• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Asilimia kubwa ya Wakenya wathamini China kama mshirika mkuu wa maendeleo

    (GMT+08:00) 2018-04-08 08:50:09

    Na Eric Biegon - NAIROBI

    Asilimia kubwa ya Wakenya wanaamini China ni mshirika mkubwa anayefaidi Kenya. Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na kampuni ya utafiti ya Ipsos, asilimia 34 ya wale waliohojiwa wanaamini kwamba Kenya iko kwenye nafasi nzuri ya kuinuka kiuchumi China ikiwa mshirika wake ikilinganishwa na asilimia 26 ambao wanaamini Marekani ni mshirika mwema kimaendeleo.

    Mtafiti mkuu wa Ipsos Tom Wolf anasema mtazamo mzuri kwa China inatokana na kuongezeka kwa ushirikiano na Kenya katika maeneo ya miundombinu, usalama, elimu, na utamaduni. Sera ya taifa hilo linalotawaliwa na chama cha Kikomunisti ya kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine pia inaonekana kupata uungwaji mkono kutoka kwa Wakenya wengi.

    Kwa ujumla, idhini kutoka raia wa Kenya ya serikali kuendeleza mahusiano kati ya Kenya na China inaendelea kuinuka zaidi. Utafiti huo uliofanywa na Ipsos mwezi uliopita unaonyesha kuwa asilimia kubwa ya Wakenya wamependezwa na ushirikiano kati ya Nairobi na Beijing.

    "Nje ya Afrika Mashariki, tulitaka kujua ni taifa gani la kigeni wananchi wanafikiri ni muhimu zaidi kwa Kenya kuwa na uhusiano nzuri nalo. Katika nafasi ya kwanza ni China, ikifuatiwa na Marekani, iliyomudu asilimia 8 nyuma na wengine wote kupata asilimia ndogo mno ya uungwaji mkono." alibainisha Wolf.

    Utafiti huo unaonyesha kuwa China ilipata uungwaji mkono kutoka kwa wakenya asilimia 34, Marekani ikawa ya pili na asilimia 26, Afrika Kusini ikapata asilimia 5, huku Uingereza ikimudu nafasi ya nne kwa asilimia 4. Ujerumani iliitimisha msururu wa tano bora kwa kujizolea asilimia 2 ya uungwaji mkono.

    "Matokeo haya yanaonyesha kuwa China ilijizolea matokeo chanya licha ya Marekani kuwa taifa kubwa sana 'kukita mizizi' katika nchi hiyo hasa suala la muda wa kuwepo kwake nchini Kenya ikizingatiwa." Aliongeza

    Tom Wolf, ambaye amekuwa mtafiti wa IPSOS kwa muda mrefu, alisema kuwa idadi nzuri ya wale waliohojiwa wanashikilia maoni kuwa Kenya imefaidika mno hasa katika eneo la uchumi tangu nchi hiyo ya Afrika Mashariki kujenga mahusiano ya kibiashara na taifa hilo kubwa kiuchumi katika bara la Asia.

    "Tuliuliza ni nini cha mno wanaodhani ni muhimu zaidi katika mahusiano mazuri kati ya Kenya na China au Marekani. Kwa wote wawili, ni faida za kiuchumi. Asilimia 14 zaidi hata hivyo walitaja China kuleta faida za kiuchumi. Ama kwa kweli, asilimia 95, karibu wote wanataja China kwa suala la kiuchumi. "Akasema Wolf wakati wa kutolewa kwa utafiti huo.

    Lakini ni kwa nini taswira ya Marekani unaendelea kudorora? Ripoti hiyo inasema kuwa hii huenda imetokana na dhana kuwa wanaingilia masuala ya ndani ya nchi marafiki. Hata hivyo, China haina lawama kwa suala hili.

    "Kando na masuala ya kiuchumi, Wakenya wengi wamezungumzia hali ya kuingiliwa hasa kwa njia ya siasa na uchaguzi na mataifa ya nje. Tunajua malalamiko yote ambayo kiongozi wa upinzani Raila Odinga aliyatoa kuhusu Marekani na mabalozi wa magharibi. China haikutajwa kuhusiana na kuingilia uchaguzi wowote. Sidhani China ilisema lolote wakati wa uchaguzi Kenya. Si kawaida kusikia mchina nchini Kenya akitoa maoni kuhusu siasa. "Wolf alifichua

    Asilimia ndogo ya wale waliohojiwa, hata hivyo, bado wanaamini kwamba China na Marekani ni tishio kubwa kwa maendeleo ya kiuchumi na kisiasa nchini Kenya.

    "Katika hili, hakuna tofauti halisi ya takwimu. Lakini tukiangalia sababu, wasiwasi wa wananchi kwa China inahusiana na masuala ya kiuchumi. Wale walio na wasiwasi kuhusu Marekani wanaelezea kuwa msaada katika juhudi za kupambana na ugaidi imesababisha kuongezeka kwa mashambulizi nchini humo. "Utafiti huo ulibaini.

    Mbali na masuala ya ushirikiano kati ya Kenya na nchi marafiki, utafiti huo pia iliangazia mada kama vile uelewa wa haki za binadamu, ugatuzi na mambo ya siasa yalivyo kwa sasa.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako