• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Taasisi zaungana kuzuia kuenea kwa maradhi ya Ukimwi Afrika

    (GMT+08:00) 2017-07-14 18:34:31


    Na Eric Biegon, Beijing – China

    Juhudi za kimataifa za kuzuia maambukizi na kuenea kwa maradhi ya ukimwi unashika kasi. Jicho la dunia sasa linaangazia juhudi za kuwashawishi watu wengi iwezekanavyo ili kujua hali zao.
    Programu ya Umoja wa Mataifa kuhusu HIV & AIDS (UNAIDS), imeshirikisha msaada kutoka taasisi mbalimbali hasa vyombo vya habari ili kuhamasisha watu hasa katika Afrika kukumbatia utamaduni wa kujipima ili kuhakikisha wote wanatambua hali zao za afya. Hii ikiwa ni  katika jitihada za kuhakikisha ugonjwa wa ukimwi utakoma kuhorodheshwa kama tishio la afya ya umma kufikia mwaka 2030.

    UNAIDS hivi karibuni ilisaini mkataba na chombo maarufu cha habari nchini China StarTimes Group, ambapo taasisi hizo mbili zitafanya kazi kwa pamoja ili kuongeza ufahamu kuhusu ugonjwa wa ukimwi  kupunguza unyanyapaa na ubaguzi wa watu wanaoishi na maradhi hayo.

    Hata hivyo mkataba huu wa maelewano ulitiwa saini huku kukiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu wale ambao bado hawajui hali yao ya afya.

    "Tuna asilimia 45 ya watu ambao wameathirika na ukimwi lakini bado hawajui. Wataendelea kueneza ugonjwa huu kwa kutojua." Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Michel Sidibe alibainisha.


    Ndani ya makubaliano hayo, vipindi kadhaa vitapepererushwa kwenye televisheni katika mitandao ya matangazo ya Startimes ambayo inapatikana kote barani Afrika.
    "Sisi tunaungana na nyinyi kupambana na adui huyu wa binadamu. Ni juhudi za ulimwengu wote." Akasema rais wa Startimes Group Pang Xinxing.

    Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS alionyesha matumaini kwamba janga hilo  litadhibitiwa kwa kiasi kikubwa kama watu watapata elimu ya kutosha kuhusu kujilinda wenyewe.

    "Tunahitaji kuweka watu zaidi kwa matibabu. Iwapo tutafanya hivyo, tutapata mafanikio mengi. Nafurahi tuna mpango huu kwa sasa. Tunataka kufikia watu milioni 18 ambao hawana uwezo wa kupata dawa. Maisha yao yamebaki katika mizani." Sidibe alisema kwa wasiwasi mkubwa.
    Hata hivyo Sidibe ana maoni kwamba maelezo ya kutosha yatawezesha watu kujihami na kuwa na uwezo wa kulinda afya zao wenyewe huku akitoa rai  kwa wadau wote kuinua juhudi zao marudufu ili kutimiza malengo ya huba sifuri, Vifo sifuri na unyanyapaa na ubaguzi sifuri.

    "Iwapo tutaweza kufikia watu mahali walipo, kuwahamasisha juu ya matumizi ya kondomu, kuwawezesha kupata habari kamili, basi tutakuwa na uwezo wa kupunguza maambukizi mapya mno." Alisema Sidibe

    Maneno yake yalipata uungwaji mkono kutoka kwa rais wa Startimes ambaye anasisitiza kwamba "Habari ni msingi ili kushinda vita dhidi ya ukimwi. Ugonjwa huu unaweza kumalizwa iwapo sisi wote tutufanya kazi kwa pamoja "

    Kwa maoni yake, Pang alisema ushindi dhidi ya janga hili utapatikana lakini akazungumzia hofu yake kuhusiana na changamoto zilizopo katika juhudi za usambazaji wa taarifa kuhusu kuzuia virusi kwa watu wote.

    "Startimes imeamua kufanya kazi na UNAIDS kwa sababu tuna uwezo na tuna wajibu wetu wa kijamii na hii ndiyo sababu sisi tunaungana kwa pamoja." Akasema bwana Pang

    Kwa mujibu wa Pang, Startimes ilianza kupeperusha vipindi kuhusu ukimwi katika mtandao wake mwaka wa 2016 na hata ikashiriki katika usambazaji wa habari kuhusu Ebola nchini Nigeria, Sierra Leone na Guinea wakati virusi hivyo vilizuka katika Afrika Magharibi kati ya 2014 na 2015.

    Startimes ina mpango wa kutangaza ujumbe kuhusu maradhi ya HIV na Ukimwi hasa kuzuia, kupima mapema pamoja na kutafuta matibabu kwa zaidi ya nchi 45 za Afrika bila gharama yoyote kwa shirika la Umoja wa mataifa. Kwa maoni ya Sidibe, uamuzi huu ni wa kihistoria.

    "Tukiendelea kwa mwendo huo huo na kuongeza kasi, tutakuwa na uwezo wa kuweka watu zaidi kwa matibabu na kupunguza maambukizi kwa asilimia 95 kutoka mtu hadi mwingine," Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Umoja wa Mataifa alisema.

    Kinachoonekana kuvutia shirika la UNAIDS hata zaidi,  ni mradi unaoendelea wa Startimes wa kufikia vijiji 10,000 katika Afrika. Vijiji hivi, bila kujali umbali, vitakuwa na uwezo wa kupokea picha za digitali kupitia Televisheni spesheli inayotengenezwa na Startimes, inayotumia miale ya jua  kwa maeneo ambayo hakuna umeme.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako