• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China imejikomboa hatua kwa hatua katika kunyanyua uchumi na kupambana na umaskini ni vyema wengine wajifunze kutokana na uzoefu huo (Sehemu ya kwanza)

    (GMT+08:00) 2016-12-16 16:37:37

    Nchi za Afrika na kwingineko duniani zinatakiwa kuiga mfano wa China katika kupambana na umaskini. Mwandishi wa makala hii ambaye amekuwa nchini China kwa miezi tisa anayo mengi ya kusimulia.

    Miongoni mwa jitihada kubwa zilizofanywa na China ili kuinua uchumi wake ilikuwa ni kujielekeza vijijini ambako ndiko kulikuwa na umaskini mkubwa zaidi.

    Prof. Sangui Wang mchumi wa kilimo na maendeleo ya vijijini anasema kwamba kwa muda wa zaidi ya miaka 40 ni kama vile taifa hili lilikuwa linapigana na adui huyo mmoja yaani umaskini vijijini.

    "Kupambana na umaskini vijijini ilikuwa ni sawa na vita kwa sababu watu hao pia walikuwa wanakabiliwa na tatizo la ujinga ilituwia vigumu tuanze na nini elimu au kuondoa umaskini?" anasema msomi huyo alipokutana na wanahabari kutoka Afrika.

    Ili kufanikisha azma hiyo, ilibidi wapatikane watu wa kujitolea wenye uvumilivu wa hali ya juu. Anasema mpango huo wa kujitolea vijijini ulianza mwaka 1983, ambapo wananchi pia walitakiwa kukubali kuhamishiwa katika maeneo ambayo serikali ingeweza kuwasaidia kwa unafuu zaidi.

    Zilikuwepo changamoto nyingi katika mpango huo kwa sababu baadhi ya wananchi walihama kwa sababu ya kuamini kwamba watapewa motisha katika makazi mapya badala ya kujitegemea wao wenyewe. Baadhi yao walirejea katika makazi yao ya awali walipogundua kwamba ndoto zao hazijatimizwa katika uhamaji huo.

    "Lilikuwa jambo la kuvunja moyo sana pale serikali ilipokuwa ikifanya kila jitihada ili kuwaondoa watu wake katika umaskini lakini baadhi ya walengwa wa mpango huo hawakuona umuhimu wa jambo hilo na badala yake walitaka majibu ya haraka haraka," anasimulia Prof. Sangui.

    Hata hivyo msomi huyo anafurahi kwamba sehemu kubwa ya wananchi nchini China wameondokana na umaskini, na ni theluthi moja tu ya idadi ya watu bilioni 1.36 ambao wanahitaji msaada kutoka serikalini ili kujikimu katika mahitaji yao, sehemu kubwa ya wananchi wapo katika hali njema.

    Anasema kwamba mafanikio hayo yametokana na kuwapo kwa mikakati maalumu kwa tabaka la wenye kipato cha chini kuanzia kuwapatia mikopo yenye riba nafuu, kutengeneza ajira katika maeneo yao, na ufuatiliaji wa karibu.

    Baada ya mwandishi wa makala hii kutembelea majimbo zaidi ya 10 anaweza kulithibitisha jambo hilo, kuwa hali ya sasa ya maendeleo ya China kwa ujumla ni nzuri. Pia inawezekana hali ya kukumbuka maeneo ya vijijini ikawa bora zaidi katika utawala uliopo sasa madarakani.

    Rais Xi Jinping wa China, akiwa na umri wa miaka 15, alikwenda katika kijiji cha Liangjiahe na kuweka makazi yake hapo kwa miaka sita. Mpango huo ulilenga kuondoa tabia ya 'umangi meza' na kupenda kazi za 'kola nyeupe' kwa wasomi.

    Ilikuwa mwaka 1969, ambapo mamia ya vijana wa Kichina walianza kupelekwa vijijini, na idadi ya vijana waliofanya kazi kwa mtindo huo kwa ujumla ni 1,427.

    Akiwa kijijini hapo kijana Xi Jinping alifanya kazi sawa na wanakijiji wenzake na hatimaye akajiunga na tawi la vijana wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) mwaka 1971 akiwa kijijini hapo.

    Alifanikiwa kuwa kiongozi wa chama kijijini hapo na mwaka 1974 akawa mwanachama kamili wa CPC. Uzoefu huo ni muhimu kwa kiongozi huyo kwa sasa kwa sababu anayajua mazingira halisi ya vijijini.

    Hatimaye kiongozi huyo alijiunga na Chuo Kikuu cha Tsinghua mwaka huo huo wa 1974 kwa ajili ya masomo ya uhandisi kemikali lakini hata hivyo hakuachana na ukada wake katika chama hali iliyomfanya aendelee kupanda madaraja taratibu na hatimaye kuwa rais wa nchi.

    Kwa sasa imekuwa ni kawaida kusikia katika vyombo vya habari sehemu mbali mbali duniani juu ya kile kinachoitwa 'muujiza wa China'. Maana halisi ikiwa ni jinsi taifa hilo lilivyoweza kuondokana na umaskini kwa kasi.

    Ili kufahamu nini kimesababisha maendeleo hayo ya kasi inahitajika kufanya tafiti za kina. Mwandishi wa makala hii ameshuhudia wataalamu mbali mbali nchini humu wakikiri kwamba pamoja na kuwapo na mkakati wa ubunifu ndani ya nchi lakini pia mawazo ya wataalamu kutoka nje ya nchi yamesaidia sana ili kuinyanyua China ya leo.

    Mwandishi wa makala hii amekutana na wataalamu wengi wakizungumzia huo muujiza wa jinsi taifa hili lilivyojikwamua kutoka katika umaskini na kufikia hapa lilipo kwa sasa likiwa linayatikisha mataifa makubwa duniani hususani Marekani na washirika wake.

    Miongoni mwa mikakati iliyotumika ni pamoja na kuanzisha asasi za kiraia (NGO) za kupambana na umaskini vijijini. Maelezo ya kina ya mkakati huo yanatolewa na Bw. Bw. Wang Xingzui, Makamu Rais Mfuko wa Kupambana na Umaskini China.

    Kimsingi kinadharia wataalamu hao wawili waliotajwa hapo juu ndiyo hasa chimbuko la uelewa kwa mwandishi wa makala hii wa jitihada zilizofanyika ili kuondoa umaskini

    Tukirejea katika mada yenyewe tunaona kwamba sehemu kubwa ya huo muujiza unamtaja Deng Xiaoping kiongozi mkuu wa China kuanzia mwaka 1978 hadi 1989 kama haswa ndiye muasisi wa hicho kinachoitwa 'muujiza wa China', na mwandishi wa makala hii hana pingamizi na mtazamo huo.

    Lakini kwa upande mwingine huwezi kuzungumzia muujiza wa China bila kuzungumzia kwanza umoja wa kitaifa ambao ndiyo ilikuwa ndoto kubwa ya muasisi wa taifa jipya la China Bw. Mao Zedong. Muasisi huyo wa mapinduzi ya mwaka 1949 alidhamiria kujenga taifa lenye nguvu kubwa kisiasa na kiuchumi.

    Kwa bahati mbaya alikosa mbinu sahihi za kufikia lengo hilo ambalo mwenzake Deng alifakiwa katika kipengele hicho cha uchumi. Katika muhtasari wake ni vyema kuyataja mambo yaliyosaidia katika huo unaoitwa muujiza wa China.

    Kwanza ni ubunifu, dhana hii ilijengewa mazingira mazuri na hata wanafunzi wa vyuo vikuu na wataalamu viwandani wakapewa motisha kubwa pale walipoonesha kuja na dhana mpya walizozibuni wao wenyewe au hata kuzipata kwa njia ya tafiti mbali mbali.

    Pili ilikuwa ni kukubali mawazo mapya; katika hili Wachina wanastahili kupongezwa sana kwa sababu waliamini kwamba kuwa na itikadi tofauti na taifa la Marekani haimaniishi kwamba wapinge kila kitu alicho nacho Mmarekani.

    Kwa mantiki hiyo, serikali ya China iliyakaribisha makampuni mengi kutoka nje na hata ya Marekani kwa masharti kwamba baada ya miaka 15 teknolojia iwe imehamia mikononi mwa Wachina wenyewe.

    Pia kulikuwa na mpango mahsusi wa kuhakikisha kwamba sekta ya umma na sekta binafsi vinakua kwa pamoja. Kwa maana hiyo watumishi wa umma walioamua kuondoka ili wakafanye biashara waliruhusiwa na wakalipwa viinua mgongo vyao mara moja.

    Hata hivyo, serikali ilihakikisha kwamba kipaumbele kinabakia kwa sekta ya umma kwanza. Kwa mfano katika masoko ni lazima bidhaa zinazotokana na makampuni ya umma zipewe unafuu na upendeleo kuliko makampuni binafsi.

    Ukifanya uchunguzi mdogo utaona kwamba nchi nyingi za Kiafrika hapo ndipo zilipoanguka kwa sababu hata Tanzania kuna dhana ilijengwa kwamba makampuni ya umma yalikuwa yanaleta hasara na hivyo mengi yakauzwa au kukaribisha wawekezaji binafsi.

    (MWISHO WA SEHEMU YA KWANZA)

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako