• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Mchango wa dola milioni 20 kutoka China wa Uhifadhi Mazingira na Wanyamapori Afrika

  (GMT+08:00) 2017-05-26 10:57:52
  Na Eric Biegon, Beijing, China

  Serikali ya China imedhihirisha nia yake kubwa ya kuhifadhi mazingira na wanyamapori kwa kuongeza fedha kwa sekta hii Afrika kwa dola milioni 20 za Marekani. Toleo hili ni mara mbili ya kiasi cha fedha zilizoahidiwa mwaka wa 2014 na nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi barani Asia.

  Wakati wa ziara yake Kenya mwaka wa 2014, Waziri Mkuu wa China Li Keqiang alitangaza kuwa serikali ya Rais Xi Jinping ilikuwa imetenga dola milioni 10 za Marekani ili kuimarisha juhudi za kulinda asili na wanyama pori.

  Wakati huo, Li pia alizuru mbuga ya wanyama ya Nairobi katika ishara ya mfano wa kujitolea kwa China kwa mapambano dhidi ya ujangili na magendo ya bidhaa za wanyamapori kwa nchi yake.

  Kenya, ilionekana kama kitovu cha mpango huu kutokana na kwamba China ilitangaza kuwa inaweza kusaidia kuanzisha kituo cha Ekolojia na Wanyamapori, African Ecological and Wildlife Centre, katika mji mkuu wa nchi hiyo, Nairobi.

  Muda mfupi baadaye, shirika la uhifadhi wanyama pori la Kenya KWS, ilibainisha kwamba China ilikuwa imeahidi kutoa ruzuku kuiwezesha kupata vifaa vya ufuatiliaji wanyama mchana na usiku.

  Hizi ishara na matangazo zilipokea sifa kede kede kutoka kwa wanamazingira wa ndani ambao kwa maoni yao China hatimaye ilionyesha dhamira ya mazingira na ulinzi wa wanyamapori.

  Lakini inaonekana hii ilikuwa mwanzo tu, kwani utawala huo ulioko Beijing limetangaza kuwa kitita hicho imeongezwa maradufu kutoka dola milioni 10 hadi dola milioni 20 za Marekani. Hii iliwekwa wazi na utawala wa misitu China.

  "Kama nchi inayowajibika, China imekuwa makini kutekeleza mikataba ya kimataifa, kushiriki katika mambo ya kimataifa na kufanya ushirikiano wa kimataifa na masoko ya juu ya uhifadhi wanyamapori. Mwaka 2010 tulitangaza dola milioni 10 za Marekani kama msaada kwa Afrika kwa mambo ya uhifadhi. Kwa sasa tumeongeza kiwango hicho hadi dola milioni 20 za Marekani." Bwana Wang Weisheng, ambaye ni naibu mkurugenzi mkuu wa Uhifadhi wa Wanyamapori katika afisi ya Utawala wa Misitu alisema.

  Pembe Haramu

  Kando na kitita hiki, utawala huo ambao unasimamia biashara ya pembe za ndovu, inasema serikali ya China imetoa fursa nyingi kwa ajili ya kujenga uwezo kwa mamia ya maofisa kutoka Afrika kwa uhifadhi wa wanyamapori.

  "Tumekuwa tukiandaa mafunzo ya kimataifa na ubadilishanaji wa habari na teknolojia, kutoa msaada wa kifedha na kiufundi kwa nchi husika na kufanya kazi kwa pamoja na nchi nyingine ili kuchunguza biashara haramu." Maafisa wa Idara ya misitu ya China walisema.

  China imekosolewa kwa madai ya kufungua milango yake kwa bidhaa haramu siku za nyuma. Maono haya kulingana na maafisa wa Kichina kwa kiasi kikubwa hayana msingi. Kwa maoni yao, taifa hilo la kikomunisti limefanya mambo mengi katika miaka michache iliyopita ili kuzuia biashara ya bidhaa za wanyamapori.

  "Tuna sheria ambayo ndio kali sana duniani. China imerasimu mfululizo wa sheria na kanuni juu ya uhifadhi wa wanyamapori. Kwa hiyo, utovu cha sheria ya ununuzi, usafirishaji na mauzo ya pembe za ndovu na bidhaa zake unaadhibiwa vikali." Alisema Bwana Wang.

  Adhabu Kali

  Rekodi katika idara hiyo ama kweli zinaonyesha kuwa kuanzia mwaka 2012 kufikia mwaka 2014, watu 458 walikamatwa kwa tuhuma za magendo ya pembe za ndovu. Waliopatikana na pembe yenye thamani zaidi ya dola 145,000 za Marekani walipewa vifungo vya miaka 10 gerezani.

  Maafisa hao wakuu wanadumisha kwamba China haifanyi mzaha katika harakati zake za uhifadhi wa mazingira na wanyamapori. Wao wanalaumu mtazamo huu juu ya taarifa potovu ambazo walifichua kuwa ndio kibarua ifuatayo katika juhudi za ujenzi wa ekolojia.

  "Adhabu yetu juu ya biashara haramu ya wanyamapori ni mbaya zaidi kote duniani. Hiyo ni ukweli. Ni ukweli mtupu." Alisisitiza bwana Li Tiansong, ambaye anafanya kazi katika kituo cha utangazaji kwa idara ya misitu China.

  Katika uhalifu wa hali ya juu, maafisa hao wanasema wahalifu wanapewa kifungo cha maisha na wengine kupokonywa mali yao.

  "Wanyama wa pori walioko hatarini na bidhaa zao zikiwepo pembe za ndovu, mifupa ya simba marara na pembe za vifaru, zimepigwa marufuku kuingia China kinyume cha sheria na kuondoka kupitia gari, kifurushi au barua pepe." Bwana Wang alisisitiza.

  Ripoti iliyochapishwa na gazeti la China Daily inaonyesha kwamba 12 kati ya 24 ya makampuni zinazoshughulika na usindikaji wa pembe zimefungwa chini ya muda wa miezi mitatu iliyopita na utawala wa China. Ripoti hiyo inaendelea kusema idadi ya wauzaji wa biashara ya pembe za ndovu imepungua kutoka 149 hadi 94 kufikia sasa.

  Serikali ya China daima inashikilia nafasi yake juu ya suala hilo na kudumisha kwa wote kwamba usindikaji na biashara ya pembe za ndovu itakuwa marufuku mwishoni mwa mwaka huu.

  Ushirikiano na Mataifa

  Idara ya misitu ya China inasema nchi hiyo imeungana na nchi nyingine na mashirika ya kimataifa kupiga jeki shughuli za kupambana na biashara ya bidhaa za wanyama walioko hatarini. Mojawapo ya operesheni ile ni "Cobra".

  Matokeo yake, China inasema zaidi ya biashara hiyo haramu 850 zilivumbuliwa wakati wa operesheni hiyo. Katika ripoti iliyoko kwenye idara hiyo, kesi 300 ya biashara hiyo haramu zilipatika China.

  Maafisa hao wa misitu walidokeza kwamba tangu ziara ya Waziri Mkuu Li Keqiang kwa Kenya, Ethiopia, Nigeria, na Angola Mei 2014, hatua zaidi zimechukuliwa ili kuinua juhudi za ushirikiano juu ya uhifadhi wa mazingira na wanyama kati ya Afrika na China.

  "China imesaini makubaliano ya nchi na nchi juu ya ulinzi wa wanyamapori na Kenya, Tanzania na Afrika Kusini hadi sasa. China imetoa vifaa kwa nchi hizi za kuongeza juhudi za uhifadhi." Bwana Wang alisema.

  Hii ikiwa ni pamoja na wataalam kutoka China kutembelea Afrika na kufanya utambuzi wa jinsi ya kujenga mpango wa kina juu ya kukabiliana na biashara haramu.

  Hata hivyo, Wizara ya Misitu inakubali kwamba mengi bado yanahitaji kufanyika ili kuimarisha juhudi za uhifadhi. Kwa upande wake, maafisa hao walisema Beijing itaimarisha utangazaji, elimu na ushirikiano wa kimataifa, na kufanya kazi na jamii ya kimataifa kukabiliana na changamoto muhimu, na kuafikia upeo mpya katika kuhifadhi wanyamapori.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako