TANZANIA na China imekuwa na mahusiano ya muda mrefu katika sekta mbalimbali ukiwemo uhusiano wa Kidplomasia, kiuchumi, kisiasa pamoja na kijamii.
Kutokana na mahusiano hayo na kijiografia, Tanzania ni nchi mojawapo kati ya nchi nne za Afrika zilizohusishwa katika pendekezo la Ukanda Mmoja na Njia Moja iliyoundwa na Rais wa China Xi Jinping kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kutimiza maendeleo ya pamoja na kuonesha utekelezaji wa majukumu wa China na nchi wajumbe wa pendekezo hilo.
Katika nchi za Afrika, pendekezo hilo limejikita katika nchi nne ambazo ni Kenya,Tanzania, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) katika ujenzi wa miundombinu,uwekezaji, ujenzi wa viwanda na mengineyo kwa lengo la utekelezaji wa pendekeo hilo.
Kando ya mkutano wa kilele wa Baraza la kimataifa la Ukanda Mmoja na Njia Moja ukifanyika kwa siku mbili,ujumbe kutoka Tanzania ulikutana katika mji wa Changzhou katika Jimbo la Jiangsu lililoteuliwa na Serikali ya China kuwekeza nchini Tanzania wakisaka wawekezaji.
Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Waziri wa Biashara, viwanda na Masoko wa Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali pamoja na Balozi wa Tanzania nchini China , belwa Kairuki.
Katika mji huo,kulifanyika mkutano mkubwa uliojulikana kwa jina la Mkutano wa fursa za Uwekezaji na Biashara Tanzania "Forum of Investment and Trade Opportunities in Tanzania", ikiwa ni uhamasishaji uwekezaji katika viwanda mbalimbali kusaidia kukuza uchumi wa nchi na kuongeza ajira.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wawakezaji kutoka katika mji huo zaidi ya 100 kuhusu changamoto mbalimbali za uwekezaji nchini Tanzania ambapo Waziri Amina kwa kushirikiana na watendaji wa taasisi zinazohusika na uwekezaji na Biashara nchini waliwapatia ufafanuzi wawekezaji hao.
Mara baada ya mkutano tayari wawekezaji 20 walihaidi kutembelea nchini Tanzania, mwezi ujao ili kujionea maeneo mbalimbali ya uwekezaji hasa katika sekta za vyakula, kilimo, ujenzi, Ushonaji na viwanda vingine.
Katika mkutano huo, watendaji wa serikali waliokuwepo ni kutoka kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) John Mnali, Mwakilishi wa Kituo cha Uwekezaji Zanzibar, Nasriya Nassor, Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Godwill Wanga na Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Joseph Simbakalia.
Akizungumza katika mkutano huo,Waziri anasema kuwa fursa hiyo ya kueleza uwekezaji nchini ni kupitia pendekezo la Ukanda Mmoja na Njia Moja inayotekelezwa na China kwa Tanzania kutafuta fursa mbalimbali za uwekezaji.
Anasema kijiografia nchi ya Tanzania imekuwa sehemu ya kuunganisha nchi za Afrika Mashariki kwa kutumia miundombinu mbalimbali ikiwemo inayopendekezwa katika kipaumbele hicho
Kwa kutumia kipaumbele hicho,Tanzania inaendesha miradi ya Bandari mpya ya Bagamoyo na kupanua bandari za Mtwara, Dar es Salaam and Tanga huku ukiendelea ujenzi wa reli ya kati na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Kimataifa vya Julius Nyerere na kile cha Zanzibar .
Anasema katika kurahisisha usafiri kutoka Tanzania na China,kwa kutumia Shirika la Ndege la Serikali (ATCL) ndege mpya inatarajia kufika nchini mwaka huu itafanya safari zake baina ya nchi hizo mbili.
Mji wa Changzhoe ni mji Rafiki na jiji la Dar es Salaam msafara huo ulitembelea viwanda mbalimbali vinavyotaka kuwekeza nchini ikiwa ni kuona utendaji wake ambavyo ni kiwanda cha kutengeneza Makoti cha Yilingwiye Fibre-Making na kampuni ya ChangzhouMachinery and Equipment Import and Export kinachotengeneza mashine mbalimbali.
Waziri Amina anazungumza mara baada ya mkutano kuwa wamepata mafanikio makubwa kwani kampuni zaidi ya 20 wamesema wataenda nchini kuangalia maeneo ya uwekezaji.
Anasema wawekezaji hao wanaoenda nchini wanataka kuwekeza katika sekta za viwanda vya nguo,vifaa vya ufundi, kilimo, ujenzi na mengineyo baada ya kupata maeneo watafanya maamuzi.
Anaeleza kuwa baada ya kukutana na wawekezaji hao waliikuwa na masuala mbalimbali yaliyohitaji ufafanuzi ikiwemo hisa, kodi, hati na mazingira mengine waliyoona yana utata katika uwekezaji.
Waziri anasema kwa kuchirikiana na watendaji alioambatana nao waliweza kuwapa ufafanuzi wa masuala hayo kama serikali na kuwa kuna kamati imeundwa ya kurekebisha baadhi ya mambo yaliyokuwa yakisumbua hapo awali.
"Baada ya kuwapatia ufafanuzi imeonesha kuwahamasisha wawekezaji hao toka China na kuhaidi kuangalia maeneo ya kuwekeza kwa kutumia ofisi maalum iliyofunguliwa na jimbo hilo nchini kuhamasisha biashara na uwekezaji" anafafanua.
Lakini pia alitaka wawekezaji toka China wanapofika kutafuta maeneo ya uwekezaji nchini kukutana na taasisi husika za serikali ili kuepuka matapeli wanaoeleza kuwa masuala ya uwekezaji nchini ni magumu kwa lengo la kujipatia pesa.
Kuanzia mwaka 1996 mpaka sasa tayari kampuni sita kutoka mji huo wameishawekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo utoaji huduma, nguo, jenzi usambazaji vifaa vya umeme.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |