• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Ni Xi Jinping tena, Bunge laamua

   Abebeshwa matumaini ya China mpya

   Je, Afrika wana chao? Kipi?

  (GMT+08:00) 2018-03-17 18:40:29

  Majaliwa Christopher

  Kuchaguliwa tena kwa Rais Xi Jinping kuongoza China kunafungua ukurasa mwingine mpya wa ushirikiano kati ya nchi hiyo na mataifa mengine hususan nchi za bara la Afrika.

  Hii ni kutokana na sera ya Bw. Xi ya kuimarisha uhusiano wake wa kidiplomasia na nchi zingine duniani huku serikali yake ikiendeleza, ikisisitiza huku ikiamini katika dhana ya usawa na faida kwa wote katika aina yoyote ya ushirikiano.

  Wajumbe wa Bunge la Umma, kwa kujitokeza mamia kwa maelfu kumpitisha kwa kauli moja kuendela kuongoza inaashiria imani kubwa walio nayo juu yake kusimamia maslahi ya China kiuchumi na kusimamia, kutetea na kulinda itikadi, hadhi na hazina za taifa.

  Bw. Xi amechaguliwa mapema leo Jumamosi, ikiwa ni takribani wiki moja tangu Bunge la Umma kupitisha mabadiliko ya Katiba na kuondoa ukomo wa muda wa urais ambao awali ulikuwa mihula miwili.

  Mabadiliko hayo yanampa nafasi Rais Xi kuendelea na urais bila ukomo.

  Bunge la Umma la China ndicho chombo chenye mamlaka ya juu zaidi ya kupitisha sheria na kupigia kura mapendekezo ya mabadiliko ya vifungu vya Katiba.

  Pamoja na kazi zingine, ni chombo ambacho pia kina mamlaka ya juu kabisa ya kumchagua rais, naibu rais, serikali, kamati maalum ya kijeshi pamoja na kumchagua mwanasheria mkuu.

  Kuchaguliwa kwa mara nyingine kwa Bw. Xi ambaye tayari sera zake za kimataifa ziko wazi zikiwa zinaamini katika usawa, zinakuja kipindi ambacho dhana ya diplomasia ya kiuchumi imekuwa inapewa kipaumbele.

  Katika kipindi chake cha miaka mitano iliyopita, Bw. Xi ameonekana akibuni, kuanzisha na kutekeleza mambo mbalimbali ya kiushirikiano duniani ambayo yanalenga hasa katika kukuza uchumi na kufanya dunia kuwa sehemu nzuri ya kuishi.

  Moja ya mambo muhimu kabisa ambayo pia yameanza kuwa na faida ya moja kwa moja yaliyoanzishwa ndani ya kipindi chake ni mradi wa mabilioni ya dola wa Ukanda Mmoja na Njia Moja.

  Huu ni mradi kabambe unaolenga kuunganisha bara za Afrika, Asia na Ulaya katika sekta zote, kikubwa ikiwa ni katika miundombinu ya reli na barabara.

  Hili ni jambo ambalo nchi zote zinazohusika na mradi huu litafurahia zaidi kuona mhasisi wake anarejea tena katika nafasi yake ya urais huku pia ukomo wa muda kukalia nafasi hiyo ukiwa umondolewa.

  Rais Xi alibuni huu mradi mwaka 2013 Kutokana kuwepo kwa changamoto ya kuunganishwa kwa bara moja na nyingine na kusababisha ugumu katika shuguli za biashara na uwekezaji.

  Changamoto hii ilifanya mzunguko wa bidhaa katika nchi mbalimbali kuwa mgumu na wakati mwingine kusababisha kuwa na gharama kubwa.

  Vilevile hali hii ilichangia kuwepo kwa uwezekano mdogo wa kutoa bidhaa sehemu moja ya dunia kwenda nyingine kwa ajili ya kukuza maendeleo na uchumi wa bara hilo na nchi moja moja.

  Kurejea kwa Bw. Xi katika kiti cha urais, kuna maana kubwa sana, zaidi ya yote akiwa msimamizi mkuu wa mradi huu sasa ni wazi pasi na shaka kuwa msukumo mpya utakwepo katika utekelezaji wake.

  Rais Xi pia, kwa bara la Afrika amekuwa ni moja kati ya viongozi kutoka mataifa makubwa duniani aliyewahi kuja mipango mbalimbali yenye kulenga kulikomboa bara hilo kutoka katika changamoto za kiuchumi na kijamii.

  Kuchaguliwa kwake tena kunafufua na kuipa uhaia zaidi mipango na ahadi mbalimbali ambayo kwa nyakati tofauti ametoa kulisaidia bara la Afrika.

  Bw. Xi pia katika kipindi chake hiki anategemewa na viongozi wa Afrika kusimamia utekelezaji wa ahadi yake ya kutoa dola bilioni 60 kufadhili miradi ya maendeleo barani humo.

  Hatua ya Rais Xi ililenga kushugulikia mambo makuuu yanasababisha bara la Afrika lishindwe kusonga mbele kimaendeleo, ikiwemo masuala ya miundo mbinu, ukosefu wa wataalamu walio na ujuzi mbali mbali na ukosefu wa fedha za kuendeleza miradi hiyo.

  Haya ni baadhi ya maeneo makuu ambayo viongozi wa Afrika wanatarajia kuwa awamu nyingine ya Rais Xi yatayapa kipaumbele unaostahili.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako