• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • China imejikomboa hatua kwa hatua katika kunyanyua uchumi na kupambana na umaskini ni vyema wengine wajifunze kutokana na uzoefu huo (SEHEMU YA TATU)

  (GMT+08:00) 2016-12-16 16:39:10

  Kulingana na uzoefu wa China, watu wanaoutumikia mfuko wa kupambana na umaskini wamegawanyika katika makundi matatu; kwanza ni wale wenye ajira za kudumu, pili ni wale wa muda na tatu ni washauri ambao hawajaajiriwa lakini hulipwa kutokana na kazi zao za kitaalamu kila wanapozitoa kwa taasisi hiyo.

  Lakini pia taasisi hiyo kukaribisha wataalamu mbali mbali ambao hushirikiana nayo katika kutoka mafunzo ya nyumba kwa nyumba. Lengo mahususi ni kuhakikisha kwamba kila mwanaushirika anachangia kwa njia mbalimbali kuanzia fedha hadi muda.

  Katika ziara za kuitembelea China, mwandishi wa makala hii ameshuhudia baadhi ya vijiji vilivyohamishwa ili kutoa nafasi kwa kilimo cha kibiashara na kisha wakulima wamejengewa nyumba za kisasa za makazi na kupata huduma zote muhimu ikiwa ni pamoja na kulipwa fidia kutokana na kuhamishwa.

  Katika maeneo ya mijini, akina mama wamekuwa wakipewa pikipiki za gurudumu matatu aina ya bajaj vivyo hivyo watu wenye ulemavu. Lakini pia wamekuwa wakijengewa migahawa ya kisasa majumbani mwao kwa ajili ya wateja waliopo jirani.

  Kwa vijijini, mkakati mwingine umekuwa ni kuwapatia mifugo kama ng'ombe wa maziwa, nguruwe, kuku na hata mbuzi ili wafuge kwa malengo ya biashara. Kwa upande mwingine mfuko huo umekuwa ukifadhili utengenezaji wa kazi za sanaa kama vile kupaka rangi katika mapambo na kufuma vitambaa.

  Hata hivyo ni vyema kuzitambua jitihada za Serikali ya China katika kuwasaidia raia wake. Mfano halisi ni namna ilivyowahudumia waathirika wa tetemeko la ardhi katika jimbo la Sichuan lililotokea mwaka 2008 na kusababisha vifo vya watu kati ya elfu 88,000 hadi 90,000 na wengine 15,000 kujeruhiwa vibaya.

  Kwa hakika Serikali ya China imefanikiwa kuondoa maumivu ya madhara ya tetemeko na kuwa kivutio cha utalii katika eneo ambalo liliathirika na tetemeko hilo.

  Kwa sasa kati ya mwezi Machi hadi Disemba wakati mwingine eneo hilo hutembelewa na watu wapatao elfu ishirini kwa siku (20,000) kwa ajii ya utalii. Watu hao ni kutoka ndani ya China, Japan, Korea na nchi nyinginezo duniani.

  Katika mkakati huo wa kulisaidia jimbo la Sichuan, kwanza kila jimbo katika Jamhuri ya Watu wa China (PRC) lilipewa kipande cha kazi cha kutengeneza maeneo yaliyoharibiwa na tetemeko kama vile ujenzi wa hospitali shule na nyumba za makazi.

  Baada ya hapo ziliundwa asasi za kiraia zipatazo 150 ili kutafuta namna ya kuwasaidia wahanga wa tukio hilo. Kwa sasa waathirika wote wamejengewa nyumba na wanapata ruzuku kila mwezi.

  Kulingana na maelezo ambayo mwandishi wa makala hii aliyapata kutoka kwa wafanya biashara wenyeji wa eneo hilo, watu waliokuwa wanapata kipato cha kiasi cha Yuan elfu mbili kwa mwezi (2,000) sawa na Dola $ 400, leo wanapata hadi Yuan elfu kumi kwa mwezi (10,000) sawa na Dola 1700.

  Hatua zaidi zilizochukuliwa na serikali ya China kuwasaidia wananchi wa eneo hilo, kwanza ni kujenga jumba la makumbusho ya tetemeko hilo ambalo leo hutembelewa na watu wasiopungua elfu mbili kwa siku (2,000).

  Pili ni kuwahimiza wananchi wa majimbo mengine kutembelea eneo hilo ili kuongeza kipato cha wenyeji na kujionea mambo yalivyokuwa.

  Majengo mengi ya zamani ya kifalme ambayo yalikuwa ni ya mbao na yalikuwa yamesahaulika leo yamefufuliwa kwa ajili ya kuvutia biashara ya utalii. Kutokana na mkakati huo kuna bidhaa nyingi zinazozalishwa na wenyeji na kuuzwa kwa watalii wa ndani na wa nje.

  Katika jumba la makumbusho, kuna picha mbali mbali za wahanga wa tetemeko hilo, video na jinsi Serikali ya China ilivyojitahidi kuwasaidia wahanga wa tukio hilo. Ikiwamo yaliyoandikwa magazeti na kauli za viongozi walipotembelea eneo hilo zimewekwa kwenye video.

  Mwandishi wa makala hii alipata nafasi ya kulitembelea jimbo la Shandong ambalo ni la tatu kwa nguvu ya uchumi nchini China.

  Katika Sensa ya Taifa ya Mwaka 2015 jimbo hilo lilipatikana na wakazi milioni 98.47, ikiwa ni asilimia saba ya idadi nzima ya taifa la China. Jimbo hili limekuwa likichukua nafasi ya tatu katika nguvu ya uchumi kwa muda wa miaka 17 mfululizo sasa.

  Miongoni mwa mambo muhimu ya kiuchumi aliyoyashuhudia mwandishi wa makala hii ni kwamba jimbo hilo ndilo linaongoza kwa uzalishaji wa umeme nchini pote.

  Pia llinaongoza katika tafiti za kina kirefu cha bahari na masuala ya teknolojia kwa ujumla. Jimbo hili limebarikiwa kwa hazina kubwa za kiuchumi pamoja na kwamba ndipo mahali alipozaliwa, kuishi kufariki, na kuzikwa mwanafalsafa maarufu wa China, Confucius.

  Jimbo hili lina ushirikiano mkubwa na nchi za Kiafrika kutokana na biashara. Makampuni kutoka jimbo hili yamekuwa yakisafirisha makontena kwenda katika Bara la Afrika na baadhi ya nchi zinazofikiwa na bidhaa hizo ni pamoja na Liberia, Tanzania, Ethiopia na Kenya.

  Kampuni ya Hisense ambayo makao makuu yake ni katika jimbo hili imefungua tawi lake kubwa nchini Afrika Kusini. Uwekezaji huo mkubwa umezalisha ajira, na pia licha ya kulipa kodi kwa serikali ya nchi hiyo, kampuni hiyo pia imekuwa ikitoa misaada mbali mbali kwa jamii.

  Kwa mujibu wa Mkurugezi wa Biashara Jimbo la Shandong Bw. Qiu Tiabin ushirikiano kati ya jimbo lake na nchi za Kiafrika unaenda vizuri japo kuna changamoto kadhaa.

  Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kushuka kwa thamani ya fedha katika nchi za Afrika na kukosekana kwa ukanda wa biashara katika baadhi ya maeneo.

  Ushirikiano huo na Bara la Afrika ni wa muda mrefu kwani mwaka 1968 timu ya madaktari kutoka jimbo hili ilitembelea Tanzania na kuanzia wakati huo kumekuwapo na uhusiano endelevu.

  Licha uhusiano huo katika sekta ya afya kampuni ya Inspur kutoka jimbo hili ndiyo iliyoziuzia taasisi kadhaa za umma nchini Tanzania kompyuta kwa ajili ya matumizi ya ofisini ikiwamo Idara ya Uhamiaji.

  Mitambo mingine inayopatikana katika kampuni hiyo ni pamoja na inayotumika katika mawasiliano ya askari polisi, na uhakiki wa ulipaji kodi na utunzanji wa taarifa kwa ujumla.

  Mfumo huo wa utunzaji wa kumbukumbu na taarifa umesaidia kwa kiwango kikubwa katika ufuatiliaji kwa njia za kielektroniki wa mizigo kutoka inapopakiwa hadi inakopakuliwa.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako