• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • UTALII: JANGWA LINAPOGEUZWA KUWA KIVUTIO CHA UTALII

  (GMT+08:00) 2016-09-02 15:26:31

  Na Elias Mhegera, Beijing

  Miaka 30 iliyopita serikali ya jimbo la Ningxia hapa China iliamua kwamba jangwa lililopo katika eneo hilo liwe kivutio cha "utalii jangwani" au kwa Kiingereza "desert tourism"

  Katika kutimiza azma hiyo watafiti walichunguza ni mmea gani upandwe ili kuliondoa jangwa na badala yake kuwepo uoto wa kijani ndipo ikaonekana kwamba mmea aina ya CALLIGONUM MONGOLICUM unaweza kuota jangwani.

  Na ndipo ikaanza kufanyika kazi ya mkono kwa kutumia vibarua kupanda aina hizo za mmea, katika eneo kubwa ambalo mpaka leo bado upandaji unaendelea hatua kwa hatua.

  Mmea huu una sifa nyingi lakini kubwa zaidi ni uwezo wake wa kustahimili jua kali na hata baridi kali. Zaidi ya hayo mara unapofanikiwa kukua basi maana yake ni kwamba utakapo zaa matunda yake huwa na mbegu ambazo zitajipanda upya na baada ya muda eneo lote la jirani huwa na miti ya aina hiyo.

  Katika jangwa kuna upepo mkali ambao unaweza kuifunika mimea, lakini hali ni tofauti kwa mmea huu ambao hata ukifunikwa na vumbi hilo baada ya muda utaibuka tena.

  Ni katika juhudi za kuondokana kabisa na jangwa katika eneo hilo hatimaye bwawa la maji likachimbwa, mimea mikubwa ikaoteshwa na kwa sasa eneo hilo ni kivutio kikubwa kiasi kwamba watu wasiopungua milioni tatu (3,000,000) ambao asilimia 65 ni Wachina na 35 iliyosalia ikiwa ni wageni, hufanya utalii wa jangwani kila mwaka.

  Unapokuwa njiani kuelekea mahali hapo ukakutana na vumbi kali la jangwani huwezi kuamini kwamba mbele yako kuna uhai, lakini ukiishafika maeneo yenye uhai na kijani kibichi ndipo utafahamu kwamba mwanadamu anaweza kufanya miujiza kwa kutumia mikono yake.

  Itoshe kusema hapa kwamba penye nia pana njia, ukilinganisha jangwa lilivyokuwa kama unavyoona katika picha zangu za awali halafu ukaenda kwenye kijani kibichi inadhihirisha kwamba kama nilivyosema awali, kweli mwanadamu akidhamiria kutenda jambo kubwa anaweza.

  Ndani ya hifadhi hiyo kuna mabanda makubwa 'green-house' ambamo mimea mbali mbali huoteshwa. Kama unavyoona picha moja nikitoka hotelini kupata chakula nikiongozana na wanahabari wenzangu kutoka nchi nyingine za Afrika.

  Faida ya mmea huu wa Calligonum mongolicum ni kwamba unaweza kuishi na mimea mingine kwa pamoja bila madhara yoyote. Inafahamika kwamba baadhi ya mimea ikichanganywa na mimea ya aina nyingine athari kubwa ni kunyonya maji yote ardhini na kusababisha mimea mingine kunyauka na hatimaye kufa kabisa.

  Lakini pia watafiti wamegundua kwamba mmea huu unapotimiza miaka mitano huwa unakuwa na mabadiliko makubwa sana kuanzia kwenye matawi yake hadi utungaji wa maua. Hali hiyo husababishwa na tabia za mmea huo kuendana na mazingira yaliyopo, kwa hiyo japo sifa yake kuu ni kustahimili misuko suko lakini pia kwamba unaweza kubadilika kila wakati kulingana na mazingira husika.

  Tabia nyingine ya mmea huo ni kuhama na una mahusiano mazuri na mimea mingineyo. Kwa mfano majani yake yanaweza kutumika kama mbolea au uoto kwa mimea mingine. Na imethibitika kwamba kila unapohama huzaa tabia mpya tofauti na zile za awali

  Ni jambo jema mmea huu ukapandwa katika maeneo kadhaa ya Tanzania ambayo tayari yameonesha tabia za nusu jangwa kama vile katika mikoa ya Dodoma na Singida.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako