• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Sekta ya Elimu: Tukumbuke elimu ni zaidi ya kufuta ujinga

  (GMT+08:00) 2016-11-15 10:06:30

  Kwa muda mrefu sasa kila maadhimisho ya siku ya elimu yanapokaribia, tumekuwa na desturi ya kujadili maendeleo ya elimu kwa kuangalia kigezo cha watu wanaojua kusoma na kuandika. Tunaangalia takwimu hizo kwa kuwa zamani hasa kipindi baada ya uhuru, hicho kilikuwa moja ya vigezo muhimu vya kuangalia maendeleo ya elimu. Lakini kwenye karne hii tunayoita karne ya sayansi na teknolojia, kuna mengi sana tunayotakiwa kuyatumia kama vigezo vya kupima maendeleo ya elimu. Kuna baadhi ya vigezo tumefanya vizuri, kuna baadhi ya vigezo tunajikongoja na kwenye vigezo vingine bado tuko nyuma sana.

  Kina mama kuweza kusoma kadi za kliniki

  Mwanzoni mwa miaka ya 60 hadi kufikia miaka ya 80 tulikuwa tukiimba kuhusu kufuta ujinga, na hata kuna wakati tulikuwa na madarasa ya kisomo cha manufaa ambayo tulisema lengo lake lilikuwa ni kufuta ujinga. Yaani kuwawezesha watu kujua kusoma na kuandika. Mahitaji ya kufanikisha hilo hayakuwa makubwa, baadhi ya wakati kulikuwa na madarasa kwenye ofisi za CCM, wakati mwingine hata watu walikaa chini ya mwembe na mwalimu aliweza kuwafundisha watu kusoma na kuandika.

  Mwaka 1988 kiwango cha kujua kusoma na kuandika Tanzania kilikuwa 59.1%, mwaka 2002 kilikuwa 69.4% na sasa kimepungua kidogo. Tukiangalia mahitaji na mazingira ya wakati baada ya uhuru, naweza kusema tulifanikiwa kupunguza ujinga, ambapo kina mama wengi anaweza kusoma kadi za kliniki, na watu wengi wanaweza kuandika majina na anuani zao wanapojaza fomu katika ofisi za serikali.

  Zama za elimu ya chini ya mwembe

  Wakati wa maadhimisho ya siku ya elimu ya kimataifa Septemba 8, na siku ya walimu hapa China Septemba 10, nilikuwa najaribu kuangalia jinsi tunavyoangalia changamoto zinazokabili juhudi za watanzania na juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya elimu. Mbali na changamoto ya upungufu wa walimu, nyumba za walimu, kuchelewesha mishahara ya walimu, lingine linalolalamikiwa zaidi ni hali mbaya ya majengo ya shule zetu, hasa shule za msingi inayowafanya baadhi ya walimu kutofurahia kazi yao na wengine kufikia hatua ya kusema hali inawakatisha tamaa kufanya kazi yao.

  Kati ya majengo ya shule ambayo hadi leo ni imara ni yale ya shule zilizojengwa na mkoloni kama vile Malangali, Iyunga, Pugu au Ilboru (shule ambazo zimetoa viongozi wetu wengi), na mengine machache yaliyojengwa baada uhuru na katika miaka ya karibuni, lakini yaliyo mengi hasa ya shule za msingi bado hayaridhishi na hayako katika kiwango ambacho tungependa, au yanaendelea kuonekana kuwa katika mazingira yanayofanana na elimu ya kufuta ujinga.

  Siku hizi tunashuhudia maendeleo makubwa ya ujenzi kwenye majengo mbalimbali mijini. Sielewi ni kwanini bado hali kama hiyo haionekani kwenye shule zetu. Haionekani kama ni kitu kikubwa sana cha kushangaza na kusema kinahitaji teknolojia ya kisasa.

  Katika mazingira ya sasa ya sayansi na teknolojia, hatuwezi kuendelea kuwa na mazingira ya kutoa elimu chini ya mwembe au kwenye shule zinazofanana na mazingira ya elimu ya kufuta ujinga. Shule za sasa zinahitaji kuwa na mazingira yanayomwezesha mwanafunzi kupata elimu ya kuchanganua mambo yanayomhusu na yanayohusu jamii yake, na kuwa tayari kupokea teknolojia itakayomwezesha kujifunza na kupokea teknolojia za kisasa.

  Elimu ya bure ya miaka 15

  Nimebahatika kutembelea baadhi ya shule za China katika miji mbalimbali. Mbali na majengo ya shule kuwa nadhifu na kulindwa vizuri, moja kati ya mambo ambayo yamenishangaza ni kuwa katika kila darasa lina umeme, projekta, kompyuta na huduma ya internet. Mambo hayo mbali na kuwarahishia walimu kazi ya kufundisha, pia yanawawezesha wanafunzi kujua mambo mengi zaidi. Labda ni vigumu kwa nchi yetu kufikia hatua kama hiyo haraka, kwa kuwa kufikia hatua kama hiyo kuna gharama zake, lakini tunaweza kuanza japo mijini.

  Kwenye kampeni zinazoendelea za uchaguzi wa rais wagombea wamekuwa wanazungumzia kuboresha elimu ya msingi na kufikia hatua ya kusema kuwa elimu ya msingi itatolewa bure. Hapa China serikali inagharamia ujenzi wa majengo ya shule, kuwalipa walimu, gharama mbalimbali za kuendesha shule na hata kuwapatia wanafunzi vitabu vya kiada na walimu vitabu vya kufundishia. Mzazi anachotakiwa kuchangia ni kulipia gharama za chakula cha mchana ambazo si kubwa, na kumnunulia mtoto madaftari ambayo bei yake ni ndogo kiasi kwamba hata mtu mwenye kipato cha chini kabisa anaweza kumudu. Kutokana na uzoefu ilionao China kwenye mambo haya, si jambo baya kama tungeelekeza nguvu zetu za ushirikiano kwenye sekta ya elimu ili kutoa msukumo zaidi kwa maendeleo ya elimu.

  Wakati China ilipoadhimisha siku ya walimu, nilisoma habari moja inayosema wilaya moja iliyo nyuma kabisa kimaendeleo iliyoko kusini magharibi mwa China ilitangaza itaanza kuanzia mwaka kesho kutoa elimu ya miaka 15 bila malipo, wakati sehemu nyingine nchini China hata zilizo mbele kimaendeleo zinatekeleza miaka 9 ya elimu ya bure……..

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako