• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • "Canton Tower": Mnara wenye hisia mchanganyiko japo kivutio kikubwa cha utalii

    (GMT+08:00) 2017-05-04 08:40:02
    Na Theopista Nsanzugwanko, Guangzhou

    GUANGZHOU ni mji maarufu katika jimbo la Guangdong lililopo Kusini mwa China huku ukiwa na wananchi wengi kutoka nchi za Afrika wakijihughulisha na masuala mbalimbali lakini wengi wao wakifanya biashara za aina tofauti.

    Ni dhahiri kuwa wengi wakisikia mji huo wanahusianisha na masuala ya kibiashara pekee na kusahau vivutio mbalimbali vya utalii vya kitaifa na kimataifa vilivyopo kwenye mji huo.

    Nimepata fursa ya kutembelea mji huo na kukutana na vivutio mbalimbali ikiwemo maonesho ya kimataifa yajulikanayo kama "Canton Fair" yaliyosheheni vitu na Teknolojia mbalimbali kutoka nchi ya China na nyingine duniani.

    Maonesho hayo yaliyoshirikisha kampuni za bidhaa, huduma na mengineyo yamedhihirisha uhusiano imara baina ya China na nchi nyingine duniani katika kukuza Teknolojia mbalimbali.

    Lakini kubwa zaidi unapotembelea mji wa Guangzhou ni vema kufika katika kinara cha utalii kinachofahamika duniani ambao ni mnara wa Canton "Canton Tower" ambao unashika nafasi ya tatu kwa urefu duniani ukiwa na mita 600 .

    Katika mnara huo na mazingira yake, unajionea watalii wengi wa ndani na nje ya nchi wakitembelea na kufika juu ya mnara wanapoangalia mandhari yote ya mji huo huku kukiwa na matukio mbalimbali yanayofanyika ndani ya mnara.

    Mnara huo ambao ni jengo jipya la kisasa ni la kihistoria na kivutio cha utalii likiwa na mita 600 toka usawa wa bahari huku kukiwa na ghorofa zaidi ya 100.

    Katika ghorofa ya 106 kwenye urefu wa mita 424 kuna mgahawa ambao unaweza kukaa watalii zaidi ya 400 kufurahia chakula na mambo mbalimbali .

    Mnara huo ujenzi wake ulifanyika kuanzia mwaka 2007 na kufunguliwa kwa umma mwaka 2010 ukiwa wa tatu kwa urefu duniani ambapo wa kwanza ukiwa na mita 828 wa nchini Dubai na wa pili una mita 634 ukiwa Tokyo Japan.

    Mnara wa Canton una eneo la mita za mraba 114,054 na una umbo la mita 450 huku antena ya mlingoti ya mita 150 juu, kwenye umbo la kujisokota huku unadhifu wake ukiongezwa na taa zenye rangi mbalimbali hasa nyakati za usiku unafanya mnara huo kuonekana wa kipekee.

    Viongozi wa jimbo la Guangdong wanaeleza kuwa maelfu ya watalii wanafika katika mnara huo kutoka sehemu mbalimbali duniani na kufanya kuwa eneo la kivutio cha utalii.

    Wanaeleza kuwa tangu ulipofunguliwa na kuwa kivutio imeingiza mamilioni ya Dola za Marekani katika sekta ya utalii.

    Watu wa mataifa mbalimbali wamekuwa wakifika katika mnara huo kwa shughuli mbalimbali kutokana na huduma zinazopatikana ikiwemo kupiga picha za harusi,mgahawa, michezo mbalimbali,kumbi za sherehe na mengineyo.

    Mnara huo umejengwa kwa malighafi, na uzito wa jumla ya tani 50,000 unaowezesha kukabiliana na majanga mbalimbali ikiwemo tetemeko la ardhi.

    Katika kupanda mnara huo "lift" zinatumia muda mchache wa dakika moja na nusu kutoka eneo la chini la jengo hilo hadi juu kwenye ghorofa hizo zaidi ya 100.

    Katika lift hizo unapopewa tahadhari ya masikio kupata shida kidogo kutokana na mwendo wa haraka kuna kifaa cha hewa kudhibiti hewa katika lifti na kuelezwa ni kifaa cha kwanza duniani kuwekwa kwenye lifti.

    Malipo kwa ajili ya kupanda katika mnara huo ni tofauti kulingana na umbali unaotaka kwenda kwani ukiwa juu kabisa ya mnara huo, unaweza kuona maeneo ya mji huo kwa upana zaidi .

    katika mnara huo unaweza kupandishwa juu zaidi kwa kutumia kifaa maalum "Sky Drop" kwa watu watano na kuwapeleka juu zaidi kisha kuwashusha kwa mwendo wa kasi.

    Kwa waliobahatika kupanda katika kifaa hicho kilichowekwa katika rekodi ya dunia "Guiness World record", unaweza kupandishwa hadi mita 455 hadi 485.

    Kwa kutumia "Sky Drop" unaweza kukaa au kusimama kwa kadri unavyoweza lakini wengi wanaojaribu wanasimulia hofu kubwa kwa jinsi unavyopelekwa juu na kushushwa.

    mmoja wa waliopanda kifaa hicho licha ya kueleza jinsi alivyopata hofu kubwa wakati wa kushuka lakini amepata uzoefu mkubwa ambabo hawezi kuupata sehemu nyingine.

    Pia katika mji huo kuna, ufukwe wa Pearl River ambao ni mto wa tatu kwa ukubwa nchini China ukiwa na urefu wa Ml 1500 ambao kwa jina maarufu la kichina ni Zhujiang River, huku awali ukifahamika kama "Canton River" .

    Nyakati za usiku utashuhudia watalii wakiwa katika meli wakiangalia mandhari nzuri ya mji huo ikiwemo mnara unaovutia ulio kwa taa za aina mbalimba na mandhari ya mto huo mkubwa unaopita barabara juu .

    Ukiwa ndani ya meli ukifurahia mandhari yake, hasa nyakati za usiku unakuwa katika mgahawa ambao unapatiwa vinywaji vya aina mbalimbali na natunda huku ukizunguka kuangalia pande zote.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako