• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yapania kumaliza Ugonjwa wa Malaria duniani ndani ya miaka 10 kwa kutumia MDA

    (GMT+08:00) 2017-04-20 09:59:40
    Na Theopista Nsanzugwanko, Guangzhou, China

    CHINA imeweka mkakati wa kuhakikisha wanatokomeza ugonjwa wa Malaria Duniani kwa kutumia dawa inayoua vimelea vya magonjwa ya ugonjwa huo katika mwili wa binadamu.

    Kundi la watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dawa za asili za Kichina cha Guangzhou waliwaeleza waandishi wa habari kutoka nchi za Afrika waliotembelea Chuo hicho kuwa lengo lao ni kutokomeza ugonjwa wa Malaria katika miaka 10 ijayo kwa kutumia "Mass Drug Administration" (MDA).

    Kiongozi wa watafiti hao, Dk Changsheng Deng alisema kuwa kuzuia maambukizi katika mwili wa binadamu ni suluhisho la kutokomeza ugonjwa huo duniani na hasa katika nchi za Afrika zinazoathirika zaidi kuliko kuzuia kuumwa na mbu au mazalio yao.

    Dk. Deng alisema katika kufanikiwa suala hilo, watatumia dawa itakayoenda katika seli ya mwili wa binadamu na kupambana na vimelea vya Malaria,jambo lilionesha mafanikio makubwa.

    Alisema kutumia mpango wa Fast Elimination of Malaria by Sourcr Eradication (FEMSE) ambayo tayari imefanyiwa majaribio katika nchi zinazokabiliwa na ugonjwa huo kama Kambodia, Comoro, Vietnam na China na kuonyesha mafanikio makubwa na kuwa suluhisho la tatizo hilo.

    "Mpaka sasa hakuna upinzani uliojitokeza katika matumizi ya dawa hii ambayo imeonesha mafanikio makubwa ,kuliko dawa yeyote kutokana na kufanya kazi katika mzunguko wa damu kwa kuangamiza vimelea vya ugonjwa huo" alisema.

    Alisema shirika la afya Duniani (WHO) liliishakubali matumizi ya dawa hiyo miaka miwili iliyopita na tayari wamekaa na maafisa kutoka shirika hilo na kujadili namna ya kutumia dawa hiyo kutokomeza ugonjwa huo katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

    "Tunataka kutokomeza ugonjwa huu katika miaka kumi ijayo, na tuko tayari kushirikiana kitaalamu na nchi za Afrika, lakini kwa ushirikiano wa masuala ya madawa kati ya China na nchi za Afrika yanapitia serikalini hivyo tuko tayari" alisema.

    Dk Deng na timu yake ya watafiti wanashauri kuwa nchi zinazoathirika sana na ugonjwa huo wanahitaji kutumia tiba hiyo ili kupunguza vifo vywa wananchi wengi kwa mujibu wa Shirika la afya duniani anateseka sana.

    Alisema kwa mujibu wa ripoti ya Malaria kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la sahara kwa mwaka 2015 kuna asilimia 89 ya maambukizi ya ugonjwa huo huku kukiwa na asilimia 91 ya vifo vinavyotokana na malaria.

    "Mradi wa majaribio ya dawa hii uliofanyika nchini Comoro na kuonyesha mafanikio makubwa kwa maeneo yaliyokuwa yakisumbuliwa na ugonjwa huo kutokuwa na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo kwa kipindi kifupi" alisema.

    Alisema tathimini ya kudhibiti malaria na Artemisinin plus Mass Drug Administration iliyofanyika nchini Comoro kati ya mwaka 2007-2014 inaonesha maambukizi ya ugonjwa wa malaria yalipungua kwa asilimia 99.8 na kutokuwa na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.

    Alisema kwa nchi za Afrika suala la gharama za matibabu ni jumuishi,kwani matibabu kwa mtu mmoja ni dola za marekani 17.

    Deng alisema katika kuhakikisha nchi za bara la Afrika zinapambana na ugonjwa huo wako tayari kushirikiana na vyuo vikuu, taasisi za utafiti na wanasayansi kutoka nchi za Afrika.

    Naye, Rais wa Chuo kikuu hicho cha Guangzhou, Zhaoliang Wang alisema wanataka rafiki zao wa Afrika kuelewa maendeleo ya matumizi ya Artemisinin kwa kutumia watafiti kukabiliana na tatizo hilo.

    Alisema kwa miaka 19 China wamekuwa wakitoa matibabu hayo na kufanyia maboresho mbalimbali na Madaktari wanaeleza kuwa kwa asilimia 100 matumizi ya matibabu ya Artemisinin Mass Drug Administration ni bora na wameanza majaribio katika nchi za Kenya, Tanzania na Malawi.

    Artemisinin iligunduliwa na mtaalamu wa dawa wa kike kutoka nchini China, Tu Youyou, ambaye alikuwa wa kwanza kupata tuzo ya Nobel katika sayansi kutoka nchini humo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako