• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Hifadhi ya Summer Palace, kivutio cha Utamaduni na Utalii 

  (GMT+08:00) 2017-07-24 11:12:17

   

  Na Eric Biegon katika Beijing, China

  Hifadhi ya Summer Palace mjini Beijing inajumuisha ziwa kubwa bandia, kisiwa na kilima vilivyotengenezwa na binadamu.

  Moja ya maeneo mengi yanayotembelewa sana na watalii katika mji mkuu wa China, Beijing, ni Summer Palace. Hapa ni nyumbani mwa wafalme wakuu wa zamani wa taifa la China. Ni sehemu iliyoko Kaskazini-magharibi mwa mji wa Beijing na imejengwa katika ardhi yenye upana wa kilometa 3.08 mraba.

  Ni sehemu ambayo ni muhimu kutembelea jijini Beijing jinsi ilivyo "the Great Wall" na makavazi ya ikulu maarufu kama "Forbidden City." Ama kwa kweli Summer Palace inaaminika kuwa sehemu walimokimbilia watawala wa zamani waliokimbia majira ya joto jingi.

  Hifadhi hii pia lina maeneo makubwa ya bustani, majengo, ziwa bandia ya Kunming na vijito kadhaa vilivyotengenezwa na mwanadamu bila kusahau vilima vilivyotengenezwa na binadamu.

  Asilimia 75 ya eneo lenye maji kwa sasa ni sehemu ambapo udongo ulichimbuliwa na kutumika katika ujenzi wa mlima mrefu unaozingira sehemu hiyo. Ziwa Kunming kwa sasa ina viziwa tatu bandia zikiwemo Nanhu, Tuancheng na Zaojiantang.

  "Summer Palace ni kivutio kikubwa kwa watalii wa ndani na nje," Kathleen Xie, ambaye kazi yake ni kuelekeza watalii wanaozuru sehemu hii alisema.

  "Kwa wakati huu wa mwaka, tunapokea wageni 20,000 kwa wastani kwa siku, lakini idadi inaongezeka wakati wa hafla maalum," aliongeza mwanamke huyo ambaye amefanya kazi katika hifadhi hiyo ya umma kwa miaka 13 sasa.

  Nauli ya kuingia katika hifadhi hiyo, ikiwa ni pamoja na safari ya mashua juu ya ziwa Kunming inagharimu Yuan 30 pekee au dollar 5 za marekani.

  Nilipozuru hifadhi hiyo hivi karibuni wageni waliozuru sehemu hiyo hawakuzuiliwa na mvua kidogo iliyokuwa ikinyesha.

  Makundi ya watalii waliofika hapa walishikilia miavuli na wengine wao waliovaa mavazi maalum ya mvua, walifuatilia kwa makini na kusikiliza wasimamizi wa hifadhi hiyo wakielezea asili na nafasi ya kila masalio au vituo vya Summer palace.

  Kila baada muda fulani, wote waliofika walichukua picha za kipekee au za kikundi labda tu kwa minajili ya kukumbuka hifadhi hii ya kifalme ya kale.

  Wazo la kutengenezwa kwa Summer Palace ilitolewa miaka ya 1153 wakati wa utawala wa Jurchen, wakati mfalme Wanyan Liang alibadilisha makao makuu ya Jin hadi kutoka Huining hadi mji wa Beijing.

  Hatimaye, mfalme huyo alitoa amri ya kujengwa kwa ikulu ndani ya sehemu hiyo iliyokuwa na vilima vilivyojaa miti yenye harufu nzuri.

  Katika mwaka wa 1271, wakati wa Utawala wa Yuan, mhandisi Guo Shoujing alianza juhudi za kuelekeza maji kutoka Shenshan Spring iliyokuwa kijijini Baifu kuingia ziwani Kunming ili kuhakikisha ugavi wa maji imara kwa ikulu.

  Summer Palace hatimaye ilikamilika mwaka 1764 kwa gharama korongo ya zaidi ya milioni 4.8 pesa za wakati huo

  Desemba mwaka wa 1998 Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la umoja wa mataifa UNESCO, liliratibu ikulu hiyo katika orodha yake ya urithi wa dunia.

  Kulingana na shirika la UNESCO, Summer Palace ilipata nafasi ile kwani "Mazingira ya asili ya milima na maji ya wazi imeoanishwa pamoja na vipengele muhimu bandia kama vile mabanda, kumbi, majumba, mahekalu na madaraja kuunda sehemu iliyojaa usawa wa thamani bora."

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako