• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Balozi mpya wa Tanzania akabidhi nyaraka za utambulisho na kusema kipaumbele kwa sasa ni mafunzo kwa wahandisi wa Tanzania

    (GMT+08:00) 2017-03-22 16:16:59

    Balozi mpya wa Tanzania nchini China Bw Mbelwa Kairuki amehaidi kutumia uhusiano uliopo kati ya China na Tanzania ili kuzalisha wataalamu wa sekta mbalimbali, kwa kuanzia katika miaka mitano ijayo anatarajia kupata wahandisi 1,000. Balozi Kairuki amesema hayo baada ya kuwasilisha hati za utambulisho kwa Rais Xi Jinping, ikiwa ni mwezi mmoja tangu kuripoti kwenye kituo chake cha kazi.

    Balozi Kairuki amesema tangu enzi za kutafuta uhuru, Tanzania na China zimekuwa na uhusiano wa kihistoria, na akiwa mwakilishi wa nchi atahakikisha anatafuta fursa mbalimbali kuhakikisha wanatumia teknolojia za China inayoendelea kwa kasi.

    Amesema katika kupata wataalamu atahakikisha kwa miaka mitano ijayo wanapatikana wahandisi 1,000, ili kusaidia katika usimamizi wa miradi mipya mikubwa ya ujenzi wa miundombinu inayofanywa nchini Tanzania kwa sasa. Bw Kairuki ametaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Standard Gauge, ambao awamu ya kwanza inatarajia kuanza wakati wowote, kuikarabati reli ya Tazara ambayo ilijengwa na China, pamoja na ujenzi wa mji mkuu mpya wa Dodoma.

    Aidha, amesema atahakikisha wataalamu wa Tanzania wanapata nafasi za mafunzo ya muda mfupi katika sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo, Sayansi na Teknolojia, Tehama na nyinginezo, na tayari kwa mwezi mmoja akiwa nchini humu amepata fursa kwa wataalamu 10 kujifunza kuzalisha mbegu bora.

    Balozi Kairuki amesema ataanza kwa kuwatafutia nafasi za mafunzo watanzania kulingana na mpango wa maendeleo kwa kuweka malengo ya kupata idadi fulani ya wataalamu wa serikalini na binafsi. Ameeleza kuwa kuna vyuo nchini Tanzania vinavyotoa elimu hiyo, lakini wengi wanaohitimu hawaendani na mahitaji, hivyo kupata elimu nchini China kwenye utaalamu wa ujenzi wa miundombinu, kutapunguza gharama wakati wa kujenga na hata kufanyia ukarabati wa miundombinu baada ya ujenzi.

    Amesema ili kufikia malengo hayo atatumia njia tatu ambazo ni kuiomba wizara ya biashara, na ya mambo ya nje China kuongeza ufadhili wa wanafunzi katika sekta mbalimbali kutoka 100 hadi 200, huku akishauri serikali asilimia 50 ya ufadhili huo uwe kwa wahandisi na hiyo iwe mpango maalum kwa kila sekta.

    Bw Kairuki pia amesema akiwa hapa China atatembea katika vyuo vikuu mbalimbali ili kuwaomba waongeze ufadhili kwa wanafunzi na wengi wao kwa muda huu wawe wahandisi huku akihakikisha ubalozi unatoa taarifa nchini Tanzania kuhakikisha wazazi wenye uwezo wanawapeleka watoto wao kusoma katika vyuo vyenye viwango ili kupata elimu bora.

    Akizungumzia mafunzo ya muda mfupi kwa wataalamu kutoka Taznania, amesema tayari wataalamu 10 kutoka TIRDO na SUA watafika China mwezi ujao, kwa ajili ya kujifunza jinsi ya kuzalisha mbegu bora huku wengine kutoka taasisi nyingine watafika kujifunza masuala la TEHAMA.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako