• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • China yaahidi mahusiano dhabiti na nchi marafiki baada ya mafanikio yake ya kiuchumi

  (GMT+08:00) 2017-10-21 15:45:30

  Na Eric Biegon katika Beijing, China

  Rais wa China Xi Jinping sasa anasema uchumi wa nchi yake ilistahimili dhoruba kali na kuinuka tena baada ya kipindi ambapo ilisajili utendaji usio wa kuridhisha.

  Kiongozi huyo wa Kichina alisema hayo huku akisisitiza kuwa Beijing itabaki mwamba wa kiuchumi duniani. Rais huyo alifichua kwamba pato la nchi yake limeongezeka kwa trilioni 4 Dola za Marekani katika miaka mitano iliyopita.

  Kwa sababu hii, Rais Xi alitoa hakikisho kwamba China itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kimataifa, na kudumisha kuwa serikali yake "haitafunga milango yake kwa mataifa ya nje; ila itaendelea kuwa wazi zaidi na zaidi."

  Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kongamano la kitaifa la 19 la Chama tawala cha Kikomunisti ya China, CPC, Jumatano, kiongozi huyo wa China alisema kwamba uchumi huo ambao ni wa pili kwa ukubwa duniani imedhihirisha ishara za kufufuka na kuahidi kwamba uchumi huo tajiri barani Asia itabaki dhabiti kuanzia sasa kwenda mbele.

  Rais Xi aliyeonekana mchangamfu, alielezea mafanikio ya serikali yake tangu alipoingia madarakani mwaka 2012, akisema uchumi wa nchi yake imedumisha kiwango cha ukuaji wa kati ya juu na kufanya China kiongozi miongoni mwa mataifa ya uchumi mkubwa.

  "Ikiwa pato la kitaifa lilipanda kutoka trilioni 54 hadi trilioni 80 Yuan (trillioni 8.3 dola za Marekani hadi trilioni 12.3 Dola za Marekani) China imeimarisha nafasi yake kama uchumi wa pili kwa ukubwa duniani na kuchangia zaidi ya asilimia 30 ya ukuaji wa uchumi wa dunia." Alisema Xi.

  Rais Xi alisema matokeo mazuri yalirekodiwa kwa sababu serikali yake ilitumia njia bora ya maendeleo na ikajaribu kubadilisha mtindo wa ukuaji.

  "Taasisi mpya ya uchumi wa wazi imekuwa ikiboreshwa kwa kasi. China sasa inaongoza duniani katika biashara, uwekezaji zinazotoka, na akiba ya fedha za kigeni," alisema.

  Milioni 60 waondolewa umaskini

  Kutokana na matokeo mazuri ya kiuchumi, kiongozi huyo alisema serikali yake ilikuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kijamii na kisiasa na kwa kasi ilianza kuboresha hali ya maisha ya watu.

  Yeye hasa alisisitiza matokeo mazuri ya juhudi za serikali yake ya kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi wa China tangu yeye alipochukua kiapo cha kuwa rais. Kwa maoni yake, utawala huo unaoongozwa na CPC hatimaye imeshinda vita dhidi ya umaskini.

  "Maendeleo imara yameafikiwa katika mapambano dhidi ya umaskini. Zaidi ya watu milioni 60 wameondolewa kutoka kwenye umaskini na hesabu ya idadi ya watu kwa uwiano imeshuka kutoka asilimia 10.2 hadi asilimia chini ya 4."Rais Xi alidokeza.

  Xi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti,CPC, alisema nchi yake itahakikisha kwamba itakapofika mwaka 2020 wakazi wote wa vijijini wanaoishi chini ya umaskini wataondolewa kutoka hali hiyo na kwamba itaondolewa katika kaunti zote na mikoa maskini.

  "Tuko makini kusaidia watu kujiamini katika uwezo wao wenyewe kujinasua kutoka kwenye umaskini." Alisema.

  Lakini, matokeo mazuri si hayo tu kwani mtazamo wa uchumi umeonyesha mafanikio makubwa katika sekta ya ajira. Xi alisema kwamba ajira imesajiliwa kwa kasi kwani zaidi ya watu milioni 13 walipata kazi kila mwaka mijini.

  Mahusiano ya China na Afrika

  Tangu Rais Xi kuchukua hatamu za uongozi mwaka 2012, China imesaini mikataba mikubwa hasa na nchi zinazoendelea za Afrika. Ni wiki mbili tu zilizopita, ambapo kiongozi huyo alitangaza kuwa serikali yake itatoa rasilimali zaidi za kifedha na vifaa kwa msaada wa kupambana na changamoto za usalama duniani kama vile ugaidi, uhalifu mtandaoni na uhalifu wa kupangwa.

  Xi hasa alisema China itasaidia kwa kujenga na kuboresha mifumo ya mawasiliano na maabara ya uchunguzi wa jinai katika nchi 100 zinazoendelea. Pia alitangaza kwamba serikali yake itaanzisha chuo cha kimataifa cha kutoa mafunzo kwa maafisa 20,000 kutoka nchi zinazoendelea chini ya Wizara ya Usalama wa Umma.

  Msaada huu katika sekta ya usalama ulitolewa baada ya mikataba mbalimbali ambavyo vimetiwa saini kati ya China na nchi za Afrika katika kipindi cha miaka michache iliyopita.

  Katika mwaka 2015, wakati wa mkutano kuhusu ushirikiano wa China na Africa maarufu FOCAC iliyoandaliwa nchini Afrika Kusini, Xi aliahidi kuingiza bilioni 60 dola za Marekani katika bara la Afrika kwa juhudi za kufufua uchumi zilizokwama.

  Baadhi ya miradi yametekelezwa katika nchi nyingi za Afrika hasa zile za Afrika Mashariki. Miradi hayo yanapatikana katika maeneo ya viwanda, miundombinu, kilimo cha kisasa, huduma za kifedha, maendeleo ya kijani, biashara na uwekezaji, uwezeshaji, kupunguza umaskini, ubadilishanaji wa watu-kwa-watu, amani na usalama.

  Mipango hii kwa mujibu wa rais wa China, inalenga kusaidia nchi za Afrika kumaliza vikwazo vya maendeleo tatu ambazo ni miundombinu mbovu, uhaba wa fedha wa kufadhili miradi, kuongeza kasi ya maendeleo ya viwanda na kilimo cha kisasa, na kutambua maendeleo huru na endelevu.

  Na huku uchumi wake ukiinuka, China inatarajiwa kuimarisha juhudi zake za utandawazi katika kipindi cha pili cha uongozi wa Rais Xi Jinping madarakani ambao unatarajiwa kudhibitishwa mwishoni mwa kongamano la wanachama wa CPC wiki ijayo.

  Jumla ya wajumbe 2,307 wanahudhuria mkutano wa chama hicho, ambapo Chama cha Kikomunisti cha China kitawatambulisha viongozi wapya ambao watatoa mwongozo wa nchi katika kipindi cha miaka mitano ijayo huku Rais Xi Jinping akiwa msingi wake.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako