• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Mafanikio na Changamoto mpya za Sera ya Mtoto mmoja wa China

  (GMT+08:00) 2016-11-15 10:07:26

  KWA muda wa zaidi ya miaka 35 sasa nchi ya China imekuwa inafuata Sera ya Mtoto mmoja, sera ambayo lengo lake kubwa ni kudhibiti ongezeko kubwa la idadi ya watu, ambalo China iliona kuwa ni changamoto kwa familia na kwa serikali. Mwanzoni wakati sera hii inaanza kutekelezwa kulikuwa na maswali kama kweli itakuwa na ufanisi na kama kweli inaendana na utamaduni wa wachina.

  Chimbuko la Sera ya Mtoto mmoja

  Katika miaka mingi iliyopita Wachina waliishi katika familia kubwa. Kwa mfano wakazi wa Beijing walikuwa wakiishi katika nyumba zenye (Ua) zinazoitwa Hutong, ambazo ndani walikuwa wakiishi Bibi na Babu, Baba na Mama na Watoto. Familia iliyokuwa na mwonekano kama huo ilionekana kuwa ni familia yenye furaha na iliyokamilika. Kwa hiyo kubadilisha muundo kama huo ambao ulikuwa umezoeleka kwa muda mrefu halikuwa jambo rahisi.

  Aidha, baada ya China kuwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu lililoleta shinikizo kwenye raslimali za nchi, iliamua kutafuta njia ya kudhibiti ongezeko la watu. Mtazamo ukapelekwa kwenye ubora wa idadi ya watu na sio ukubwa wa idadi ya watu. Tukiangalia kwa haraka yote mawili yamefanikiwa hadi kufikia leo.

  Mkuu wa Kitivo cha Sayansi Jamii na Idadi ya Watu cha Chuo Kikuu Cha Renmin cha China, Zhai Zhengwu, amesema kuwa tangu sera hiyo ilipotolewa mwaka 1978 na kuanza kutekelezwa mwaka 1980 ilianze kufanya kazi hadi kufikia mwaka 2011 ambapo ilifanikiwa kuepusha watoto milioni 400 kuzaliwa. Muhimu zaidi ni kuwa lengo kuu la sera hiyo yaani kupunguza umaskini na taabu zinazotokana na idadi kubwa ya watu limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

  Kwenye miji mingi ya China na hasa katika sehemu ya Mashariki mwa China, kiwango cha maisha ya watu kimeinuka karibu katika pande zote. Chakula, Elimu, Afya, Makazi, Usafiri na huduma nyingi za jamii zimewafikia watu wengi.

  Mmoja wa waanzilishi wa sera hiyo, Ma Yinchu, ambaye alipata shahada ya pili ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Yale kilichopo nchini hapa, na Shahada ya Udaktari ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Columbia, ongezeko kubwa la idadi ya watu liliwabidi watu watumie zaidi mapato yao katika matumizi badala ya kupanua uzalishaji, hali ambayo ilikuwa ni kikwazo kwa maendeleo ya nchi. Tafiti zinaonyesha kuwa ongezeko kubwa la idadi ya watu lisipoendana na ongezeko la uzalishaji wa chakula, linakuwa changamoto kubwa kwa uchumi wa nchi.

  Kwa nchi yetu Tanzania pamoja na kuwa tulikuwa na kampeni kubwa ya uzazi wa mpango, kwa sasa inaonekana kuwa kila mtu anaamua kuzaa kutokana na uwezo wake na imani zake. Uzuri ni kwamba bado hatujafikia hali ya kuwa na ongezeko kubwa la watu kuliko uwezo wa uzalishaji wa chakula. Katika mazingira ya sasa ya mabadiliko ya hali ya hewa na kupungua kwa uzalishaji wa chakula unaotegemea hali ya hewa kuna uwezekano baadaye tukakumbana na matatizo mkubwa.

  Changamoto inayolikabili Taifa la watu wa China

  Hata hivyo unapotatua tatizo moja, inawezekana bila kujua kuwa unatengeneza changamoto nyingine. Kwa sasa China inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazotokana na mabadiliko yaliyoletwa na sera ya mtoto moja kwenye jamii. Changamoto ya kwanza ni ile inayoitwa 4-2-1, yaani mtoto mmoja ambaye ni mtoto pekee katika familia, imefika wakati anatakiwa kuwatunza wazazi wake na bibi na babu wa pande mbili. Hii ni kazi ngumu ambayo wakati sera hii inaanza kutekelezwa halikufikiriwa sana.

  Changamoto nyingine ni ile inayotokana na mawazo ya jadi ya wachina kupenda watoto wa kiume. Wachina ni watu wanaojali kuendeleza ukoo na kuona kuwa mtoto wa kiume ndio anaweza kutekeleza jukumu hilo. Hivyo pamoja na kufikiria hali ya matunzo ya uzeeni, inawafanya baadhi ya watu kuendeleza maoni ya jadi na kuona ni bora kupata mtoto wa kiume.

  Matokeo yake ni kuwa China imejikuta katika hali ya kukosa uwiano kati ya watoto wa kiume na watoto wa kike. Takwimu zilizotolewa mwaka 2013 hapa China zinaonesha kuwa idadi ya watoto wa kiume inaonekana kuwa kubwa kwa wastani wa wavulana 117 kwa wasichana 100.

  Vilevile kutokana na kuzaliwa kwa idadi ndogo ya watoto ikilinganishwa na idadi ya jumla ya watu nchini China, kwa sasa idadi ya wazee hapa China imeongezeka, sababu kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa sio kubwa. Na kuongezeka kwa idadi ya wazee maana yake ni kuwa gharama za kuwatunza wazee hao zinaongezeka na hata uwingi wa nguvu kazi katika jamii pia unaopungua. Hizi ni baadhi tu ya changamoto ambazo China inakabiliana nazo kutokana Sera ya Uzazi wa Mpango.

  Mafunzo kwa Tanzania

  Mara nyingi sera zinapotolewa huwa zinalingana na mazingira na wakati, lakini kama mazingira na wakati vikibadilika, sera hizo zisipofanyiwa marekebisho basi zitakuwa zimepitwa na wakati au zitakuwa tatizo kwa wakazi wa eneo husika.

  Hivyo basi sisi kama Tanzania tunaweza kujifunza kutoka kwa wenzetu Wachina katika sera yao ya Uzazi wa Mpango. Takwimu zilizotolewa nchini hapa (China) zinaonesha kuwa mwaka 2012 idadi ya watu wenye umri wa kufanya kazi nchini hapa ilianza kupungua kwa mara ya kwanza.

  Kwa wakati mmoja, idadi ya wazee nchini China inaongezeka kwa kasi zaidi kuliko ile ya wastani wa dunia na inakadiriwa kuwa itakapofika mwaka 2020, kati ya kila wazee wanne duniani, mmoja anatoka China. Kupungua kwa nguvu kazi na kuongezeka kwa wazee kumeilazimisha serikali ya China kuboresha sera yake, sio tu ya mzazi wa mpango bali pia hata sera nyingine kama vile kuchelewesha muda wa kustaafu.

  Kwa hiyo sisi kama Watanzania tunapoandaa sera tusiangalie leo tu, hata kama tukiangalie leo tunapoona tatizo kwa sera zilizopo tunatakiwa kuwa makini kizirekebisha haraka iwezekanavyo.

  Ukubwa wa familia kwa sisi Watanzania bado ni sababu inayochangia ugumu wa maisha kwa familia nyingi. Lakini tukizungumzia suala la kudhibiti ongezeko la idadi ya watu kwa mujibu wa sheria kama ilivyo hapa China, litakuwa ni jambo gumu litakalokabiliwa na upinzani mkubwa. Hii haiondoi ukweli kuwa ukubwa wa familia tunazoshindwa kuzimudu ni tatizo. Pamoja na kuwa China ni nchi kubwa na Tanzania ni nchi ndogo, kuna mambo ambayo yanafanana sana kwenye jamii zetu. Wachina kwa ujumla ni watu wa familia na wanapenda familia kubwa japokuwa changamoto za kiuchumi na kijamii zilifanya waangalie namna ya kupunguza ukubwa wa familia ili kuhakikisha kuwa changamoto za kiuchumi haziwi sababu ya kupoteza furaha ya familia.

  Sisi watanzania kwa jadi yetu ni watu wa familia pia. Si ajabu kukuta familia ina watoto watano au hata zaidi, japo si wengi wanaokubaliana na ukweli kuwa ukubwa wa familia ni chanzo cha changamoto za kiuchumi kwa familia nyingi za watanzania, ukweli ni kwamba ukubwa wa familia sio tu ni mzigo kwa wenye familia, bali pia ni mzigo kwa jamii na hata kwa serikali kwa ujumla. Pamoja na kuwa kwa sasa China inakabiliwa na changamoto za sera za kudhibiti idadi.

  Mwitikio wa wananchi wa China kuhusu Sera ya kuwa na Watoto wawili

  Kumbukumbu zinaonyesaha kuwa, Ni mwaka mmoja sasa tangu Sera ya kuwaruhusu wanandoa nchini China kuwa na mtoto wa pili kama mmoja kati yao ni mtoto wa pekee katika familia ianze kutekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini China. Lakini hali halisi ni kuwa, ombi la kuzaa mtoto wa pili halikuongezeka kwa kiasi kikubwa kama wachina walivyotarajia.

  Tangu sera ya kuwa na watoto wawili ipitishwe, kwa hapa Beijing, zaidi ya wanandoa elfu 30 wamejiandikisha kwa ajili ya kupata mtoto wa pili. Na maombi ya watu 28,778 yamekubaliwa, idadi ambayo ni ndogo kuliko iliyokadiriwa awali ambayo ilikuwa ni elfu 50. Wanandoa wengi ambao wanaweza kuwa na mtoto wa pili wameamua kutofanya hivyo mwaka huu, lakini hii haimaanishi kuwa hawataki, bali labda hawakao tayari kwa mtoto wa pili.

  Mnamo mwaka 2013 Bunge la China lilipitisha maazimio ya kurahisisha sera ya mtoto mmoja kwa mujibu wa Televisheni ya taifa hilo.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako