• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • China imejikomboa hatua kwa hatua katika kunyanyua uchumi na kupambana na umaskini ni vyema wengine wajifunze kutokana na uzoefu huo [Sehemu ya pili]

  (GMT+08:00) 2016-12-16 16:38:31

  Kuna mazingira yalijengwa ili kupata uhalali wa uamuzi huo kwamba ujamaa umeshindwa kwa hiyo inabidi kujaribu njia nyingine ya kuleta maendeleo.

  Kwa kiwango kikubwa mpaka sasa bado mataifa ya Afrika hayajajikomboa kutokana na dhana hiyo. Kinyume chake taifa la China limeendelea kuweka kipaumbele katika sekta ya umma na limefanikiwa sana kwa njia hiyo.

  Mafanikio hayo yametokana na nidhamu ya kazi uadilifu na kutooneana haya pale mmoja au kikundi cha watu wanapodhihirika kufuja mali za umma.

  Kingine kikubwa kilichofanyika ni kuimarisha miundombinu. Katika hili wataalamu wote wa miundombinu duniani wanakubaliana kwamba China ndiyo inayoongoza kwa kuwa na miundo mbinu bora ya usafirishaji duniani.

  Lakini miundo mbinu inayoongelewa hapa ni katika maana au dhana pana na wala siyo barabara na reli peke yake kama ilivyozoeleka kwa wengi. Kinyume au nyongeza yake ni kwamba miundo mbinu inatakiwa iendane na masuala ya ugavi wa nishati, mawasiliano ya simu na majengo. Pamoja na mfumo mzima wa ujenzi unaombatana na uhamaji wa watu kutoka eneo moja hadi jingine. Kwa maana hiyo ujenzi wa miundombinu umekuwa pia ukidhamiria kuzuia uhamaji holela wa watu.

  Katika kudhibiti hilo tafiti zilifanyika na kuangalia ni wapi watu wamelalia zaidi katika taifa hilo na ni kwa nini hali hiyo inajitokeza? Ili kubadili hali hiyo, serikali ya China ilijenga taasisi nyingi zaidi za kielimu kama vile vyuo vikuu na hospitali za rufani na hata taasisi za kibenki katika maeneo ambayo watu waliyakimbia.

  Serikali ya China ilipowakaribisha wawekezaji wakaelekezwa huko huko ambako wananchi walipakimbia, na miongoni mwa vivutio walivyopewa wawekezaji ilikuwa ni kupewa ardhi kubwa bure. Kwa mtindo huo huo hata wawekezaji wazawa nao wakapewa maeneo hayo bure ili kuhamishia huko idadi kubwa ya watu.

  Serikali ilifanya usajiri na kuwatambua watu wenye vipato vya chini zaidi katika mfumo wa usajili unaoitwa 'Hukou'. Wakati mwingine katika lugha isiyo rasmi mfumo huo huitwa 'Huji'.

  Kimsingi mfumo huu huamua kwamba mtu atapewa huduma stahiki za umma bure kama vile matibabu kulingana na mahali aliposajiliwa. Vivyo hivyo mtu anaweza kuhama kutoka kijijini kwenda mjini kwa kudhihirisha kwamba ana mtaji wa kutosha.

  Serikali ya China iliunda sera maalumu kwa ajili ya kupambana na umaskini kulingana na mahitaji ya eneo moja hadi jingine.

  Kwa mfano watu ambao walionekana kuwa ni mafukara zaidi walipewa misaada ya aina yao tofauti na wale wenye unafuu wa kipato.

  Katika kulinyanyua tabaka hilo kuna jitihada za aina tatu zinafanyika, kwanza ni kuwapatia misaada ya bure, pili ni kuwapatia mikopo yenye riba nafuu na tatu ni kuweka muongozo wa matumizi ya pesa inayotolewa katika kulisaidia kundi hilo.

  Katika kufanikisha zoezi hilo jumla ya ofisi 138 zimefunguliwa nchini pote. Kazi za ofisi hizo ni kuwasimamia wahusika katika makundi yao lakini pia kuangalia ufanisi wa miradi inayotolewa na serikali kwa ajili ya makundi hayo.

  Lakini pia ofisi hizo husaidia kutia hamasa serikali za majimbo jirani kuwasaidia wale wenye mahitaji makubwa, kuzisaidia asasi za kiraia za kuondoa umaskini, na pia kuwakaribisha wadau wengine na wasamaria wema.

  Katika kufanikisha azma hiyo Mfuko wa Kupambana na Umaskini China umekuwa ukishirikiana na wadau wafuatao: kwanza ni makundi ya kijamii, watu binafsi wenye miradi mikubwa, asasi za kiraia na mifuko mingine ya kuondoa umaskini.

  Lengo ni kuhakikisha kwamba kila mradi ulioanzishwa unarudisha faida kwa walengwa. Mfuko wa kuondoa umaskini ulianzishwa mwaka 1989, mpaka sasa umekwisha wasaidia raia milioni 25 wa China na kuzalisha faida ya kiwango cha dola bilioni 2.8.

  Mfuko huo unaoajiri watu zaidi ya elfu tatu, wengi wao ni wataalamu wa uendeshaji wa masuala ya fedha kwa wenye mitaji midogo na pia wataalamu wa asasi za kiraia za kupamabana na umaskini.

  Miongoni mwa miradi iliyofanikishwa na mfuko huu ni pamoja na kutoa mabegi na madaftari na vifaa vingine vya shuleni kwa watoto watokao katika familia maskini. Pia kujenga mabweni kwenye maeneo yenye umaskini mkubwa.

  Mfuko huo pia umewalipia ada wanafunzi wa masomo ya juu ya sekondari na vyuo vikuu. Msaada huo hufanyiwa kwanza utafiti kabla ya kutolewa katika eneo husika.

  Kwa mfano yapo maeneo ambayo mahitaji yake makubwa zaidi ni afya kwa wanafunzi, wengine ni chakula, kwa wengine ni masuala ya dharura na kwa wengineo ni makazi.

  Baada ya tafiti hizo, serikali ikiona hitaji kubwa la kwanza ni daraja basi itaanza na mradi huo na kisha itajenga vyanzo vya mapato kama vile mahoteli, maduka n.k. Pamoja na hayo serikali imekuwa ikiviunganisha vijiji hivyo na mashirika mengine ya kimataifa yanayopambana na umaskini.

  Licha ya jitihada hizo, serikali imekuwa ikitoa mafunzo mengine kama vile ya ujasiriamali huko vijijini. Pia imekuwa ikikaribisha vijana na watu wengine katika makundi tofauti kwenda vijijini kwa lengo la kusaidia kuondoa umaskini.

  Uchangiaji wa pesa umekuwa ukitoka katika vyanzo mbali mbali kama vile michango ya mashirika na makampuni, michango ya watu binafsi, michango ya mashirika ya kujitolea, michango kwa maendeleo ya jamii kutoka taasisi mbalimbali.

  Serikali imetoa unafuu wa kodi kwa wale wanaochangia jitihada zake za kupambana na umaskini. Baadhi ya michango huja katika muundo wa utaalamu, fedha, na kulipia gharama za matangazo katika vyombo vya habari.

  Serikali imekuwa ikitoa mafunzo kwa vijana katika maeneo mbalimbali ili wajiandae kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya vijijini lakini pia imekuwa ikitoa mafunzo ya ujasiriamali huko huko vijijini kwa vijana waliokosa nafasi za kujiunga na vyuo vikuu.

  Hata hivyo mfuko wa kupambana na umaskini umekuwa ukichukua tahadhari kubwa katika kupokea na kutumia misaada mikubwa inayopokelewa. Kulingana na Bw. Wang ambaye ni mtaalamu wa uendeshaji wa taasisi za aina hiyo, mara nyingi asasi za kiraia zikipokea pesa nyingi husambaratika mara fedha hizo zitakapoisha.

  Anashauri kwamba njia nzuri ya kuendesha miradi ya aina hiyo kwanza ni kuhakikisha kwamba ni endelevu, pili mtiririko wa pesa unatakiwa usitikisike wala kuyumbishwa, na pia kuwe na michango ya wanachama ili waione hiyo taasisi kwamba ni mali yao.

  (Mwisho wa sehemu ya pili)

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako