• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Soko la China, fursa iliyo wazi kwa watanzania tunayoichezea

    (GMT+08:00) 2016-11-15 10:05:40

    Mwezi Julai mwaka jana serikali ya Tanzania ilituma ujumbe mkubwa wa kiutendaji hapa Beijing China, uliokusanya watu kutoka wizara, idara, makampuni, jumuiya na taasisi mbalimbali za Tanzania, ukiwa na lengo la kutafuta fursa za biashara kwa ajili ya Tanzania na watanzania. Kwenye mkutano huo wa mawaziri wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), lengo kubwa lilikuwa viongozi wa kisiasa kuangalia maendeleo ya ushirikiano kati ya China na Afrika, na viongozi wengine watendaji walikuwa wakiangalia ni vipi wataweza kupata fursa zenyewe na kuzitumia. Kwenye mkutano huo kuna mambo mawili makubwa niliyoyaona, moja la kufurahisha na lingine la kusikitisha.

    Nilifurahi sana kwa kuwa toka nianze kufuatilia ushiriki wa Tanzania kwenye mikutano ya kimataifa, huu ndio ushiriki nilioushuhudia kwa macho yangu ukiwa ni ushiriki wa maana. Wajumbe waliokuja walionekana wazi kuja wakiwa na malengo halisi, na kupigania kufikia malengo hayo. Nakumbuka jinsi Katibu Mkuu wa wizara ya mambo ya nje Bw John Haule, alivyokuwa akiratibu wajumbe ili kuendana na malengo waliyojia, nakumbuka maofisa vijana kutoka wizara ya mambo ya nje wakiongozwa na Bw Kairuki, na hata maofisa wa ubalozi walivyokuwa wakifanya kazi kubwa kuusaidia ujumbe wa Tanzania. Nikiwa mtanzania niliona fahari kubwa kuona maofisa wa ubalozi, wafanyabiashara, wakulima, wanasiasa wanafanya kazi kwa pamoja kwa lengo moja.

    Lakini jambo moja kubwa lililonisikitisha ni kwamba, kuna baadhi ya mambo ambayo ni ya muhimu sana, lakini wajumbe wengi walikuwa hawayajui. Jambo hilo ni kuwa watendaji kutoka kwenye maeneo ya uzalishaji wa mazao walikuwa hawajui kama mazao yao yanahitajika kwenye soko la China, na yanaweza kuingia kwenye soko la China bila kutozwa ushuru. Kuna orodha kubwa ya bidhaa kutoka Tanzania zinazoweza kuingia kwenye soko la China bila kutozwa ushuru, lakini habari hizo zinawafikisha jumuiya za wakulima na wafanyabiashara? Pamoja na hilo inasikitisha kwa kuwa kila kukicha kuna kilio cha wakulima wa Tanzania kuhusu masoko ya mazao yao. Nakumbuka niliongea na Profesa Haji Semboja aliyeiwakilisha bodi ya korosho, alinieleza kwa masikitiko jinsi mkulima wa korosho wa Tanzania anavyoibiwa na wafanyabiashara wanaonunua korosho moja kwa moja kutoka kwa wachuuzi kwa bei ya chini sana, wakati wangeweza kuuza korosho hiyo kwa bei nzuri sana kwa wanunuzi wa China.

    Sababu kubwa kwanza ni kuwa hakuna mipango na nguvu ya pamoja ya kutumia soko la China. Soko la China ni kama kinywa kikubwa kinachohitaji chakula kingi, ambacho wakulima wadogo wadogo wakiwa mmoja mmoja hawawezi kukidhi mahitaji yake. Bila kuwa na uzalishaji wa maana, kwa maana ya kiasi na ubora, bado tutaendelea kuliangalia soko la China bila kunufaika nalo vya kutosha. Ili kutumia soko la China, kunahitajika kuwe na uzalishaji mkubwa na wa muda mrefu, na si ule wa kulima leo, kuuza kesho na kufurahia mapato kidogo na kuacha uzalishaji na kusahau soko. Wachina huwa hawafanyi biashara kwa mtindo huu, wanapenda mshirika wa biashara mwenye uwezo wa kutoa bidhaa nyingi na kwa muda mrefu. Na kibaya zaidi ni kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao wameona udhaifu huu, na kuamua kununua bidhaa kwa wakulima wadogo wadogo na kuweka hali fulani kama ya "kuhodhi" soko, na kumpunja mchuzi..

    Mwishoni mwa mwezi Agosti China ilitoa waraka kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika, ukiendelea maendeleo changamoto na mustakbali wa uhusiano wa uchumi na kibiashara kati ya China na Afrika. Waraka huo umezungumzia mambo mengi, ikiwa ni pamoja na ongezeko la kasi la biashara kati ya China na Afrika, ongezeko la uwekezaji wa China barani Afrika na maeneo uwekezaji huo unakoelezwa, na hata changamoto zilizopo kwenye ushirikiano huo.

    Kwa watu tunaofuatilia mambo yanayohusu uhusiano kati ya China na Afrika, na China na Tanzania waraka huu si jambo jipya sana kwa sababu yaliyomo ni yale ambayo tayari yamekuwa yakifanyika na yanaendelea kufanyika. Isipokuwa waraka huu ni majumuisho na maelezo ya mambo yaliyofanyika tangu China itoe msukumo mpya kwenye uhusiano kati yake na nchi za Afrika, hasa tangu baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) lilipoanzishwa mwaka 2000. Lakini vilevile waraka huu unaonesha ni jinsi China ilivyojipanga vizuri katika kuendesha uhusiano na ushirikiano kati yake na nchi za Afrika.

    Pamoja na kuwa lengo la uwekezaji na biashara ni kupata faida, kwenye waraka huo pia tunaweza kuona kuwa China haina nia ya kujinufaisha tu, bali pia ina udhati wa kuzisaidia nchi za Afrika, kama zikijipanga vizuri na kama zikiwa na nia ya dhati ya kutaka kujiendeleza. Aya tano za waraka huo (kuhimiza maendeleo endelevu ya biashara, kuboresha uwekezaji na ushirikiano kwenye mambo ya fedha, kuhimiza ushirikiano kwenye shughuli za kilimo na usalama wa chakula, kuunga mkono ujenzi wa miundo mbinu, kuboresha maisha wa watu na kuwajengea uwezo wa kujiendeleza, pamoja na kuhimiza ushirikiano kati ya nchi mbalimbali za Afrika), zote zinaonesha udhati wa China katika kushirikiana na watu wa Afrika katika kuleta maendeleo. Lakini tukijiangalia sisi wenyewe waafrika, au tukijiangalia sisi watanzania tunaweza kuona kuwa bado kuna kitu kinapungua kwenye ushirikiano wetu wa kibiashara na marafiki zetu. Ni kama tunakosa udhati kwenye kufanya biashara, hata pale tunapopewa fursa ya soko kubwa kama la China kwa mashariki nafuu, tunashindwa kuwatangazia wakulima wetu kuwa sasa tunatakiwa kujipanga tulime kwa wingi mteja yuko tayari.

    China inajua kuwa sehemu kubwa ya watu wa nchi nyingi za Afrika, kama ilivyokuwa China katika miaka michache iliyopita, ni wakulima. Kama nguvu kazi nyingi ya watu katika nchi iko kwenye kilimo, basi kuwa makini na kilimo na wakulima, kuna matokeo mazuri kwa watu hao na nchi kwa ujumla. Ni kutokana na kuelewa ukweli huo, na ni kutokana na uzoefu wake, ndio maana China ikaona kuwa, pamoja na kuendelea kuwapatia misaada mingine, ni vizuri kuwasaidia marafiki kwa kuwawezesha katika maeneo mbalimbali, na hata kuwapatia soko la bidhaa na mazao yao.

    Lakini kwa sisi watanzania tukijaribu kujiangalia kwa undani, tunaweza kuona baadhi ya mambo tunayofanya katika ushirikiano kati yetu na China yanatakiwa kuboreshwa. Kwa mfano, unapozungumzia kuhusu kutumia fursa ya soko la China kwa bidhaa za kilimo tunazozalisha Tanzania, utaona kuwa kuna kitu fulani kama kutupiana mpira. Maofisa wa serikali wanasema jukumu la serikali ni kuweka mazingira kwa ajili ya wakulima na wafanyabiashara kuchangamkia fursa hizo, serikali haiwezi kujiingiza huko. Ukiwauliza wakulima na wazalishaji wenyewe wanasema wanahitaji msaada ili waweze kunufaika na soko hilo, kwani wao kama wao bila mkono wa serikali, ni vigumu sana kunufaika na soko la China.

    Ukichambua wanachoongea maofisa wa serikali, utaona ni sawa na kile tunachokisikia wanachoongea wanasiasa wa Marekani, au nadharia za uchumi za uchumi za mwanafalsafa Adam Smith, kuwa serikali hazipaswi kujiingiza kwenye mambo ya uzalishaji na biashara, kwa kuwa haya ni majukumu ya watu si majukumu wa serikali. Lakini tunatakiwa kukumbuka kuwa Marekani na Tanzania zina mazingira tofauti sana, wamarekani wana uwezo mkubwa wa kufanya shughuli za uzalishaji na kwenda kuziuza katika masoko ya sehemu mbalimbali duniani. Tena wao hawapendi serikali iwaingilie, isipokuwa wanataka serikali ifanye kazi ya kuweka mazingira ya kuwawezesha kufanya shughuli zao.

    Lakini Tanzania si Marekani. Tukiangalia ukweli wa mambo kuhusu uwezo wa wakulima wetu na wafanyabiashara kufanya biashara ya kimataifa ni mdogo sana, hauwafikii hata ule wa baadhi ya majirani zetu, bila msaada madhubuti wa serikali, hawawezi kwenda popote, baadhi hata wanashindwa kufanya biashara ndani ya Tanzania. Mfano mmoja nilioushuhudia kwenye maonesho ya biashara hapa China ni kuwa, kuna mnunuzi mmoja alipenda sanaa za kazi za mikono, na alisema zinafaa sana kwa biashara zake, lakini alipopewa oda ya makontena kumi kwa mwaka alisema anaweza kujitahidi kutoa robo kontena kwa mwaka. Huyu ni mfanyabiashara aliyekuja China kutangaza bidhaa zake kwa juhudi zake binafsi, kama angewezeshwa, huenda watanzania wengi zaidi wangenufaika na fursa yake.

    Tukiangalia China inavyojipanga katika kushirikiana na nchi za Afrika na hata Tanzania, unaona kabisa kuwa serikali ya China haijiweki pembeni kuwasaidia wafanyabiashara wanaotaka kuwekeza na kufanya biashara Afrika. Kwa mfano kuna Mfuko wa Maendeleo kati ya China na Afrika CAD Fund, mfuko huu unalenga kuwasaidia wafanyabiashara wa China wanaotaka kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo katika nchi za Afrika, hasa miradi inayozinufaisha pande zote mbili. Mfuko huu unataja wazi ni maeneo gani ambayo yanapewa kipaumbele, na hata namna ya kuwasaidia wachina wanaotaka kufanya biashara katika nchi za Afrika.

    Lakini tukiangalia upande wetu wa Tanzania, ni vigumu kuona mpango uliowazi wa kutumia na kunufaika na soko la China. Serikali bado haina mfuko wowote unaofanana na CAD fund, japo kusaidia wafanyabiashara wa Tanzania kuuza bidhaa zao China, au hata utaratibu unaotaja ni bidhaa gani ambazo inaweza kutoa msukumo na kuhimiza uzalishaji wake, kuwahamasisha na kuwasaidia watu kuzalisha bidhaa hizo ili tutumie soko la China. Serikali inaweka mkazo kwenye sera za jumla (macro policies), lakini kuwa na sera peke yake bila hatua za kuisukuma sera hiyo, hatuwezi kuwa na matokeo yoyote ya maana. Wakulima na wafanyabiashara hawafahamishwi wazi kuhusu fursa zilizopo, na wachache wanaofahamu hawasaidiwi kunufaika na fursa hizo. Matokeo yake ni kuwa fursa ipo, tunaiongelea tu bila kuitumia.

    Kama serikali yetu ingekuwa na sera ya wazi, inayosema tutauza kahawa, korosho au tumbaku kwa wingi, basi ni bora ingewahimiza wakulima wa mazao hayo, kuwapa msaada wa fedha, kiufundi na kiutalaamu na kusimamia kwa nguvu uzalishaji mkubwa wa mazao hayo, na kwenda kutumia soko la China. Ni vigumu sana kwa mzalishaji mmoja mmoja peke yake bila kupata msaada madhubuti kutoka kwa serikali kuweza kutumia fursa hiyo. Vinginevyo tutaendelea kuongea na kufurahia kuhusu kuwepo kwa fursa hiyo, bila kunufaika nayo hata kidogo.

    Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kwenye baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, kuna orodha ya zaidi ya bidhaa 4,700 kutoka kwa nchi za Afrika zenye uhusiano wa kibalozi na China, zinazoweza kuingia kwenye soko la China bila ushuru. Idadi hii ya bidhaa si ndogo, na huenda unahusu mazao yote tunayozalisha katika eneo lote la Tanzania. Kama watanzania (serikali, wakulima na wafanyabiashara) tukijipanga, na kutumia vizuri fursa hii. Kuna uwezekano mkubwa sana wa kupiga hatua katika kuwaendeleza wakulima na wafanyabiashara. Lakini kama mtu mmoja mmoja akiachwa atumie fursa hii, mchakato mgumu na mrefu unaweza kufanya tushindwe kunufaika nayo.

    Kilichopo kwa sasa ni kuwa, kwenye upande wa siasa uhusiano ni mzuri sana, urafiki kati ya China na Tanzania upo kwenye kiwango cha juu sana. Wenzetu wachina wamejipanga vizuri na kunufaika na ushirikiano huo. Kama watanzania tutaendelea kuona fahari ya urafiki tu, bila kutumia fursa ya urafiki mzuri iwe fursa ya biashara, basi tutakuwa tunachezea fursa iliyopo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako