• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mpango wa Mkanda Mmoja Njia Moja yachochea ukuaji wa soko ya mali nchini Kenya

    (GMT+08:00) 2018-02-16 18:16:34

    KNIGHT Frank sasa inasema soko ya mali isiyohamishika nchini Kenya imefaidika mno kutokana na mpango wa Mkanda Mmoja Njia Moja. Kwa mujibu wa kampuni hiyo ya ushauri wa mali, idadi kubwa ya miradi kwa sasa yanatekelezwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki chini ya udhamini wa mfumo huo unaopendekezwa na serikali ya China.

    Katika ripoti ya hivi karibuni iliyochapishwa na kampuni hiyo iliyopewa jina "New Frontiers", China inaendelea kuwa mshirika mkuu wa Kenya katika biashara na uwekezaji. Kiwango cha ushirikiano, kwa mujibu wa Knight Frank, inaendelea kuongezeka pakubwa ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita wakati nchi hiyo ya Mashariki ya Mbali iliweza tu kuwekeza asilimia ndogo kwa Kenya.

    Hata hivyo kampuni hiyo inasema mpango huo wa mkanda mmoja njia moja itachochea kuinuka zaidi kwa ushirikiano kati ya Kenya na China.

    "Maendeleo ya ujenzi kupitia mpango wa BRI, iwe inayohusiana na miundombinu, vifaa, vitongoji au makazi mapya ya mjini katika miongo ijayo itakuwa kubwa." Ripoti hiyo ilinakili.

    Mkurugenzi mkuu wa Knight Frank Ben Woodhams alibainisha kuwa ushawishi wa China katika soko ya mali isiyohamishika nchini Kenya tayari unaonekana, huku kukiwa na mifano kama vile kununuliwa kwa hisa kwa wawekezaji kutoka China katika jengo jipya maarufu la Two Rivers, mradi wa ujenzi wa makazi unaotekelezwa na kampuni ya Erdermanns mjini Athi River na ujenzi wa jumba la AVIC la matumizi mchanganyiko kwenye sehemu ya Chiromo wilayani Westlands.

    "Kama kitovu katika kanda, Nairobi kwa sasa ni mlango kwa uwekezaji kutoka Mashariki ukingia barani Afrika na kwa kweli tuna msisimko sana kuhusiana na fursa ambayo mpango huu unatoa kwa Kenya." Akasema Woodhams.

    Aidha ripoti hiyo inasema chini ya mfumo wa mkanda mmoja njia moja, Kenya ni miongoni mwa masoko mengine 15, kati ya mataifa 69 wanachama, ambayo imetambuliwa kama nchi zisizo za msingi za mfumo huo.

    Mbali na Kenya na Tunisia, ripoti hiyo inafichua kwamba mataifa 13 zisizo za msingi kwenye BRI zimejiunga na benki ya Asian Infrastructural Investment Bank (AIIB), ambayo inasema ni taasisi muhimu katika kuwezesha mpango huo wa China. Benki ya AIIB ilizinduliwa mwaka 2016 na China ikachangia bilioni 50 dola za Marekani kama mtaji.

    Mkuu wa utafiti katika kampuni hiyo nchini Kenya Charles Macharia anasema idadi ya bidhaa zinazoagizwa na Kenya kutoka China iliongezeka mno kwa karibu bilioni 3.4 dola za Marekani katika mwaka wa 2016, hii ikiwa ni karibu mara tatu ya bidhaa zilizoagizwa mwaka wa 2010, hasa kutokana na uagizaji wa bidhaa hifadhi na vifaa vingine.

    "Idadi hii itaongezeka zaidi kutokana na ujenzi wa miradi kupitia mpango wa BRI wa China, ambayo ni pamoja na reli ya kisasa ya SGR, na bandari ya Lamu pamoja na ile ya ukanda wa Lamu-South-Sudan na Ethiopia (LAPSSET), miradi ambayo kwa kiasi kikubwa zinafadhiliwa na China." Alisema

    Kampuni ya AVIC International Afrika inawekeza milioni 100 dola za Marekani katika jingo lake lililoko Nairobi. Jengo hilo litakuwa kitovu cha shughili za kampuni hiyo barani Afrika.

    Kampuni ya China ya Erdermann pia inajihusisha na mradi wa ujenzi wa makazi utakaogharimu milioni 60 dola za Marekani katika mji wa Athi River iliyoko nje kidogo ya mji mkuu, Nairobi.

    Uwekezaji huo utakuwa wa hawamu ya tatu wa kampuni hiyo katika ujenzi wa Great Wall Gardens, ambayo ni pamoja na ujenzi wa vitengo 2000 vya vyumba vya kulala.

    Ripoti hiyo inabainisha kuwa idadi kubwa ya mataifa yanayoshiriki mpango huo wa mkanda mmoja njia moja yanashuhudia ukuaji wa haraka wa kisasa na ukuaji wa miji na kusababisha kuongezeka kwa mahitaji ya barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, mabomba na miundombinu ya teknolojia.

    Mbali na uwekezaji katika miundombinu, ripoti hiyo inasema ongezeko la kuunganishwa kwa baadhi ya masoko yanayokuwa itasababisha kuongezeka kwa fursa za biashara, na kusaidia kuunganisha mataifa haya na uchumi wa dunia.

    Knight Frank inasema kuwa imebuni "Belt and Road Index" pamoja na "Non-Core Belt and Road Index" ili kuleta mwelekeo mpya na ufahamu zaidi katika uchambuzi wa masuala yanayohusiana na mpango wa mkanda mmoja njia moja.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako