Na Eric Biegon katika Beijing, China.
Kote duniani, wengi wamekuwa makini na kuelekeza macho Beijing siku za hivi karibuni kutokana na mkutano wa kitaifa wa 19 wa Chama cha Kikomunisti cha China. Bila shaka, viongozi wa dunia na watu kutoka kila ngazi ya maisha wanakodolea jicho tukio hilo linalofanyika mara moja kila baada ya miaka mitano linalofanyika kwenye mji mkuu wa China, ikiwa taarifa ni za kuaminika. Lakini, matokeo ya mkutano huo yatakayowekwa hadharani mwishoni yanasubiriwa kwa hamu na gamu zaidi na wote.
Lakini ni kwa nini swala la chama cha kisiasa likafuatiliwa na ulimwengu mzima kwa namna hii?
China katika hali yake ya sasa kinaongozwa na Chama cha Kikomunisti, ambalo ni chama mwanzilishi na mtawala wa Jamhuri ya Watu wa China. Kongamano hili ni halfla ya kuchagua viongozi wa chama kwa kipindi cha miaka mitano yajayo. Hatimaye, mkutano wa kitaifa wa CPC inatarajiwa kutoa mpango wa China wa maendeleo chini ya Rais Xi Jinping mpaka mwaka 2022 na kuendelea.
China inajivunia uchumi wa pili kwa ukubwa duniani na hii, angalau, inaelezea umuhimu wa mkutano huu. Imechangia zaidi ya asilimia 30 ya ukuaji wa uchumi wa dunia mwaka huu peke yake. Hii ni kama kusema China ikipiga chafya, dunia yote upata homa. Katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu Xi Jinping alitaja kanuni 14 za msingi za Ujamaa wenye mtazamo wa Kichina. Sifa moja kuu ya kanuni hizi ni maslahi ya kitaifa ya China katika masuala ya kimataifa.
Muda mfupi baada ya kuchukua uongozi mwaka 2012, rais Xi Jinping alianza kubuni njia mpya ya diplomasia ya nchi yake. Tangu wakati huo, amezungumzia diplomasia maalumu yenye sifa za Kichina kama kanuni ya kutoa mwongozo kwa taifa lake.
Alidumisha wazo hili kwenye taarifa aliyosoma mbele ya wajumbe 2,307 wa Chama cha Kikomunisti waliokuwa wanakutana katika ukumbi wa bunge la taifa hilo wiki iliyopita.
"Tumefanya jitihada ya kila haina katika harakati za kutafuta diplomasia maalum ya nchi yenye sifa za Kichina, hivyo kuendeleza ajenda ya kidiplomasia ya China kwa kina, katika ngazi zote, yenye sura tofauti na kujenga mazingira bora ya nje kwa ajili ya maendeleo ya China." Yeye alisema.
Vipengele muhimu vya diplomasia hii maaluma yenye sifa za Kichina vinasisitiza kwamba China inapaswa kutekeleza sera za kigeni wa kipekee katika kukuza amani na maendeleo. China hata hivyo haiwezi kufikia malengo hayo kwa kutoa kama sadaka haki zake za msingi na maslahi ya taifa..
Lakini kipengele kingine ambalo labda kimefuatiliwa kwa makini duniani linahusiana na harakati za mtindo mpya wa uhusiano wa kimataifa ambalo msingi wake ni mafanikio kwa wote. Hapa, taifa hilo kubwa kiuchumi barani Asia limetangaza mpango kama vile Mkanda Mmoja Njia Moja.
Baada ya kutangazwa na rais Xi tangu mwaka 2013 hatimaye ilizinduliwa Mei 2017, mfumo huu wa Mkanda mmoja njia moja inatumika kama mwongozo wa China kwa ajili ya maendeleo ya kimataifa na uratibu. Mpango huu umeundwa kama jukwaa la kuhakikisha mafanikio ya pamoja, na nchi nyingi zinazoendelea hasa kutoka Afrika, zimejiunga katika mfumo huo.
Hata hivyo hii si kipengele pekee cha diplomasia ya China. China imeahidi kukuza utaratibu mpya wa kimataifa. Hivi karibuni, China imekuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya kidiplomasia. Hii pia ilinakiliwa katika taarifa yake kwa mkutano wa CPC.
Kiongozi huyo wa China alisema serikali yake imefanikisha mpango wa Mkanda mmoja njia moja, kujenga benki ya Asia Infrastructure Investment Bank (AIIB), kuanzisha mfuko wa Silk Road, kuwa mwenyeji wa mikutano mikuu kama vile vya mkanda mmoja njia moja, mkutano wa 22 wa APEC wa viongozi wa kiuchumi, Mkutano wa G20 2016, Mkutano wa BRICS miongoni mwa mengine.
"China inapigania maendeleo ya jamii ya pamoja kwa watu wote. Tumehamasisha mageuzi ya mfumo wa utawala wa kimataifa." Yeye alisema.
Jukumu la China katika mabadiliko ya hali ya hewa pia imeinua nchi hiyo ya Mashariki ya mbali kufikia kilele cha majadiliano ya kimataifa. Muda mfupi baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutangaza kujitoa kwa nchi yake kutoka mkataba wa Paris, China mara moja ilichukua uongozi wa mkataba huu ya Mabadiliko ya tabianchi.
Tangu wakati huo, Beijing imekuwa mwenyeji wa mikutano yenye kiwango cha juu na viongozi kutoka kote duniani ili kujadili jinsi ya kuzindua nishati safi. Kwa kujaza nafasi iliyowachwa wazi na Marekani, China ilitangaza kuwa itatekeleza majukumu yake kikamilifu katika mabadiliko ya hali ya hewa.
Kwa sababu ya mbinu hizi, Rais Xi alisema wazi kwamba ushawishi wa China ulimwenguni, uwezo wa kuhamasisha na kubadilisha misimamo umeongezeka. Kwa maoni yake, China imechangia pakubwa katika kupatikana kwa amani na maendeleo mpya ya kimataifa.
Wengi ndani ya chama hicho cha kikomunisti wanaona diplomasia maalum yenye sifa za Kichina chini ya rais Xi kama wenye hatima mzuri kwa maendeleo katika jamii ya kimataifa huku ikizindua ukurasa mpya katika mahusiano baina ya mataifa ulimwenguni.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |