• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Mafanikio ya Kihistoria China katika kurejesha jangwa kuwa rafiki wa binadamu, wanyama na mimea

  (GMT+08:00) 2017-06-30 09:04:36
  Na Theopista Nsanzugwanko, Inner Mongolia, China

  JANGWA la Kubuqi lililopo katika mji unaojitawala nchini China wa Inner Mongolia ni mfano tosha kwa nchi mbalimbali duniani hususan Afrika zinazokabiliwa na changamoto ya kuwepo jangwa au kuongezeka kwa hali hiyo.

  Katika jangwa hilo lenya ukubwa wa kilometa 18,000 wamefanikiwa kurejesha hali ya maisha ya watu kwa kuondoa umasikini licha ya miaka ya nyuma watu wa maeneo hayo kukimbia kuishi kutokana na hali ya hewa.

  Ukifika katika eneo la jangwa hilo kwa kiasi kikubwa utashangaa kwa jinsi kulivyo na hali ya hewa ya kijani kwa kuwepo kwa miti ya aina mbalimbali maeneo ambayo awali hakukuwa na miti,hakukufanyika kilimo au shughuli mbalimbali za maendeleo ya kibinadamu.

  Waandishi wa habari 27 kutoka nchi za Afrika walitembelea jangwa hilo na kujionea mafanikio makubwa yaliyopatikana ikiwa ni pamoja na kuendelea kwa shughuli za kibinadamu,maendeleo ya kiuchumi na utunzaji wa mazingira na wao kushiriki kupanda miti.

  Ikiwa ni miaka 29 sasa kati ya miaka 30 iliyopewa kampuni ya Elion Resources Group (ELION) kwa ajili ya kupambana, kuondoa na kuzuia jangwa na kufanya eneo hilo la jangwa kuwa rafiki wa mazingira kwa binadamu, wanyama na mimea.

  Kampuni hiyo iliyoanzishwa na Wang wenbiao miaka ya 1990 imepewa kazi na serikali ya nchi hiyo katika kuhakikisha eneo hilo linabadilika na tayari wamefanikiwa kwa robo ya eneo hilo ambalo ukifika hutafahamu kama kulikuwa jangwa kwani shughuli mbalimbali zinaendele.

  Kitakachokuonesha utofauti ni baadhi ya sehemu zinazoendelea kufanyiwa kazi kwa kupandwa miti na kuandaa mashamba na ufugaji katika eneo hilo ndiyo kunaweza kukupa picha kamili ya eneo hilo lililokuwa mwanzo.

  Lakini Kampuni hiyo iliyowekeza zaidi ya pesa za China bilioni 1 kwa ajili ya utafiti na maendeleo na kujua nini cha kufanya jambo lililosaidia kufikia maendeleo hayo na sasa wanaomba kuongezewa miaka 20 ili kufanikisha kumaliza tatizo hilo katika eneo lote.

  Afisa mtendaji wa kampuni hiyo, Zhao Xu anaweka wazi kuwa katika kipindi hicho waliwekeza zaidi ya RNB bilioni 30 lakini sasa eneo hilo lina uwezo wa kukuza uchumi wa thamani ya RNB bilioni 100 katika kilimo, ufugaji, utalii, viwanda, madawa na nishati ya kisasa.

  Anasema katika eneo hilo wana mimea ya aina zaidi ya 1,000 kama "Cistanche" na "Sacsaoul" inayoweza kukua katika hali ya hewa ya eneo hilo huku watu zaidi ya 100,000 wakinufaika kwa kubadili maisha yao.

  "Hakika licha ya kubadili maisha ya watu wa hapa hata afya za wananchi wa mji wa Beijing zimeimarika kutokana na vumbi la Jangwa lililokuwa likielekea katika mji huo kupungua kutokana na kuzuiwa na miti iliyopadwa" anasema.

  Anasema kwa kutumia mimea inayostawi katika maeneo hayo wameanzisha viwanda vya madawa asilia ya kichina yanayotokana na mimea hiyo ikiwa ni pamoja na kuunda taasisi ya utafiti kuendeleza dawa za asili kutoka maeneo ya jangwa na vyakula vya asili.

  Anasema walivyoanza wananchi wengi walishangaa na kuona kama wanapoteza muda kutokana na kuona jambo hilo halitawezekana lakini waliwashirikisha kwa kuwafundisha kupanda miti kwa kuwapatia pesa ya China 30 kwa kila mti uliopandwa lakini kwa ukosefu wa teknolojia ni miti michache ilikua.

  Baadaye waliwafundisha Teknolojia zitakazowezesha miti kukua na kuwalipa RNB 2,000 kwa mwezi jambo lililofanya wananchi kushindana katika upandaji miti huku wengine wakifanya ndiyo ajira zao za kuwapatia vipato. Anasema kwa sasa wana wanachama 5,000 ambao wamejikita katika miradi ya upandaji miti na mengineyo na kusaidia katika ujenzi wa miundombinu kama barabara, shule, nyumba, hospitali, kilimo na mengineyo.

  Kwa kutumia barabara zinazopita katikati ya jangwa hilo imewezesha wakazi wa maeneo hayo kusafirisha bidhaa kutoka maeneo tofauti. Pia kwa wakulima wameweza kupatiwa mimea inayohimili ukame katika maeneo ya jangwa na kuleta faida ukiwemo mmea ambao unatumika kutengeneza dawa nyingi za asili nchini China na mengineyo. Anasema Wenbio ameahidi dunia kupitia Shirika la umoja wa mataifa kuhakikisha katika kipindi cha miaka 10 nijayo watakuwa wameokoa eneo la kilometa za mraba 10,000 katika hali ya jangwa duniani na kufanya kuwa na mazingira rafiki kwa binadamu,mimea na viumbe vingine.

  Kwa sasa kampuni hiyo imeanza kueneza njia hizo za kupambana na uwepo wa jangwa katika maeneo mengine nchini China kama Qinghai – Xizang na eneo la Hebei Zhangbei. Kuanzia mwaka 2007, Umoja wa Mataifa uliteua eneo hilo la Kubuqi kuwa eneo maalum la kufanyika mikutano ya kimataifa ya kila mwaka ya kukabiliana na hali ya jangwa na maendeleo ya uchumi katika maeneo yenye hali hiyo duniani hivyo kufanya kuwa eneo maalum la kuweka mikakati ya kukabiliana na hali hiyo.

  Mkurugenzi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP Erik Solheim amesema mafanikio ya China katika kurejesha misitu katika maeneo ya jangwa ni mfano kwa nchi nyingine katika kukabiliana na athari za kuenea kwa jangwa. Solheim anasema, badala ya kulichukulia suala la kuenea kwa jangwa kama tatizo, inapaswa kutazamwa kama fursa ya maendeleo ya uchumi na kutoa nafasi za ajira. Solheim alikuwa akizungumzia jangwa la Kubuqi ambalo ni la saba kwa ukubwa nchini China lililoko kwenye mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya Ndani, ambapo katika miongo mitatu iliyopita, robo ya eneo la jangwa hilo imegeuzwa kuwa msitu.

  Nchi za Afrika kupitia jangwa la Sahara ambalo lina eneo la takriban asilimia 30 za bara lote la Afrika,wanaweza kujifunza kupitia kampuni hiyo kuthibiti kuenea zaidi. Nchini Tanzania inaelezwa kukabiliwa na hali ya kuenea kwa jangwa na ukame ambapo takwimu zinaonyesha kuwa takriban asilimia sitini na moja (61) ya eneo la nchi liko katika hatari ya kugeuka jangwa. Miongoni mwa mikoa ambayo imeathirika zaidi ni pamoja na Singida, Dodoma, Shinyanga, Manyara, Simiyu, Geita na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Arusha.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako