifukuzwa na eneo hilo likafungwa na kupewa jina la Forbidden City, yaani jiji lililozuiliwa.

    Hata hivyo katika utawala wa ufalme si kila mtu aliyeruhusiwa kuingia ndani ya wigo wa kasri hiyo ya kifalme ambayo imejitanua kwa umbali mkubwa sana. Na hivyo, ngome hiyo ilikuwa imezuiliwa kwa maana zote, wakati wa ufalme na hata baada ya kufungwa kwa ngome nzima.

    Kasri hiyo ambayo kwa sasa inatambuliwa rasmi kwa jina la 'Jumba la Makumbusho la Kasri ya Kifalme' lina ukubwa wa mita za mraba 700,000, ndani kuna majengo yapatayo 800 na vyumba zaidi ya 9,000. Kasri hiyo kwa Kiingereza 'The Forbidden City ndiyo kubwa kuliko zote duniani.

    Ni kutokana na sifa hizo, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliitambua kasri hiyo kama mojwapo ya kumbukumbu na hifadhi za kimataifa kuanzia mwaka 1987. Sifa mojawapo kubwa ya majengo hayo ni matumizi ya mbao katika ujenzi wake.

    Ingawaje mfalme alitakiwa kuwa na vimada wasiozidi 72 lakini alitakiwa pia kuwa na mke mmoja aliyetambuliwa rasmi kama malkia, ndani ya Ikulu hiyo lipo jengo maalumu la malkia.

    Kila baada ya miaka mitatu mfalme alitakiwa kushuhudia zoezi la kuajiri maafisa wa itifaki ambao kazi yao ilikuwa ni pamoja na kupanda farasi wakiwa na mavazi maalumu, wakipambwa kwa medali na vito maalumu vya dhahabu na fedha, na kuizunguka kasri ya kifalme katika kona zake zote ikiwa pia ni mbwembwe za kuipamba ngome hiyo.

    Katika usaili huo wa kuwapa ajira vijana, watahiniwa wasiopungua 500 walipewa mafunzo maalumu kwa siku nne na kisha siku tatu za usaili zilifuata na zoezi hilo la usaili lilisimamiwa na mfalme mwenyewe.

    Kwa maana hiyo vijana hao walikaa humo ndani kwa siku zipatazo saba kwa ajli ya kazi hiyo ya mafunzo na usaili. Miongoni mwa masomo yaliyofundishwa ni pamoja na falsafa, ukakamavu, intelijensia na itifaki.

    Hata hivyo mfalme hakutakiwa kuzaa watoto zaidi ya 100 na pia ufalme mmoja haukutakiwa kuwa na wanaukoo ziaidi ya 999, kwa sababu kwa mila za Wachina mara wanaukoo wa kifalme wakitimia 1000 basi inabidi kuanzisha ufalme mwingine na ndiyo maana kwa kukwepa gharama za kuwatunza wafalme walidhibitiwa juu ya idadi ya watoto wanaoweza kuwazaa.

    Habari njema pia ni kwamba kwa sasa majengo hayo ya kifalme ni neema kwa Serikali ya China kwa sababu watu wapatao elfu tano (5000) hutembelea kivutio hicho kwa siku moja pekee.

    Asilimia 60 ni watalii wa ndani na asilimia 40 ni wageni kutoka nje. Katika miezi ya Julai na Agosti watalii hufikia hadi elfu nane kwa siku (8,000).

    Mwisho.

    1. Watalii wakiingia ndani ya ngome hiyo

    2. Mwandishi wa makala hiinaye akijitosa katika kona mabali mbali za ngome hiyo

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako