• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yataka mataifa ya Africa yatoe habari zaidi kuhusu nafasi za uwekezaji

    (GMT+08:00) 2017-03-30 16:47:45
    Na Eric Biegon - Beijing, China

    Serikali ya China imefichua kuwa iko tayari kuwekeza zaidi katika bara la Africa. Wizara ya biashara ya nchi hiyo hata hivyo inasema ni wajibu wa nchi za Afrika kutoa taarifa za kutosha kuhusu maeneo ya uwekezaji ambayo usimamizi wa Beijing utaingiza rasilimali zaidi.

    "Tunahitaji misingi maalum ya ushirikiano. Pande zote mbili zinapaswa kufanya tafiti kufahamu juu ya mfumo wa ushirikiano na njia ya kifedha ya kuboresha uwezo wa Afrika kufikia kiwango cha kujiboresha yenyewe." Maafisa wakuu wa wizara biashara walisema.

    Wizara hiyo inasisitiza kuwa Afrika ni bara kubwa ya nchi 54 ambazo zina hali tofauti kabisa. Kwa maoni yake, lazima kuwe na usahihi katika suala la miradi ya kuwekeza.

    Bwana Wang Dong, ambaye ni mkurugenzi katika idara ya masuala ya Africa katika wizara hiyo, aidha alikanusha madai kwamba China, ambayo ina Uchumi wa pili mkubwa zaidi duniani, imelimbikizia uwekezaji wake katika uchumi zilizonawiri barani Africa kama vile Kenya, Tanzania, Afrika Kusini na Ethiopia ikilinganisha na nchi zilizo na uchumi ndogo.

    "Kuna maeneo mengi ya ukuaji lakini tunahitaji maelezo zaidi kutoka nchi za ndani. Nchi za Afrika lazima ziweke juhudi kubwa katika kutoa taarifa zinazohitajika. Kwa mfano, wanaweza kutoa taarifa zaidi na ya kina kwa njia ya ubalozi wetu." Alisisitiza

    Akihutubia kundi la waadishi wa habari kutoka Afrika mjini Beijing kuhusu hali ya ushirikiano baina ya China na Afrika, Wang alidokeza kuwa idadi kubwa ya makampuni ya kichina zinanuia kuanzisha shughuli katika bara hilo.

    Hata hivyo alidai kuwa habari kidogo inapatikana hasa kuhusu maeneo mapya ya kuwekeza.

    "Kukiwa na habari za kutosha, makampuni ya Kichina zitakuja Afrika kuanzisha biashara zao." Alisisitiza.

    Hata hivyo alifichua kuwa mazingira ya kazi katika nchi mwenyeji kwa kiasi kikubwa inachangia swala la uwezekano wa uwekezaji kutoka China.

    "Tunahitaji hali na mazingira mazuri ya kuwekeza. Nchi za Afrika lazima zitoe mazingira yanayofaa biashara. "Alibainisha Bw Wang

    Hata hivyo, alisisitiza kwamba utawala wa rais Xi Jinping imeongeza uwekezaji katika nchi zenye uchumi ndogo barani Afrika kwa zaidi ya asilimia 6 kwa mwaka mmoja tu uliopita.

    Serikali hiyo inayoongozwa na Chama cha Kikomunisti imeorodhesha maeneo kumi ya ushirikiano baina yake na Africa kuanzia Viwanda, Kilimo, Miundo mbinu, Kawi, Biashara na uwekezaji, Kupunguza umaskini, Afya, Rasilimali za binadamu, Mpango wa kijamii pamoja na Amani na usalama.

    Kwa mujibu wa ratiba ya utekelezaji, mwaka huu wa 2017 ni mwaka muhimu na China inasema ina nia moja tu, kuhakikisha utekelezaji wake kikamilifu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako