• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Milima si kigezo cha kuikimbia Tibet

  (GMT+08:00) 2016-08-12 10:36:11

  Na Elias Mhegera, Bejing

  Mara ukiambiwa kwamba unatakiwa kupimwa hali ya afya yako kabla ya kwenda Jimbo la Tibet unaweza kupatwa na mshituko wa moyo. Ndivyo ilivyokuwa kwa wanahabari wenzangu 28 kutoka Bara la Afrika hivi karibuni.

  Kizaa zaa kilianza pale tulipoanza kudokezwa kwamba Tibet ipo kwenye uwanda wa milima ya Himalaya na si kila mtu anaweza kwenda huko na asikutane na mshituko utokanao na upungufu wa hewa ya oksijeni.

  Mchujo huo haukuwa mwepesi kwa sababu kila mmoja alijiona anastahili kwenda huko lakini baada ya kufahamishwa hali ya milima basi ndipo hofu ikatanda nani aende na nani aachwe.

  Na ikafika siku ya safari na tukaelekea huko, mwandishi wa makala hii alikuwa ni mmoja wa wanahabari walioamka siku ya kwanza wakiomba kuongezewa hewa ya oksijen walau kwa siku hiyo ya kwanza kutokana na maumivu makali ya kichwa.

  Madaktari wakasema maumivu hayo yalitokana na upungufu wa hewa hiyo muhimu mwilini na hivyo mwanahabari huyu hakuwa na njia nyingine bali kuivaa mirija ya oksijeni ili kuokoa jahazi.

  Kwa haraka haraka labda mtu angeweza kusema kwamba huo ndiyo mwisho wa mambo. Lakini siku ya pili hali ilikuwa tofauti na haswa pale baadaye mwanahabari huyu alipopata nafasi ya kushiriki utalii wa vijijini.

  Ilikuwa katika kijiji cha kitalii cha Tashigang kilichaonzishwa maalumu mwaka 1998 kwa ajili ya utalii na kilimo. Leo eneo hilo ni kivutio cha wastani wa watalii wasiopungua 1000 kwa siku.

  Huko kulikuwa na wapishi waliopata mafunzo maalumu kwa ajili ya kuwapikia watalii na hata kutoa huduma nyinginezo iwapo wageni wangeamua kujipikia wenyewe.

  Kwa mfano mhusika anaweza kuamua kuchinjiwa kuku au kufuliwa nguo na mambo mengineyo ya kifamilia lakini akaamua kujipikia yeye mwenyewe. Lipo eneo la kutosha kwa ajili ya michezo mbali mbali kama vile kurusha mishale, kupanda farasi na hata kuchunga ngombe.

  Mgeni anaweza kushangazwa na ujasiri uliofanywa na serikali ya China wa kupasua barabara katikati ya milima ili kuvuka ng'ambo ya pili ambako kuna uhai mkubwa kutokana na hazina ya maji ambayo hutumika katika kilimo cha umwagiliaji hususani kwa zao la mpunga.

  Pia kuna hoteli za kitaliii ambazo sasa zimekuwa kivutio kikubwa kwa ajili ya mikutano na mapumziko kwa watu ambao wamechoshwa na kelele za magari na viwanda na hata uchafuzi wa mazingira. Wakulima wamewezeshwa kulima kulingana na mahitaji ya watalii wa ndani na wa nje pia.

  Wapo wasanii ambao wanaweza kuimba nyimbo za jadi ili mradi kuonesha utamaduni wa taifa ambao unatunzwa kwa njia za maandishi na mapokeo kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

  Kipo chuo cha kilimo na hata ufundi ili kuwaandaa vijana kwa ajili ya kujiajiri wao wenyewe badala ya kutegemea kuajriwa na serikali au mashirika.

  Kwa hakika hata kama mtu alipatwa na maumivu ya kichwa siku ya kwanza mara akiishaona mandhari nzuri ya kijiijini atayasahau yote yaliyopita.

  Wakulima wa eneo hilo wamegeuka kuwa wapishi wazuri siyo kwa sababu wamepata mafunzo pekee bali uzoefu kutokana na maombi ya wageni wanaokwenda katika jimbo hilo mara kwa mara.

  Labda kivutio kikubwa kingine kwa mtu anayetoka Afrika ya Mashariki kama ilivyokuwa kwa mwandishi wa makala hii atokaye nchini Tanzania, ni uwepo wa mionzi mikali ya jua ambayo inatumika kuzalisha nishati.

  Kutokana na uwepo huo wa nishati yapo mafriji na hata magari yanayotumia nishati ya mionzi ya jua. Lakini si hivyo tu bali hata mitambo ya ulinzi majumbani inategemea nishati hiyo na ndiyo maana mapaa takribani yote katika mji wa Lhasa makao makuu ya jimbo yamejaa paneli za kukusanya mionzi ya jua.

  Mwisho

  Pichani mwandishi wa makala hii akifurahia zoezi la kupanda farasi katika kijiji cha kitalii cha Tashigang.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako