• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • China na  mikakati zaidi  kusaidia  sekta ya afya barani Afrika 

  (GMT+08:00) 2018-02-21 17:02:40

  Na Theopista Nsanzugwanko – DAR ES SALAAM

  SERIKALI ya China imeelezea nia yake ya kuhakikisha kuwa Afrika inakua na afya njema.

  China ina lengo la kusaidia Afrika kukabiliana na changamoto za afya wakati huu ambao ushirikiano baina yao unaingia enzi mpya.

  Serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Xi Jinping imeratibu maeneo kadhaa ambayo serikali yake itaingilia kati ili kuimarisha na kuinua viwango vya ubora katika sekta ya afya barani afrika ambayo kwa muda mrefu imedorora.

  Baadhi ya hatua zilizotangazwa na tume ya taifa ya mpango wa afya na uzazi nchini humo ili kukuza afya katika Afrika, ni pamoja na kusaidia bara kuendeleza mifumo ya afya ya umma.

  Pia sera, utafiti wa magonjwa, kuimarisha kinga na matibabu dhidi ya malaria na magonjwa mengine ya kuambukiza pamoja na kuimarisha afya ya mama na mtoto, bila kusahau afya ya uzazi.

  Akizungumza na waandishi wa habari kutoka Afrika walitembelea nchi hiyo , mkurugenzi wa masuala ya Afrika Yong Feng, alisema kuwa nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi barani Asia pia itashinikiza ushirikiano kati ya hospitali za China na Afrika, kwa kupitia mfumo sawia na ule wa miji dada'Sister Cities'.

  Mfumo wa "Sister Cities" unakuza kubadilishana maelezo na inatazamia kuleta umoja na makubaliano katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na afya.

  "Tunataka kutoa mafunzo kwa madaktari, wauguzi, wahudumu wa afya ya umma na wafanyakazi wa utawala kwa nchi za Afrika." Alisema Yong Feng.

  Pia ,Yong anasema serikali ya Rais Xi inasaidia ujenzi wa vituo vya utafiti vya matibabu vya kikanda na kituo cha kudhibiti ugonjwa wa Umoja wa Afrika, pamoja na kuimarisha maabara na uwezo wa uchunguzi na utafiti wa nchi zinazoendelea katika bara la Afrika.

  Lakini si hayo tu kwani China inasema itaendelea kupeleka kikosi cha matibabu kuelekea Afrika, ikiwa ni pamoja na kikosi cha muda mfupi chenye wataalam wa kliniki wa kutoa huduma za bure za haraka.

  "Malaria bado ni changamoto kubwa kwa Afrika. Ni ugonjwa unaoua. China itatoa dawa aina ya artemisinin kwa Afrika ili kupambana na malaria kwa mamilioni ya watu." Alisema

  Aidha, idara hiyo ya ushirikiano wa kimataifa inasema itaendelea kushinikiza mashirika ya kutoa matibabu na afya kutoka China kuwekeza zaidi barani Afrika.

  Serikali hiyo inayoongozwa na Chama cha Kikomunisti, kulingana na Yong, itaendelea kutia moyo makampuni ya Kichina kupanua shughuli zao na kutoa huduma za afya katika Afrika.

  "Tunatarajia kuboresha miundombinu ya afya katika Afrika kupitia ujenzi, ukarabati na kuandaa vituo vya afya." Bwana Yong alisema.

  Ofisa huyo alisema nchi yake itaendelea kuandaa mazungumzo kuhusiana na afya kupitia mikutano mahsusi ya ushirikiano baina ya China na Afrika kama vile kwenye jukwaa la FOCAC.

  Mwaka 2017, wasomi 350 na maafisa kutoka China na Afrika walikutana jijini Beijing kwa ajili ya mkutano wa kimataifa wa mazungumzo kuhusu ushirikiano wa afya kati ya China na Africa. Wakati wa mkutano huo uliohudhuriwa na rais wa China Xi Jinping, miradi 16 ya utafiti yalijadiliwa. Pia katika ajenda kulikuwa na majadiliano kuhusu dawa muhimu, afya na maendeleo, dawa za jadi, na bidhaa katika sekta ya afya.

  Kwa muda mrefu, China imekuwa ikishiriki katika mikakati mbalimbali ya afya katika bara la Afrika. Tangu mwaka 1963, China imetuma vikosi vya matibabu vilivyohusika katika mipango mbalimbali katika nchi 40.

  Tume hiyo inasema karibu wataalamu 989 wametumwa. Raia zaidi ya 2,100 kutoka Afrika wamepata mafunzo katika mchakato huo. Rekodi pia zinaonyesha kuwa misaada ya elimu ya matibabu zimetolewa. Nafasi 812 kwa mfano, zilitolewa kwa wanafunzi kutoka Afrika mwaka 2015.

  Aidha, China imetoa huduma za upasuaji wa macho bila malipo katika nchi kama vile Botswana, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Mauritania, Ghana, Morocco, Burundi, na Sierra Leone tangu mwaka 2014.

  Mchango mwingine mashuhuri wa China kwa Afrika ni udhibiti wa malaria katika nchi ya Comoros na ugonjwa wa "Schistosoma" nchini Tanzania.

  Mwezi Novemba mwaka jana ,Madaktari Bingwa na wataalamu wa afya 381 kutoka Jeshi la China walifika katika bandari ya Dar es salaam na kutoa matibabu kwa watanzania.

  Watu 10,000 walipatiwa huduma ya matibabu na vipimo kwa madaktari hao waliofika na meli ya uchunguzi na matibabu ya China (Peace of Ark) huku wagonjwa wengi wakibainika kuwa na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, presha na moyo.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako