• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Sanya kuongeza watalii kwa asilimia 10

  (GMT+08:00) 2018-04-13 17:32:23

  Na Majaliwa Christopher, Sanya, China

  Uongozi wa Manispaa ya Sanya, mji maarufu kwa utalii uliopo kusini zaidi mwa China, imetangaza mkakati wake wa kuongeza idadi ya watalii kwa asilimia 10 kila mwaka.

  Sanya, ni mji unaopatikana kando kando ya Bahari ya Kusini ya China katika jimbo la Hainan, takribani kilomita 2,300 kutoka mji mkuu wa Beijing.

  Mji huu wa kitalii maarufu kama 'Hawaii ya Asia' umejizolea umaarufu mkubwa barani Asia na duniani kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii pamoja na hali nzuri ya hewa, ukiachilia mbali ukarimu wa wenyeji wake na kuimarishwa kwa ulinzi na usalama.

  Kwa mujibu wa takwimu kutoka serikali ya manispaa, kwa mwamka wa 2017, watalii waliofika na kulala mjini Sanya walikuwa zaidi ya milioni 18.3 huku wale waliofika kuangalia vivutio mbalimbali na kurudi walikuwa 69,800.

  Pamoja na kupokea idadi kubwa ya watalii katika kipindi cha mwaka jana, serikali ya manispaa ya Sanya imeweka wazi kuwa inachukua hatua mbalimbali kuhakikisha kila mwaka watalii wanaongezeka kwa asilimia zisizopungua 10.

  Akizungumza na wana habari kutoka barani Afrika waliokuwa katika programu maalumu ya mafunzo, Mshauri wa Kamati ya Utalii Bw. Tang Sixian alisema kuwa mwaka uliopita, serikali ilifanikiwa kukusanya jumla ya yuan bilioni 40.6 kutoka kwa watalii waliongia mjini Sanya.

  Bw. Tang alisema kwamba mji huo ambao kwa shughuli za kitalii unafananishwa na mji wa Hawaii umejiwekea mikakati mbalimbali ya muda mfupi na muda mrefu kuhakikisha unakuwa sehemu bora zaidi barani Asia na duniani kwa shughuli za utalii.

  Kwa mujibu wake, hadi sasa, mji wa Sanya wenye ukubwa wa kilomita za mraba 35,400 na wakazi wapatao milioni 9.26, una hoteli za kutosha na huduma muhimu zenye viwango vya kimataifa kwa ajili ya kuwahudumia wageni.

  "Kuna hoteli za kitalii zipatatazo 256 zenye jumla ya vyumba 56,300. Hoteli zenye hadhi ya nyota tano ni 35," Bw Tang alisema na kusisitiza kwamba huduma bora zenye hadhi ya kimataifa ni moja kati ya vipaumbele vyao.

  Aliongeza katika kuhakikisha kuwa watalii wanafurika katika mji wa Sanya ambao pia una ulinzi na usalama wa kutosha, kuna baadhi ya nchi ambazo raia wake wanatembelea Sanya bila masharti ya viza.

  Mji wa Sanya, kwa mujibu wa Bw. Tang, umeweza kutua tuzo mbalimbali huku pia ikitambuliwa na taasisi za kimtaifa kuwa moja ya maeneo salama na bora kutembelea.

  Kwa mfano, mwaka 2017, jarida la New York Times ilichapisha kuwa Sanya ni moja kati ya sehemu 52 bora zaidi duniani kutembelea.

  Akizungumza na CRI Swahili, Bw. Andrei Anatoly kutoka nchini Urusi alisema Sanya ni moja kati ya maeneo mazuri kwake kutembelea kutokana na kuwa na anga ya bluu na mwangaza mzuri wa jua na fukwe nzuri.

  Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa wakati sehemu ya kaskazini ya dunia ikiwa katika majira ya baridi, ambapo hali ya hewa ni baridi sana, theluji inaanguka, upepo wa baridi unavuma na maji ya mito kuganda kuwa barafu, lakini sehemu ya Sanya inakuwa na tofauti kabisa na huwa na hali ya hewa nzuri na ya kipekee.

  Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa mchango wa shughuli za utalii kwa uchumi wa China kwa mwaka 2017 ulikuwa ni asilimia 7.1.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako